Juma Mtanda, Morogoro. jphtjuma@gmail.com
Kikundi cha vijana cha Michumvini kinachojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya mbogamboga kimempigia magoti mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdullaziz Abood kwa kupewa pembejeo za uzalishaji wa zao la mbogamboga baada ya kuacha kujihusisha na masuala ya uhalifu mkoani hapa.
Wakizungumza na gazeti hili mjini hapa, vijana hao walisema kuwa wameacha kujihusisha katika matukio ya uhalifu na badala yake watajikita katika shughuli za uzalishaji wa ya mbogamboga.
Walisema bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo ikiwemo mbengu bora na mbolea.
Mmoja wa vijana hao, Ayubu Hamza (36) alisema changamoto kubwa ni kupata mbegu bora za mbogamboga za spinachi, vitunguu, kabichi, sukumawiki na nyinginezo.
“Vijana tumefanya mapinduzi makubwa kwani awali tulijihusisha sana katika uhalifu kama ubakaji, wizi, utumiaji wa madawa ya kulevya lakini tumeachana nayo na kujikita katika uzalishaji wa mazao ya mbogamboga,”alisema Hamza.
Hamza alisema kuwa endapo mbunge wao, Abdullaziz Abood atawawezesha kupata pembejeo itawasaidia kusonga mbele kimaendeleo na kuzalisha mbogamboga zenye ubora.
Kiongozi wa kikundi hicho kilichopo mtaa wa Ukota kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Juma Chadadi (45) amewapokea vijana tano kati ya vijana 75 kutoka katika tawi la chama cha Mapinduzi (CCM) na kuungana nao katika ujasiliamali wa uzalishaji wa mbogamboga.
Chadadi alisema kuwa mwanzo baadhi ya vijana walijenga tabia ya kuunda maskani na kujishughulisha na unywaji wa pombe ya moshi (Gongo), uvutaji wa madawa ya kulevya kama bangi, kufanya matukio ya uhalifu yakiwemo wezi, ubakaji na kupora mali lakini alijitahidi kuwabadilisha na kujiingiza katika ujasiliamali.
“Kulikuwa na kijiwe cha vijana cha kuvuta bangi na kupanga matukio ya uhalifu lakini sasa hivi kijiwe hicho kimegeuzwa kuwa kijiwe cha mfano cha vijana wajasiliamali kwa kuzalisha mazao ya mbogamboga,”alisema Chadadi.
Awali uongozi wa kikundi hicho, waliomba msaada wa mwandishi mkoa wa Morogoro, Hamida Shariff kutafuta wadau akiwemo Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdullaziz Abood ili kuwapatia pembejeo,kupata eneo, karakana ya uselemala na sehemu ya kufyatulia tofali.CHANZO/MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment