UKIOA MWANAFUNZII AMA KUMPACHIKA UJAUZITO MIAKA 30 JELA INAKUHUSU.
SERIKALI ya Awamu ya Tano inagharamia elimu msingi ili kutoa fursa ya mtoto wa kitanzania bila kujali jinsi yake, aelimike kwa kupata maarifa na ujuzi wa kujitambua na kujiweka sawa kuzikabili changamoto katika maisha yakiwemo mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Ili azma ya serikali itimizwe lazima wanafunzi waliokusudiwa waipate elimu hiyo bila vikwazo na wapate fursa hiyo kwa ajili ya ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla. Lakini watoto nchini, hasa wa kike wamekuwa wakikabiliana na changamoto nyingi kufikia malengo ya kupata elimu, zikiwemo mimba na ndoa utotoni.
Inadaiwa kuwa, Tanzania ni moja ya nchi zinazokabiliwa na changamoto ya ndoa za utotoni zinazosababishwa na mila potofu, elimu duni, umasikini unaosababisha wazazi kuwa na tamaa za kupata mali kukidhi haja zao pamoja na sheria kandamizi.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) mwanzoni mwa mwaka huu zinaonesha kuwa Tanzania ni nchi ya tatu inayoongoza kwa ndoa za utotoni duniani.
Mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinyanga, Tabora, Mara, Dodoma, Lindi, Mbeya, Morogoro, Singida, Manyara, Mtwara, Pwani, Arusha, Kilimanjaro, Kigoma, Dar es Salaam na Iringa.
Taarifa ya UNFPA inaonesha kuwa watoto 13,822 waliozaliwa kati ya mwaka 2005 na 2010 ifikapo 2030 watakuwa wameolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18. Ripoti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaonesha kuwa kila mwaka wasichana 8,000 wanapata ujauzito wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi 3,000 na 5,000 wa sekondari.
Wadau wa haki za watoto wamekuwa wakihimiza sheria kandamizi zirekebishwe ikiwemo Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kifungu cha 13 kinachoruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya mahakama.
Sheria hiyo inaruhusu pia mtoto mwenye umri wa miaka 15 kufunga ndoa kwa ridhaa ya wazazi na mtoto wa kiume anayefikisha miaka 18 anaweza kuoa.
Licha ya kuwepo kwa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, inayotafsiri kwamba mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18 bado Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inaruhusu watoto wa kike chini ya miaka 18 waolewe hivyo kumaanisha kuwa inapingana na sheria zingine.
“Ndoa ya mwanangu ni ya kanisani (Kanisa la Anglikana). Ili kuweza kuwafungisha ndoa tumelazimika kudanganya umri wa binti kwa kueleza kuwa ana miaka 18 ingawa kwa uhalisia alikuwa na miaka 14,” ni kauli ya Emma, mama mkwe wa Jenny mwenyeji wa kijiji cha Kidoka wilayani Chemba alipohojiwa mwaka jana wakati utafiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA).
“Sisi ni wakristo, kwa taratibu ya dhehebu letu hairuhusiwi kuzaa nje ya ndoa, kwa kufanya hivyo unatengwa na kanisa. Kwa vile binti (Jenny) alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kijana wangu (24) tuliamua wafunge ndoa, lakini ili ndoa hiyo ifungwe kanisani tumelazimika kudanganya umri,”anasema.
Emma anawakilisha baadhi ya jamii ya Watanzania ambao bado wanaendeleza ndoa za utotoni huku wakitambua kuwa suala hilo si zuri kwa wasichana.
“Tulitumia nafasi ya kanisa kuwa na padri mpya ambaye hawajui vizuri waumini wake, tukadanganya umri wa binti ili afungishwe ndoa. Angekuwa yule padri wa zamani ningekuwa ngumu maana anajua waumini vilivyo. Hivyo cheti cha ndoa kimeandikwa ana miaka 18,”anasema.
Tafiti zinabainisha kuwa baadhi ya wazazi wanawaoza watoto wa kike mara baada ya kuhitimu darasa la saba kwa kuwa hakuna sheria ya kumlinda mtoto. Ili kuondoa changamoto hiyo Bunge la Tanzania limepitisha muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Elimu.
Rais Dk John Magufuli akisaini itakuwa sheria itakayotoa adhabu ya miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari.
Adhabu hiyo ipo katika kifungu cha 60 cha Sheria ya Elimu kinachokusudiwa kufanyiwa marekebisho kwa kuongezewa vifungu vinavyopiga marufuku ndoa kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.
Kifungu cha 60 A kifungu kidogo cha kwanza ambacho ni kipya kimeeleza kuwa itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira yoyote yale kwa mtu yeyote kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya sekondari au ya msingi.
Kwa mujibu wa kifungu hicho kipya, mtu yeyote atakayekiuka kifungu hicho, sheria hiyo imeweka wazi kuwa atakuwa ametenda kosa na adhabu yake itakuwa kufungwa jela miaka 30.
Sehemu ya tatu ya sheria hiyo imeeleza kuwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari atakuwa ametenda kosa, na adhabu yake ni kufungwa jela miaka 30.
Sheria hiyo imekwenda mbali zaidi kwa watu watakaokutwa na hatia ya kushawishi mwanafunzi wa shule ya msingi na shule ya sekondari aoe au aolewe wakati akiendelea na shule. Mhusika atakuwa amefanya kosa na adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni tano au kwenda jela miaka mitano au vyote kwa pamoja.
Sheria hiyo imewataka wakuu wa shule na walimu wakuu kutunza taarifa na kuziwasilisha kwa kamishna wa serikali au mwakilishi wake itakayoeleza kwa kina matukio ya ndoa na mimba za wanafunzi na hatua zilizochukuliwa za kisheria dhidi ya waliokutwa na hatia.
Awali, adhabu iliyotamkwa katika sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika kuwa na kosa atatozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni kosa la pili anatozwa faini ya Sh 500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju anasema sheria hiyo pia imewalenga watoto walio chini ya miaka 18 bila kujali wako shuleni au hawapo shule.
Wabunge wameonesha furaha kuhusu Sheria ya Elimu inayohusu adhabu ya miaka 30 jela. Hata hivyo, baadhi yao wametoa angalizo la kutaka kupimwa kwanza DNA kabla ya kutoa hukumu na wengine wanataka wanaokutwa na hatia pia wachapwe viboko.
Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM) anapongeza marekebisho hayo na kutaka adhabu ya miaka 30 iongezwe na kuchapwa viboko 12 kila mwezi mpaka aliyehukumiwa anamaliza kifungo kwa kuwa wahalifu hao wamezoea maisha ya gerezani.
Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu (CCM) anasema, pamoja na serikali kuja na marekebisho hayo pia iangalie namna ya kukabiliana na utoro shuleni ili wanafunzi wapate elimu.
Akijibu hoja kuhusu kutumika kwa vipimo vya vinasaba (DNA), Masaju anasema kwa sasa utaratibu huo utatumika mahakamani na kwamba, waendesha mashitaka watahakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi kwa kuwa Tanzania haina uwezo wa kupima DNA mtoto akiwa tumboni.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Eda Sanga anasema marekebisho ya Sheria ya Elimu yaliyofanywa mwelekeo mzuri katika kulinda watoto hasa wa kike.
“Ingawa kuna wanaokosoa kuwa marekebisho hayo hayaelezi namna ya kumlea mtoto atakayezaliwa baada ya mtu aliyempa mimba au kuoa mwanafunzi akiwa amefungwa, lakini sisi tunaona ni mwelekeo mzuri.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment