OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ikimtaka kujibu malalamiko ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba.
Aidha, ofisi hiyo imeutaka uongozi wa chama hicho kueleza hatua ulizopitia hadi kufikia uamuzi wa kumvua uenyekiti na kumsimamisha uanachama msomi huyo.
Ofisi hiyo imeupa uongozi wa CUF hadi kesho saa 9:30 alasiri kuhakikisha umejibu barua hiyo uliouandikia. Agosti 29, Prof. Lipumba aliwasilisha malalamiko kwenye ofisi hiyo akipinga kuvuliwa uenyekiti na kusimamishwa uanachama wa CUF.
Katika mahojiano na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Laurent, alisema barua hiyo iliandikwa kwenda kwa chama hicho Agosti 29 mwaka huu baada ya ya Prof. Lipumba kuwasilisha barua siku hiyo akipinga kung'olewa kwa nafasi yake kwa madai kuwa taratibu hazikufuatwa.
Monica alilisema ofisi hiyo haiingilii masuala ya ndani ya vyama vya siasa lakini vyama vinatakiwa kufuata taratibu, kanuni na katiba zake katika kujiendesha na kufanya uamuzi wa masuala mbaliambali.
"Chama cha CUF kijieleze na kujibu barua ya msajili, ndipo tutatoa uamuzi kuhusu suala hilo. Kwanza tufahamu utaratibu uliotumika, vikao, taarifa za mkutano pamoja na katiba ya chama," alisema.
Alisema kanuni za vyama vya siasa zinampa mamlaka Msajili kupata taarifa za chama chochote iwapo kuna umuhimu na kuhitajika kutolewa kwa taarifa husika.
Baada ya kukabidhi barua hiyo, Prof. Lipumba alisema yeye ndiye mwenyekiti halali wa CUF licha ya Baraza Kuu la Taifa la chama hicho kutangaza kumsimamisha uanachama pamoja wenzake 10 akiwamo Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Magdalena Sakaya.
Alisema kikao kilichokaa juma hili visiwani Zanzibar na kufanya uamuzi wa kuwasimamisha uanachama, hakikuwa halali na kilikuwa nje ya matakwa ya katiba ya CUF.
0 comments:
Post a Comment