BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKAZI WA MTAA WA NYERERE WATAWANYWA KWA MABOMU BAADA YA KUWEKA VIZUIWI KWA MASAA MAWILI BARABARA KUU MOROGORO

Wakazi wa eneo la Kwa Nyerere, kata ya Mafisa wilaya ya Morogoro mkoani hapa waliofunga barabara kuu ya Morogoro–Dodoma kwa saa mbili jana, waliondolewa na polisi kwa kupigwa mabobu ya machozi.

Wananchi hao walikuwa wakitaka Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wafike maeneo hayo kwa ajili ya kusikiliza kero yao ya kupinga kubomolewa nyumba zao.

Kutokana na kufungwa kwa barabara hiyo kwa kupangwa kwa matairi, mawe na vitu mbalimbali, mabasi ya abiria yanayofanya safari za mikoani na magari ya mizigo yalikwama kwa muda katika eneo hilo.

Wananchi hao walifunga barabara hiyo kuanzia majira ya saa 5.30 asubuhi hadi saa 8.00 mchana wakitaka viongozi hao kusitisha ubomoaji wa nyumba zao waliodai umepangwa kufanyika kesho.

Hatua ya wananchi hao kufunga barabara hiyo inatokana na kuvunjwa nyumba tisa za wakazi wa Mtaa wa Nyerere kwa madai ya kuwa wamevamia eneo hilo.Inadaiwa kuwa eneo hilo linamilikiwa na mtu aliyefahamika kwa jina la John Temba.

Wakazi hao wanapinga umiliki huo kwa madai kuwa wenye nyumba hizo wako kihalali na wameishi hapo kwa miaka 10.
Hata hivyo, sakata hilo la uvunjaji wa nyumba lilisitishwa kwa muda na Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini, Abdul Aziz Abood katikati ya wiki.

Wakati wananchi hao wakisubiri sataka hilo kupatiwa ufumbuzi, jana zilitapakaa taarifa katika eneo hilo la Kwa Nyerere kuwa kesho ubomoaji wa nyumba nyingine utaendelea na ndipo wananchi hao walipofanya kikao cha dharura na kuamua kuingia katika barabara kuu kuifunga.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyejitambulisha jina la John Samuel, alisema waliamua kufunga njia ili ubomoaji wa nyumba hizo usitishwe kwa kuwa wao walijenga kwa muda na wana hati miliki.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Diwani wa kata ya Mafisa, Daud Salum alisema nyumba hizo tisa zilivunjwa bila viongozi wa mtaa wala kata kupewa taarifa.

Alisema baada ya hapo walienda mahakamani na kupata zuio la kubomoa nyumba nyingine katika eneo hilo mpaka kesi ya msingi isikilizwe.

Alisema kuwa kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Mei 31, mwaka huu lakini wameshangaa kuwepo kwa taarifa kuwa kesho kuna nyumba nyingine zinabomolewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Urlich Matei, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanawashikilia watu kadhaa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: