PROFESA IBRAHIM LIPUMBA HAPA NDIPO ALIPOLIKOLOGA NDANI YA CHAMA CHA WANANCHI (CUF)
Profesa Ibrahim Lipumba.
KATIBA YA CHAMA YA 1992 (TOLEO LA 2014)
UTARATIBU WA KUJIUZULU:
117. (1) Kiongozi yeyote wa chama anaweza kujiuzulu uongozi wake wakati wowote ule.
(2) Kiongozi atajiuzulu kwa kuandika barua na kuweka saini yake kwa katibu wa mamlaka iliyomchagua au kumteua na kiongozi huyo atahesabiwa kuwa amejiuzulu ikifika tarehe aliyoainisha katika barua yake kuwa atajiuzulu pindipo akikubaliwa na mamlaka iliyomchagua au iliyomteua, au kama hakuainisha tarehe ya kujiuzulu kwake basi atahesabiwa amejiuzulu mara baada ya katibu wa mamlaka iliyomteua au kumchagua kupokea barua hiyo na mamlaka iliyomchagua au kumteua kukubali.
UTARATIBU WA KUFIKIWA MAAMUZI:
115. Ila pale ambapo imeelezewa vinginevyo katika Katiba hii:-
(1) Uamuzi wowote ule utafikiwa kwa kura za wajumbe ambazo zinapita nusu ya wajumbe waliohudhuria katika kikao hicho.
(2) Kijifungu cha (1) cha kifungu hiki hakitoathiri uamuzi unaofikiwa kwa muafaka.
(3) Katika shughuli za uchaguzi wowote ule kura zitakuwa za siri.
(4) Masharti ya kifungu hiki hayotoathiri masharti ya vifungu vingine vyovyote vya Katiba hii ambavyo vimetoa masharti ya upigaji kura juu ya suala lolote.
UCHAMBUZI:
Ibara ya 117 imeweka wazi utaratibu ambao utatumika kwa kiongozi wa Chama kujiuzulu.
Prof. Ibrahim Lipumba alikamilisha hatua zote zilizotajwa ikiwa ni pamoja na kuandika barua, kuitia saini na kuifikisha kwa Katibu wa mamlaka iliyomchagua huku akitaja tarehe 5 Agosti, 2015 kwamba ndiyo tarehe ambayo atakuwa amejiuzulu.
Hatua iliyobakia ilikuwa ni kwa mamlaka iliyomchagua kukubali au kukataa kujiuzulu kwake; hatua hiyo ilikamilishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa ambayo ndiyo mamlaka iliyomchagua uliofanyika tarehe 21 Agosti, 2016 ambapo wajumbe 476 walimkubalia kujiuzulu kwake na wajumbe 14 walimkatalia, huku wajumbe wengine wapatao 188 wakikataa kupiga kura (abstained).
Kudai kwamba uamuzi huo ulipaswa uwe kwa kura ya siri ni kutapatapa na kupotosha kwa makusudi. Ibara ya 115 imetofautisha namna ya kupiga kura katika mambo yanaohitaji "uamuzi" yale yanayohusu "uchaguzi".
Neno "uamuzi" linatumika kwenye ibara ndogo ya (1) na (2) ambapo ibara ndogo ya (2) pia imetoa nafasi ya uamuzi kwa njia ya maafikiano (decision by consensus). Neno "uchaguzi" linatumika kwenye ibara ndogo ya (3) ambapo ndipo panapotajwa kura ya siri.
Utaratibu wa kufikia uamuzi kwa kura za kunyoosha mikono ndiyo utaratibu unaotumika katika Mikutano Mikuu ya Taifa yote ya CUF takea kuasisiwa kwake mwaka 1992 (ukiondoa wakati wa uchaguzi ambapo kura za siri hutumika).
Mfano mzuri wa kupiga kura kwa kunyoosha mikono katika kufikiwa kwa uamuzi ni huu wa kwenye picha ambayo ni katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa mwaka 2014 ambapo hapa Abdul Kambaya na Thomas Malima wanapiga kura kwa kunyoosha mikono.
Na hata katika Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa juzi tarehe 21 Agosti, 2016 wajumbe hao hao walipiga kura kwa njia ya kunyoosha mkono katika kumpata Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, utaratibu ambao ndiyo umekuwa ukitumika katika Mikutano Mikuu yote ya Taifa ya CUF na kufanywa kuwa ndiyo kanuni (convention kwa lugha ya kisheria ya Kiingereza).
HITIMISHO:
Uamuzi wa Prof. Ibrahim Lipumba kujiuzulu umekamilishwa kwa Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa kukubali kujiuzulu kwake.
Hatua iliyobaki ni kukamilisha uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama (Taifa), hatua ambayo itakamilishwa karibuni
0 comments:
Post a Comment