BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAAGIZO YA MWALI JULIUS NYERERE KUWATAKA WATANZANIA KUPIGANA VITA DHIDI YA MAADUI, YAFANYIWE KAZI KWA 100% TU

 
NI miaka 17 sasa imepita tangu Rais wa Awamu ya Kwanza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aiage dunia.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia kwa ugonjwa wa saratani ya damu, Alhamisi Oktoba 14, 1999, saa 4:30 asubuhi (kwa saa za Afrika Mashariki), katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London, Uingereza. 


Wakati wa uhai wake Mwalimu Nyerere alichukia na kukemea vikali mambo kadhaa yasiyofaa kwa mustakabali wa maendeleo ya Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Baada ya nchi kupata Uhuru, Mwalimu aliwataka Watanzania kushirikiana kupigana vita dhidi ya maadui watatu; ujinga, maradhi na umasikini.

Mwalimu pia aliamini kwamba adui mkubwa kabisa kati yao alikuwa ujinga na kwamba ukishapambana naye, basi maadui wengine waliobaki; maradhi na umasikini inakuwa rahisi kuwadhibiti. 

 
Katika uongozi wake alifanikiwa kwa nafasi yake kuondoa ujinga, Watanzania wengi, wakiwemo viongozi wetu wa sasa ambao walisomeshwa bure katika mazingira mazuri na ya kuridhisha kwa manufaa ya nchi yetu.

Kama Nyerere asingechukia ujinga kwa kuboresha mazingira ya elimu, ikiwemo elimu ya watu wazima, basi leo hii tungekuwa na viongozi ‘mazezeta’ Mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alikuja na sera ya Elimu ya Kujitegemea iliyotokana na Azimio la Arusha ikiwa ni miaka michache tangu serikali kuzifanya shule zote zilizokuwa zikiendeshwa na taasisi binafsi kumilikiwa na serikali.

Chini ya mfumo huo, Serikali ilikuja na Elimu kwa Wote (UPE) ambayo iliwataka watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule (miaka saba) kuhakikisha wanaanza shule na kwa wale ambao mfumo huo uliwaacha nje hususan watu wazima wanapata elimu ya watu wazima. 


Kama ilivyo sasa, kipindi hicho Serikali ya Mwalimu ilitoa elimu ya msingi bure ( hadi vyuo vikuu). Baadhi ya nukuu zake zifuatazo, zinaonesha jinsi Mwalimu alivyotilia mkazo sula zima la elimu.

Katika kuelezea kuwa Elimu ni Ukombozi ulio kichwani mwa aliyeelimika, Mei 20 mwaka 1974 alisema: “Kinyume kabisa na elimu... ni aina ya mafunzo yanayomfundisha mtu kujifananisha na bidhaa, ambazo thamani yake inapimwa kwa vyeti, shahada au sifa nyingine za kitaaluma.” 


Akizungumzia hali na changamoto ya Elimu ya Tanzania Oktoba 22 mwaka 1984 alisema: “Kukosa nafasi (ya kuingia kidato cha kwanza) haina maana kwamba (mwanafunzi) amefeli chochote.

Ni matokeo ya kuwepo kwa nafasi finyu sana za kidato cha kwanza. Hivyo kama kuna neno lolote kuhusu kufeli, ni kwa nchi na Serikali ya Tanzania kwa ujumla iliyofeli kutoa elimu ya sekondari kwa kila mmoja.” 


Pia alinukuliwa akisema: “Tunapoongelea kupanua elimu ya sekondari, tunaharakisha sana kusema kwamba watu watachangia ujenzi kwa juhudi zao, lakini majengo hayana umuhimu wa kwanza... Vitu muhimu katika elimu ni walimu, vitabu, na kwa sayansi ni maabara.”

Machi 5, mwaka 1998, Nyerere pia aliwakumbusha Watanzania kuwa elimu ni kwa ajili ya huduma katika jamii inayokuzunguka na si ubinafsi akisema: 


“Hakuna mtu anayetutaka kuwapenda wengine zaidi ya tunavyojipenda wenyewe: Lakini kwa baadhi yetu tuliobahatika kupata elimu nzuri tunawajibika kuboresha ustawi wa jamii tunamoishi: Ni sehemu ya kujipenda sisi wenyewe.”

Katika kusisitiza haki za elimu kwa watoto wenye ugonjwa au wenye ulemavu, Februari 18, mwaka 1974 Mwalimu Nyerere alisema: “Wasiojiweza ni wa nchi hii, wanachohitaji sana ni nafasi ya kushiriki kwa ukamilifu na kwa usawa katika mambo ya nchi yao.” 


Pia alizungumzia nguvu ya Mwalimu Agosti 27, 1966, pale aliposema: “Wale wenye wajibu wa kufanya kazi na vijana wa umri mdogo wana nguvu kubwa zisizozidiwa na nguvu za yeyote yule kwa kutilia maanani hali ya baadaye ya jamii yetu. Nguvu hizi zipo katika makundi mawili, wazazi na walimu.”

Mwalimu Nyerere ambaye pia alipata kusema kwamba “namna nzuri ya kumsaidia mtoto wa masikini ni kumpa elimu,” ni Rais wa Kwanza na ni muasisi aliyeliletea taifa hili uhuru wa kweli kutoka katika makucha ya mkoloni Desemba 9, 1961. Mwasisi huyo wa taifa alizaliwa Aprili 13, 1922 katika kijiji cha Butiama, mkoani Mara.

Alikuwa ni mtoto wa Chifu Burito Nyerere wa kabila la Wazanaki ambalo ni moja ya lahaja za Kikurya. 


Alikuwa ni miongoni mwa wasomi wachache wa wakati huo nchi ikiwa chini ya utawala wa wakoloni na ni Mtanzania wa kwanza kupata nafasi ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Edinburg, Scotland na kuhitimu mwaka 1952 katika fani za uchumi na historia
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: