Juma Mtanda,Morogoro.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero na mwanasheria wa halmashauri hiyo wanatarajiwa kuburuzwa katika mahakama kuu kitengo cha sheria na katiba ndani ya siku saba au 14 kwa madai ya kuvunja katiba ya nchi kwa kutoza tozo ya ushuru wa mazao baada ya serikali kufuta tangu mwaka 2002.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa kizuizi cha tozo ya ushuru wa mazao ya sh2,500 kwa kilo 1,00 eneo la Doko kata ya Idete barabara kuu ya Mlimba-Ifakara kinyume na sheria kwa wafanyabiashara na wakulima wa mazao.
Akizungumza na wananchi wakati wa kuvunja kizuizi cha Doko katika kata hiyo wilayani hapa, Msaidizi wa sheria mkoa wa Morogoro kwa wilaya za Kilombero na Ulanga (LHRC), Godfrey Lwema alisema kuwa anakusuduia kuwaburuza katika mahakama mkuu mkurugenzi na mwanasheria wa halmashauri hiyo.
Lwena ambaye ni Diwani wa kata ya Namawala amesema ana kusudio hilo linatokana na viongozi hao kuvunja sheria za nchi kwa kuweka kizuizi kinyume na sheria ya serikali za mitaa baada ya serikali kufuta vizuizi vya mazao ya kilimo vinavyowekwa kwa ajili ya kutoza ushuru chini ya sheria fungu la 168(C) katika tangazo Na.130 la Mei mosi la mwaka 2002.
Katika tangazo hilo serikali limefuta vizuizi vilivyowekwa na mamlaka za wilaya kwa nia ya kuziwezesha kukusanya ushuru wa mazao vinaondolewa na badala yake halmashauri za wilaya na vijijini zinapaswa kubuni utaratibu mwingine wa kukusanya ushuru wa mazao bila kutumia vizuizi.alieleza Lwena.
“Mkurugenzi mtendaji na Mwanasheria wake wamevunja kanuni na taratibu kwa kukiuka katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria".alisema Lwena.
Ofisi ya Waziri mkuu kupitia waziri wa Tamisemi imwagize waziri mwenye dhamana kumchukua hatua za kisheria dhidi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero kwa kufanya kazi nje ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Akitaja mashtaka hayo, Lwena alisema kuwa mwanasheria wa halmashauri hiyo atashtakiwa kwa kushindwa kutoa ushauri wa kisheria juu ya kufutwa kwa sheria ya tozo ya mazao wakati mkurugenzi mtendaji akifanya kazi nje ya misingi ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Lwena aliongeza kwa kunukuu vifungu hivyo vya sheria kuwa mamlaka ya wilaya vilipigwa marufuku kwa kuweka kizuizi au kuendelea kutumia vizuizi vilivyopo kwa madhumuni ya kukusanya ushuru wa mazao tangu Mei mosi mwaka 2002.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero, Godfrey Sanga alisema kuwa wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi na misingi yake.
Sanga alisema kuwa katika utekelezaji wa mpango wa makusanyo ya ushuru wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero unazingatia tangazo la serikali Na.6 la januari 8 mwaka 2010 kama lilivyorekebishwa na tangazo la serikali Na.294 la mwaka 2012 kifungu cha 4(1) (D) kuwa ushuru wa mazao utatozwa kwa 5% ya bei ya kuuzia.
0 comments:
Post a Comment