VIGOGO KUKUMBWA KATIKA KASHFA 10, MAHAKAMA YA MAFISADI TANZANIA.
WAKATI mchakato wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi ukiendelea, kuna taarifa kuwa vigogo kadhaa waliohusika na kashfa mbalimbali zikiwamo 10 zilizolikumba taifa kwa nyakati tofauti ndiyo watakaokuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuguswa na rungu la mahakama hiyo itakayokuwa chini ya Mahakama Kuu.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa miongoni mwa vigogo hao, ni wale wote ambao uchunguzi unaoendelea kufanywa na vyombo mbalimbali vya dola utabaini kuwa wanahusika katika kashfa zenye thamani ya mabilioni ya fedha.
Baadhi zikiwa ni za escrow, utoroshaji wanyama hai wakiwamo twiga, ulipaji mishahara hewa kwa watumishi hewa wa umma, ufisadi kwenye miradi mbalimbali ya halmashauri na pia ufisadi uliotokea kwenye taasisi mbalimbali za umma zikiwamo za Bandari, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mamlaka ya Bandari na pia Mamlaka ya Kodi (TRA), likiwamo sakata la hivi karibuni la kuwapo kwa mtu aliyekuwa akijiingizia Sh. milioni 7 kila dakika.
Chanzo kutoka ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria kiliiambia Nipashe jana kuwa vigogo wengine walio katika uwezekano mkubwa wa kutangulizwa katika mahakama hiyo wanaweza kuwa wahusika wa kashfa kama ya Lugumi pindi uchunguzi ukikamilika na kuonekana kuwa kuna watu walijinufaisha binafsi, mikataba ya kifisadi katika halmashauri mbalimbali nchini na pia manunuzi hewa ya bidhaa mbalimbali katika taasisi nyingine za umma.
“Mahakama hii itaanza kazi kwa kishindo… kuna kashfa zaidi ya 10 zinaendelea kuchunguzwa na pindi kazi rasmi itakapoanza, kutakuwa na mshindo mkuu,” chanzo kiliiambia Nipashe jana.
Chanzo hicho kilisisitiza kuwa makosa yatakayoshughulikiwa, kama sheria hiyo itaridhiwa na Rais na kutangazwa kwenye gazeti la serikali, ni yote yanayoangukia kwenye rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi na kulisababishia taifa hasara ama uharibifu wa mali au raslimali zenye thamani isiyopungua Sh. bilioni moja.
Ilielezwa kuwa kashfa nyingine zitakazowatanguliza vigogo kortini ni zile zinazohusiana na sheria ya misitu, ikiwamo ya usafirishaji holela wa magogo nje ya nchi na uharibifu wa misitu.
“Makosa kwa mfano ya kashfa ya kama ya Escrow, utakatishaji fedha (mabilioni ya Uswisi), mishahara hewa uchunguzi wake ukishafanyika na kubainika, watuhumiwa wake ndiyo watafikishwa katika mahakama hiyo haraka iwezekanavyo,” kiliongeza chanzo hicho.
Nipashe ilielezwa zaidi kuwa hadi sasa, tayari vyombo vya uchunguzi kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) vinaendelea na kazi kwa kasi ili kutimiza lengo la kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wa ufisadi wanafikishwa kwenye mahakama hiyo.
Aidha, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka inaendelea vyema pia na kazi ya kujifua kwa ajili ya kuhakikisha kuwa majada yote ya uchunguzi wa kesi hizo yanashughulikiwa kwa umakini ili mwishowe haki itendeke na kutimiza ahadi ya Rais John Magufuli.
Wakati wa uchaguzi mkuu kuwa serikali yake haitawavumilia mafisadi wala kuwaogopa bali itawafikisha mahakamani na kuwafunga wale wote watakaokutwa na hatia.
Wiki iliyopita, Jaji Mkuu, Mohammed Chande Othman, alinukuliwa akisema kuwa Mahakama Maalumu ya Uhujumu Uchumi na Ufisadi (maarufu kama Mahakama ya Mafisadi), itaamua kesi kwa muda usiozidi miezi tisa na kwamba itaanza na majaji 14.
Aidha, alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa kazi ya uendeshaji kesi inafanyika kwa ufanisi, wameandaa mafunzo maalumu kwa majaji 14 kwenye Chuo cha Mahakama Lushoto mkoani Tanga ili kupeana mwongozo juu ya uendeshaji wa mahakama hiyo.
Jaji Mkuu alisema, kesi zitakazoendeshwa katika mahakama hiyo ni zile ambazo upelelezi wake umekamilika ili uamuzi utolewe mapema. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupambana na uhalifu huo. Aidha, tayari Serikali imetenga Sh. bilioni 2.5 kwenye bajeti yake 2016/17 kwa ajili ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.
1. VIGOGO WA ESCROW
Hii ni kashfa iliyotikisa nchi mwaka 2014 kwa kuhusisha uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow na kusababisha baadhi ya mawaziri na wenyeviti wa kamati za bunge kuwajibishwa.
