KAMA UMEINGIA NA KUFANYA KAZI SERIKALINI, HILI NI BALAA JIPYA KWA WENYE VYETI BANDIA TANZANIA
HILI sasa ni balaa! Hivyo ndivyo yeyote anaweza kuelezea juu ya operesheni mpya iliyotangazwa na Serikali katika kuwabaini watumishi wake wote walioingia kwenye mfumo wa ajira kiujanja-ujanja wakitumia vyeti bandia vya elimu na taaluma.
Katika mpango huo mpya wa kuhakikisha kuwa yeyote mwenye cheti bandia anabainika na hatua za kikazi na kisheria zinachukuliwa, sasa serikali imedhamiria kutumia mashine zaidi ya 5,000 za kielektroniki zilizosambazwa nchini kote ili kufanikisha utambuzi wa watumishi wake na kuwapatia vitambulisho vya taifa na pia kubaini uhalali wa vyeti vya watumishi wake.
Akizungumza na waanadishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, amesema operesheni hiyo kabambe itafanyika kwa wiki mbili kuanzia Oktoba 3, 2016 hadi Oktoba 17, 2016 na kwamba, kila mtumishi atatakiwa kutoa ushirikiano katika uhakiki huo unaohusisha matumizi ya vifaa vya kisasa.
Alisema ukaguzi huo wa kielektroniki wakati wa usajili ili wapatiwe vitambulisho unatarajiwa kubaini uhalali wa kila cheti na hivyo itakuwa vigumu kwa yeyote yule aliyeghushi kunusurika.
Alisema hatua hiyo inalenga kuwatambua watumishi wenye vyeti bandia na pia watumishi hewa ambao wamekuwa wakisakwa tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani kutokana na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha kupitia malipo mbalimbali yakiwamo ya mishahara isiyostahili.
Akifafanua zaidi, Waziri Kairuki alisema watumishi wote watakaohakikiwa wanatakiwa kuwa na vyeti vyao vya kuzaliwa na vya kielimu, kitambulisho cha kazi, hati ya malipo ya mshahara (salary slip) na pia kitambulisho cha kupigia kura.
Alisema kuwa ndani ya kipindi hicho cha wiki mbili, kila mtumishi atatakiwa ahakikishe kuwa amehakikiwa na yeyote atakayekiuka agizo hilo atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.
Aidha, Waziri Kairuki alisema katika kufanikisha kazi hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo iliyotoa mashine zake 5,000 za kielektroniki kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ili kutumika kuwakagua na kuwasajili watumishi hao wa umma nchi nzima.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kunakuwapo taarifa sahihi za watu ili kuisaidia serikali katika kupanga na kutekeleza mipango yake ya maendeleo na kudhibiti usalama wa nchi,” alisema
UFAFANUZI ZAIDI
Kairuki alisema usajili huo ambao unafanywa na Nida, utaanza hiyo Oktoba 3 na kila mmoja atatakiwa kwenda na nyaraka hizo ikiwamo vyeti ili kukaguliwa na wataalamu wa utumishi kimoja baada ya kingine. Baada ya hapo, kila mmoja atapatiwa kitambulisho cha taifa.
Kairuki alisema moja ya mikakati yao ni kuunganisha mifumo ya utambuzi wa watu na mifumo mbalimbali ikiwamo ya usimamizi wa rasilimali watu na mishahara katika utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Kairuki, kuunganishwa katika mifumo hiyo kutawezesha mifumo ya kieletroniki ya usimamizi wa rasilimali watu na mishahara kutumia kanzidata ya utambulisho wa taifa ya Nida, ambayo ina taarifa za kibaiolojia na alama za vidole za watumishi wa umma.
“Kutumia kanzidata ya Nida kutatuwezesha wizara kuwa na taarifa sahihi zaidi za watumishi na kuondoa vyanzo vya watumishi hewa na vyeti bandia vinavyotokana na utambulisho danganyifu,” alisema Kairuki.
Waziri Kairuki alisema katika kufanikisha jambo hilo, ndiyo maana wamewahusisha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Nida kwa kushirikiana na wizara yake, zitaendesha ukaguzi wa vyeti, usajili na utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wote wa serikali walioko katika Wizara, idara za Serikali zinaojitegemea, tawala za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma.
“Nachukua fursa hii kuzitaka ofisi na taasisi zote za serikali kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha kazi hii muhimu ambayo itafanyika kwa nchi nzima ndani ya wiki mbili.
Watumishi wote wahakikishe wanakuwa na taarifa zote muhimu zinazowatambulisha kama vile cheti cha kuzaliwa, vyeti vya elimu, kitambulisho cha kazi, kitambulisho cha Mzazibari Mkazi, salary slip (hati ya malipo ya mshahara) inayosomeka vizuri, hati ya kusafiria na kadi ya kupiga kura,” alisema.
Kwa watumishi ambao tayari wana vitambulisho vya taifa, alisema wanatakiwa kuhakiki wakati wa utekelezaji wa usajili katika vituo vya jirani vitakavyoshughulikia jambo hilo.
Kairuki alisema kwa ofisi ambazo ziko Dar es Salaam, watumishi watasajiliwa katika ofisi zao na wale walioko katika mikoa mbalimbali, watafanya uhakiki katika vituo vilivyoko kwenye halmashauri au ofisi husika.
Alisema wamejipanga katika usajili huo na kila mkoa umepatiwa vifaa kwa ajili ya kuhakiki kwa wakati watumishi nchi nzima.
Waziri alisema waajiriwa na watumishi watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi.
NIDA WANENA
Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) wa Nida, Mohamed Hamis, alisema tayari wana mashine za kutosha zitakazowezesha kufanikisha usajili wa watumishi hao na kila mkoa wana ofisi, hivyo usajili utafanyika bila usumbufu wowote.
Hamis alisema kwa wale ambao walipatiwa vitambulisho ambavyo havina saini, watasajiliwa upya mwakani.
“Tukimaliza kuwasajili watumishi wa umma, mikakati yetu ni kwamba ifikapo Desemba 31, mwaka huu, kila Mtanzania awe na kitambusho cha uraia. Baada ya hapo tutawasajili upya wale ambao walipatiwa vitambulisho vya taifa ambavyo havina saini,” alisema.NIPASHE
0 comments:
Post a Comment