BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

YALIYOJIFICHA NYUMA YA PANZIA KWA CHAMA CHA WANANCHI CUF NA PROFESA LIPUMBA



CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeanika chanzo cha kuibuka kwa vurugu katika mkutano mkuu maalum huku kikisisitiza kuwa mchakato wa kujaza nafasi za mwenyekiti na makamu wake zilizo wazi uko palepale.

Aidha, chama hicho kimesema kimeshamaliza suala la kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kutokana na wajumbe wengi kuridhia kung’atuka kwake katika nafasi ya uongozi.

CUF juzi ilifanya mkutano mkuu maalum wa taifa jijini Dar es Salaam, lakini ukavunjika baada ya kutokea vurugu.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano wa CUF, Salim Biman, ilieleza kuwa baraza kuu la uongozi la taifa la chama hicho limejiridhisha kuwa akidi ya mkutano huo ilitimia.

Mkutano huo ulikuwa na ajenda ya kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi wazi, na kujadili kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.
Taarifa ilieleza kwa mujibu wa Ibara ya 79(3) ya katiba ya chama hicho toleo la mwaka 2014, wajumbe wa mkutano mkuu walimchagua Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti wa kuongoza kikao hicho cha mkutano mkuu kutokana na nafasi hiyo ya mwenyekiti wa chama taifa kuwa wazi.

Katika taarifa hiyo, ilielezwa pia kwamba, wajumbe wa mkutano mkuu walizikubali na kuzithibitisha ajenda mbili za mkutano huo zilizoandaliwa na kuwasilishwa na baraza kuu la uongozi taifa ambazo ni kupokea taarifa ya barua ya kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na kujaza nafasi wazi ya mwenyekiti wa chama taifa, makamu mwenyekiti taifa na wajumbe wanne wa baraza kuu la uongozi taifa.

“Baada ya kuwasilishwa ajenda ya kwanza na wajumbe kupata nafasi za kuijadili ajenda hiyo kwa uwazi na kina, huku kukiwa na mitazamo tofauti, ghafla aliyekuwa mwenyekiti wa chama taifa Profesa Ibrahimu Lipumba alilazimisha kwa nguvu kuingia ndani ya ukumbi akifuatana watu ambao si wajumbe wa mkutano mkuu huo na kuanzisha vurugu ndani ya ukumbi wa mkutano,” taarifa hiyo inaeleza.

“Viongozi wa chama na mwenyekiti wa mkutano huo waliweza kuwatuliza wajumbe na kuendelea na kikao.”

Taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya mjadala wa barua ya Prof. Lipumba, wajumbe wakizingatia Ibara ya 117(2) cha katiba ya CUF, walikubaliana kufanya uamuzi juu ya kukubali na au kukataa kujiuzulu kwake.

“Wajumbe wa mkutano mkuu walipiga kura na matokeo ni kuwa wajumbe walioafiki uamuzi wa kujiuzulu kwa Profesa Lipumba walikuwa wajumbe 476 na waliokataa kujiuzulu kwake walikuwa wajumbe 14 na wajumbe wengine hawakupiga kura ya kukubali au kukataa,” taarifa hiyo inaeleza zaidi.

“Baada ya matokeo hayo kutangazwa na wajumbe kurejea katika ukumbi kuendelea na ajenda ya pili, huku Profesa Lipumba wakati wote akiwa ndani ya ukumbi akishuhudia uamuzi huo wa wajumbe, wajumbe wachache waliokuwa wakikataa kujiuzulu kwake wakishirikiana na wale alioingia nao, walianzisha vurugu za kutotaka kuendelea kwa ajenda ya pili ya kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi.

“Kutokana na hali hiyo ya kufanya vurugu ndani ya mkutano mkuu, viongozi wa chama taifa walishauriana na kuona kuwa busara ni kuahirisha zoezi hilo la kujaza nafasi, na mwenyekiti wa kikao cha mkutano mkuu maalum wa taifa, Mtatiro alifunga mkutano huo mpaka hapo wajumbe watakapoarifiwa tena.

“Mchakato wa kukamilisha zoezi la kujaza nafasi wazi za uongozi wa chama taifa upo palepale na baada ya kukamilisha taratibu za ndani ya chama, tutatoa taarifa kwenu na kwa Watanzania wote.

“Ni muhimu kukumbukwa kwamba ajenda ya kwanza ya msingi katika mkutano mkuu huu imekamilika kwa wajumbe wengi wa mkutano mkuu wa chama taifa kukubali kujiuzulu kwa Profesa Ibrahimu Lipumba,” inafafanua zaidi taarifa hiyo.