Akaunti ya fedha hizo ilifunguliwa na Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2004 baada ya kuwapo kwa mgogoro kati ya IPTL na Tanesco kuhusu gharama ya uwekezaji ‘Capacity Charge’. Vigogo kadhaa walihusishwa na kashfa hiyo na baadhi walivuliwa nyadghifa zao, wakiwamo mawaziri.
2. MKATABA WA LUGUMI
Hii ni kashfa nyingine inayodaiwa kuwa huenda ikapeleka vigogo kadhaa katika mahakama ya mafisadi. Taarifa zinadai kuwa hadi sasa, uchunguzi bado unaendelea kuhusuiana na sakata hilo linalohusisha matumizi yenye shaka ya zaidi ya Sh. bilioni 30 katika jeshi la Polisi.
Inadaiwa kuwa Jeshi la Polisi liliangia mkataba wa thamani wa Sh. bilioni 37 na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd wa kusambaza na kufunga mitambo ya kuchukulia alama za vidole katika vituo vya polisi 108 lakini ni vituo 14 tu ndivyo vilivyofungwa huku malipo ya zaidi ya asilimia 90 yakiwa tayari yamelipwa kwa kampuni hiyo.
Kashfa kuhusu mkataba iliibuliwa Aprili 5 mwaka huu na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshi Hilary wakati wakipitia mahesabu ya jeshi hilo na kukuta mapungufu hayo na kuwaeleza kuleta makubaliano ya mkataba huo Aprili 11, mwaka huu.
3. MABILIONI USWISI
Ni mojawapo ya kashfa iliyowahi kutisa nchi baada ya kuwapo kwa madai kuwa kuna baadhi ya viongozi maarufu pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania ambao wameficha takribani Sh.trilioni 1.3 katika benki za Uswis.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Uswisi iliyotolewa Juni 2012, kuna Watanzania wamehifadhi kiasi cha dola za Marekani milioni 178 katika benki mbalimbali nchini Uswis.
4. MAKONTENA BANDARI
Rungu la majaji wa Mahakama ya Mafisadi huenda pia likawashukia baadhi ya vigogo wa waliohusika na utoroshwaji wa makontena kadhaa katika bandari ya Dar es Salaam bila ya kulipiwa kodi na ushuru lakini hadi sasa hawajafikishwa mahakamani kutokana na uchunguzi kutokamilika kiasi cha kuwagusa.
Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani, uongozi wake ulianza kuibua matukio mbalimbali wa ufisadi ikiwamo eneo la Banadarini huku washirika wake wakiwa ni viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), mawakala pamoja wa forodha pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Upotevu wa makontena 329 ndiyo ulioanza kuibuliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Novemba 27, mwaka jana baada ya kufanya ziara ya ghafla bandarini na kubaini makontena hayo yalitolewa bandari kavu bila ya kulipiwa kodi.
Upotevu huo ulisababisha baadhi ya vigogo wa TRA, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na makamishana wengine kusimamishwa kazi na baadaye kupandishwa mahakamani akiwamo aliyekuwa kamishna wa Forodha Tiagi Masamaki.
Desemba 3, mwaka jana Waziri Mkuu Majaliwa alibaini upotevu wa makontena mengine 2,431 yaliyoondolewa katika bandari kavu bila ya kulipiwa ushuru wa bandari, pamoja na ugunduzi wa upotevu wa makontena 11,049 na magari 2,019.
5. VITAMBULISHO VYA TAIFA
Hii ni mojawapo ya taasisi inayotajwa kuwa baadhi ya vigogo wake wanaweza kufikishwa kwenye Mahakama ya Mafisadi. Hali hiyo inatokana na madai kuwa yapo matumizi kadhaa yenye utata wakati wa kutekeleza mradi wa vitambulisho vya taifa.
Januari 25, mwaka huu Rais Magufuli alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Nida Dickson Maimu, pamoja na Mkurugenzi wa Tehama wa Mamlaka hiyo, Joseph Makani, Afisa Ugavi Mkuu Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria Sabrina Nyoni na Afisa usafirishaji, George Ntalima.
Kusimamishwa kwa viongozi hao kulitokana na madai ya kuwapo kwa matumizi mabaya ya Sh. bilioni 179.6 huku kazi ya uandikishwaji na utolewaji vitambulisho ukiwa unasuasua.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliagiza Mamlaka ya Ununuzi ya Umma (PPRA) kufanya ukaguzi wa vifaa vilivyonunuliwa na Nida.
Mbali na magizo hayo, Pia Rais Magufuli aliiagiza ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mahesabu ukiwamo ukaguzi wa ‘Value of Money’ pamoja na Takukuru kufanya uchunguzi kama kulikuwa na viashiria vya rushwa.
6. BODI YA MIKOPO
Baadhi ya vigogo wa katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nao huenda wakawa miongoni mwa watuhumiwa watakaopandishwa kizimbani katika mahakama hiyo baada ya kubainika kwa ufisadi mkubwa wa mabilioni ya fedha
February 16, mwaka huu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisitisha ajira ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega.
Mbali na Nyatega, pia Prof. Ndalichako aliwasimamisha kazi pia wakurugenzi wengine watatu ambao ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusuph Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja pamoja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kubainika kuwapo kwa upungufu mkubwa wa usimamizi wa fedha katika matumizi yaliyofanywa mwaka 2013.
7. MIKATABA MIBOVU
Hili ni eneo jingine ambalo huenda likawapeleka viongozi wengi katika Mahakama ya Mafisadi. Hadi sasa, kuna mikataba kadhaa mikubwa inayoligharimu taifa katika maeneo mbalimbali na pia kuna vigogo wengi wanatajwa kunufaika katika mikataba ya utata iliyoingiwa na halmashauri za miji, manispaa na majiji nchini.
Wakati akiweka jiwe la msingi katika kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi Machi 18, mwaka huu, Rais Magufuli alitoa mfano wa IPTL kama moja ya mikataba iliyoisababishia Serikali matatizo makubwa.
8. MABEHEWA FEKI
Katika kashfa hii, Serikali iliingia hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 230 baada ya kusadikiwa kuagiza mabehewa 274 kutoka India yaliyodaiwa kuwa ni feki. Inadaiwa uchunguzi mkali bado unafanyika ili ikithibitika kuwapo wahusika wa ununuzi huo ambao hawajafikishwa mahakamani, nao wachukuliwe hatua za kisheria.
Mabehewa hayo yalikaguliwa na Waziri mkuu Desemba 8, 2014 yaliingia katika kashfa baada ya kudaiwa kuanguka wakati yakifanyiwa majaribio.
Ilidaiwa kuwa mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayoulisainiwa kati ya TRL na kampuni ya Hindusthan Enginneering and Industries Limited ya india kwa thamani ya jumala ya Dola za Kimarekani 28,487,500.
Mkataba huo ulisainiwa kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India 21 Machi 2013. Bunge lilunda kamati ambayo ilikwenda hadi India kuichunguza kampuni ambayo ndiyo watengenezaji wa mabehewa hayo mabovu na kubaini kampuni hiyo iliyopewa zabuni ilikuwa haina sifa.
Pia kamati hiyo ilieleza kuwa kulikuwa na uzembe kwa watendaji wa shirika la reli ya Kati TRL ambayo imepelekea hadi kununiliwa kwa mabehewa hayo.
9. MISHAHARA HEWA
Ulipwaji wa mishahara hewa umegundulika baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani na hadi kufikia Juni 23, Rais Magufuli alisema kuwa wameshawabaini wafanyakazi hewa 12,446 waliokuwa wanalipwa zaidi ya Sh. bilioni 1.8 kila mwezi.
Hili ni eneo lingine ambalo baadhi ya wahusika huenda wakapandishwa katika mahakama ya mafisadi kwa kosa la kuisababishia hasara serikali.
Uwapo wa wafanyakazi hewa ndiyo uliomfanya Rais Magufuli atoe agizo la kusitishwa kwa ajira serikalini kwa mwezi mmoja hadi pale kazi ya kuwabaini na kuwaondoa wafanyakazi hewa itakapokamilika.
Rais Magufuli wakati akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alieleza kuwa Benki ya NMB inatakiwa kurudisha Sh. bilioni saba ilizowalipa wafanyakazi hewa 2,800 kama mafao ya kustaafu
10. ULAJI EFD’S
Hii ni kashfa ya aina yake ndani ya TRA, ikihusisha taarifa kuwa kuna mtu alikuwa akiingiza zaidi ya Sh. milioni 7 katika kila dakika kupitia mashine za stakabadhi za kielektroniki (EFD’s). Uchunguzi kuhusiana na kashfa hiyo iliyoibuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli.
WASOMI WANASEMAJE
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia kutoka Chuo cha Diplomasia, Dk. Israel Sosthenes alisema kufahamu kuwa kuna Mahamaka ya Mafisadi ni jambo zuri na anaamini kuw a itahukumu watuhumiwa wote kwa haki.
Naye Mtaalamu wa Sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema haoni mantiki ya kuanzishwa kwa mahakam hiyo.
“Ni ufisadi wa aina gani utakaompandisha mtu kizimbani, mahakama ina mamlaka gani, watu gani watakaopandishwa, pia hatujawahi kusikia malalamiko ya mahakama zingine kuwa zimeshindwa kusikiliza kesi za watu hao hadi mahakama nyingine ianzishwe,” alisema Profesa Baregu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwohede, Justa Mwaituka alisema uanzishwaji wa Mahakama ya mafisadi malengo yake ni mazuri kwa ajili ya kujenga nidhamu na hivyo kila mwananchi anapaswa kuiunga mkono.
0 comments:
Post a Comment