UNGA wa sembe na dona unaouzwa kwenye maduka, maeneo ya mijini si salama kutokana na uandaaji wake kutozingatia masharti wakati wa kusaga mahindi ili kupata unga huo, imeelezwa.
Utafiti wa kina uliofanywa na gazeti hili katika maeneo ya Tandale, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam ambako ndiko kuna mashine nyingi za usagaji wa nafaka hiyo, umebainika kuwa wengi wa wanaosaga mahindi, wanafanya hivyo bila ya kuyaosha kwa kiwango kinachotakiwa.
Madhara ya afya kwa walaji yamethibitishwa na wataalamu kutoka Bodi ya Nafaka na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Utafiti umeonesha kuwa, baada ya mahindi kushushwa katika mashine za Tandale kutoka kwa wauzaji wakubwa ambao hushusha magunia mengi ya mahindi, wasagaji huyachukua na kuanza kusaga moja kwa moja huku wakiweka maji kidogo kwa ajili ya kusaidia ulainishwaji wake.
Ingawa wasagishaji hao hutakiwa kuanza kwa kuyachambua ili kuondoa uchafu mbalimbali katika mahindi hayo, ambao kwa kawaida huanzia mashambani hadi kwenye uhifadhi, imebainika kuwa wao husaga moja kwa moja, bila kufanya hivyo.
Gazeti hili limebaini kuwa kushindwa huko kuzingatiwa kwa masharti hayo kunatokana na kukosekana kwa usimamizi wa masharti husika ya usagaji huo, ambayo yasipozingatiwa yanaweza kuwa na athari kwa walaji.
Baada ya kubaini usagaji huo wa mahindi usiozingatia masharti, gazeti hili liliwahoji baadhi ya wataalamu wa masuala ya kilimo cha chakula, ikiwemo kutoka Bodi ya Nafaka ambacho ni chombo cha serikali chenye dhamana ya kufuatilia usalama wa chakula, ambao wameeleza kuwa kinachofanywa na wasagaji hao ni kinyume na utaratibu.
Ofisa anayeshughulikia Ubora wa Bodi hiyo, Sarah Ngweke alisema kwa kawaida wauzaji wengi wa mahindi wanatumia dawa ya kutunzia mahindi pindi wanapokuwa wamevuna na wanaposubiri kuyauza.
Alisema wapo baadhi ya wakulima ambao licha ya kutumia dawa hizo, lakini hushindwa kuzingatia ubora katika uhifadhi wa mahindi na hivyo kufanya sehemu ya mahindi kuvunda. Alisema, kutokana na hali hiyo wasagishaji wanapaswa kuyaosha vema mahindi kabla ya kuyasaga ili kuhakikisha kemikali iliyotumiwa kuhifadhi inatolewa kabisa.
"Wakulima wengine hutumia dawa za kuhifadhia mahindi hayo yakiwa ghalani, sasa basi kutokana na utofauti wa uhifadhi wake mengine yanavunda na hivyo kunakuwa na uhitaji mkubwa wa kuyaosha na kuyakagua kabla ya kusaga ili kuondoa kila aina ya uchafu unaoweza kupatikana," alisema Sarah.
Alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa ili kupata unga wa dona, kuna njia bora zaidi ya kusaga mahindi ambapo alisema inatakiwa kumenywa ganda na kubakia kiini tu.
Aliongeza kuwa chini ya usagaji usiozingatia viwango, wasagishaji wanasaga na ganda lake, hivyo kushindwa kutoa dona salama.
Alisema usagaji wa mahindi usiozingatia viwango kwa ujumla unaweza kuwa na sumu kuvu inayoweza kusababisha saratani ya ini, kudumaza ukuaji wa mtoto, kushusha kinga ya mwili na hasa katika unga wa dona.
Maelezo hayo ya kitaalamu yanaashiria kuwa wasagaji wa mahindi wasiozingatia masharti wanahatarisha usalama wa walaji, kwa kuwa wauzaji wa unga huo ambao wanapeleka mahindi kwa wasagaji hao wao wanazingatia zaidi kupata faida na si kuzingatia masharti hayo.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza anasema mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa wasagaji na wauzaji wa mahindi kuzingatia masharti ya shughuli hiyo. Alisema, wakulima wanatakiwa kuweka dawa ya mahindi inayodumu ndani ya miezi mitatu na kisha kuuza mahindi hayo.
Alibainisha kuwa, TFDA inafuatilia wauzaji wa unga huo wa sembe na dona na hasa wanaofungasha kwenye mifuko na kuingiza sokoni kuhakikisha kuwa wanakaguliwa na kuwekewa nembo ya mamlaka hiyo.
Utafiti wa gazeti hili umebaini kuwa kwa wanaosaga na kuuza moja kwa moja madukani au kuuza kwenye hoteli bila ya kuzingatia masharti ya usagaji wake, wanawalisha wananchi chakula ambacho si salama.Habarileo
0 comments:
Post a Comment