Baraza kuu la uongozi taifa la chama hicho lilifanya mchujo wa wagombea tisa waliojaza fomu na kupitisha majina matatu ya wagombea wa nafasi hiyo ya mwenyekiti wa chama taifa ambao ni Twaha Taslima, Riziki Shahali Mngwali na Juma Mkumbi.

Kwa nafasi ya makamu mwenyekiti, waliopitishwa kugombea ni Salim Biman na Mussa Haji Kombo.

KAULI YA MSAJILI
Wakati mkutano wa chama hicho ukikumbwa na vurugu, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema bado inamtambua Twaha Taslima kuwa ndiye Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho.

Akizungumza na Nipashe jijini jana kuhusu vurugu hizo za juzi, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, alisema ofisi ya msajili ilipokea fomu ya mabadiliko ya uongozi (PP7) kutoka kwa viongozi wa juu wa CUF mwaka jana ambayo ilieleza kuwa Taslima atakaimu nafasi ya uenyekiti wa chama baada ya kujiuzulu kwa mwenyekiti, Prof. Lipumba.

“Mwaka jana baada ya Profesa Lipumba kutangaza katika vyombo vya habari kuwa amejiuzulu nafasi yake, tulipokea PP7 kutoka kwa viongozi wa juu wa CUF ambayo ilisainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif kuwa Twaha Taslima atakaimu nafasi hiyo, hivyo sisi kama ofisi ya msajili bado tunamtambua Taslima,” alisema Nyahoza.

Alisema kwa sasa ofisi ya msajili inasubiri taarifa kutoka kwa viongozi wa CUF kuhusu vurugu zilizotokea juzi ili itolee ufafanuzi kwa kuwa ofisi hiyo haikualikwa katika mkutano huo ingawa walikuwa na taarifa ya kufanyika kwake.

Alisema hadi jana hakukuwa na mwanachama yeyote aliyefika katika ofisi ya msajili kuelezea tukio hilo la fujo, hivyo ofisi ya msajili haiwezi kuzungumzia wala kutoa uamuzi wowote.

“Hatuwezi kutumia ushahidi wa vyombo vya habari kuhusu vurugu hizo, utaratibu ni kuwa viongozi wenyewe wanapaswa kuja kutueleza, sisi tunafanya jambo lolote kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, hata hivyo ni mapema sana kulitolea ufafanuzi jambo hilo wakati lilitokea jana (juzi),” alisema Nyahoza.

Alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni za vyama vya siasa, inaeleza kuwa chama cha siasa ndani ya siku 14 kinapaswa kupeleka taarifa ya uchaguzi wake kwa msajili wa vyama vya siasa.

Aliongeza kuwa mwaka huu CUF ilipeleka barua katika ofisi ya Msajili kuwa watafanya mkutano mkuu wa kuwachagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti Agosti 21, lakini hawakutoka taarifa ya mwaliko.

OFISI ZA CUF
Katika ofisi za CUF zilizopo Buruguni jijini Dar es Salaam, Nipashe ilikuta baadhi ya wanachama wa chama hicho wakiwa nje ya geti, wakidai kuzuiliwa kuingia ndani.

Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Serengeti, Julius Magoiga alisema alifika ofisini hapo kwa lengo la kujua hatma ya chama chake, lakini alizuliwa na walinzi kuingia ndani.

Naye Katibu wa CUF Geita, Severine Nagese alisema uamuzi wa kuwazuia wanachama wa chama hicho kutoka Tanzania Bara kuingia ndani ya ofisi hiyo siyo mzuri na wana mkakati wa kwenda kuwahamasisha wanachama wa mikoani kupinga kile alichodai ubaguzi unaoingia katika chama hicho.

CCM WAZUNGUMZA
Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema kwa sasa CUF wanapaswa kuwa na umoja.
Kuhusu madai ya CCM kumtumia Prof. Lipumba kuivuruga CUF, Ole Sendeka alisema madai hayo siyo ya kweli na kwamba chama hicho tawala hakiko karibu na mwanasiasa huyo bali Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif. 


“CCM ina historia ya karibu na Maalim Seif kuliko Lipumba. (Maalim Seif) aliwahi kuwa mwanachama wa CCM," alisema. "Na hatujawahi kuweka pandikizi CUF kwa kuwa chama chenyewe ni kichanga na hakina madhara yoyote kwetu.”


Aliongeza kuwa CCM ipo tayari kuvisaidia vyama vya siasa katika namna bora ya kufuata demokrasia.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: