MJASIRIA-MUZIKI Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’, amesababisha presha za mashabiki wa Bongo Fleva zipande na kushuka kwa kasi baada ya kupost Instagram video ya mkoko wa kifahari aina Rolls Royce, toleo la Ghost Black Badge.
“Hongera sana”, “Simba umevuta gari mpya nini?”, “aminia Platnumz wakong’ote kwa mafanikio tu.” Ni nukuu chache kati ya nyingi, kusindikiza video hiyo ya Bwana Nasibu.
Ni lake? Hilo ndilo swali ambalo Bwana Nasibu a.k.a Baba Tiffah Dangote hakutokezea kujibu, akawaacha mashabiki waelemewe na furaha, huku wengine wakiona kama wameachwa gizani.
Si unajua tena? Imezoeleka mastaa wakitupia mafoto mtanadaoni kama hivyo, husindikiza na maneno “my new ride” akimaanisha usafiri wake mpya lakini Chibu Dangote amekaa kimya.
Una habari yoyote kuhusu Rolls Royce? Asikwambie mtu, ni moja kati ya ndinga za kifahari sana ndani ya dunia hii. Si gari ya mchezomchezo, si mkoko wa kujaribujaribu, si motokaa ya kutembelea hizi barabara za Kibongo, kila baada ya mita 50 kuna tuta, eti ndiyo kulinda usalama.
Je, Diamond amefanya kweli au ameweka video hiyo kuonesha kuwa anatamani kumiliki kifaa hicho kilichotengenezwa kwa mara ya kwanza Machi 15, 1906 na wavumbuzi Charles Stewart Rolls na Sir Frederick Henry Royce? Wavumbuzi hao wakatumia majina yao ya mwisho kutoa jina la gari.
Na kama ni kweli, basi Diamond pia atakuwa anathibitisha kwamba yeye siyo wa mchezo, maana gari hilo tangu kuzaliwa kwake, limekuwa ghali na la kifahari mno bila kushuka viwango. Mastaa kibao Ulaya na Marekani wanasukuma ndinga hiyo barabarani.
Na usiende mbali, Sultani wa Brunei, Hassanal Bolkiah anatumia pia Rolls Royce, ingawa yeye ni Phantom VI. Thamani ya gari hilo ni Dola za Marekani 148,645, sawa na shilingi milioni 325.
Shughuli ni kuwa gari hilo ambalo Diamond amepost video yake kwa sasa kwenye soko la dunia, bei yake inaanzia Dola za Marekani 350,000, sawa na zaidi ya shilingi milioni 700.
Usawa huu wa Prezidaa Magu unashusha Rolls Royce la shilingi milioni 700, huyu dogo si bure, anatafuta kurogwa!Chanzo/www.luqmanmaloto.com
0 comments:
Post a Comment