WAKATI idadi ya Watanzania wanaopata ugonjwa wa saratani ikiendelea kuongezeka kila uchao, imebainika kuwa ulaji wa vyakula vyenye viambata vya kemikali hatari kiafya ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuwapo kwa janga hilo.
Aidha, sababu nyingine za kuenea zaidi zaidi kwa ugonjwa wa kansa zimetajwa kuwa ni za kimazingira na kibaiolojia ikiwamo wanaume kuwa na wapenzi wengi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa, alisema idadi ya wagonjwa imeongezeka kwa asilimia 100 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita huku wengi wao wakiwa ni wanawake.
“Idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka siku hadi siku… kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka huu, kuna ongezeko kubwa. Taasisi sasa inapokea wagonjwa wapya wa saratani 5,000 kwa mwaka kutoka wagonjwa 2,000 mwaka 2005," alisema.
Akieleza zaidi, Dk. Kahesa alisema asilimia 60 ya wagonjwa wanaofikishwa katika hospitali yao ni wanawake na kati ya hao, asilimia 36 hukutwa wakiwa saratani ya shingo ya kizazi.
Alisekwa kwa ujumla, watu wengi hupata magonjwa ya saratani kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za ulaji wa vyakula vyenye kemikali hatari pamoja na sababu za kimazingira.
Hata hivyo, licha ya kuwapo uwezekano wa kuwa na watu wengi zaidi wenye kukabiliwa na magonjwa ya saratani, Mkurugenzi huyo alisema ni asilimia 10 tu ya wagonjwa nchini kote ndiyo hufika hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.
“Kama mnavyofahamu, suala la kufika hospitalini mapema kwa ajili ya matibabu linaathiriwa na changamoto nyingi. Kuna watu wanapata saratani lakini kwa kutokuelewa, wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji na wengine hukimbilia kuombewa katika nyumba mbalimbali za ibada kwa kuhisi kuwa ni mambo ya kishirikina," alisema na kuongeza:
"Ukiangalia kwa haraka, unaweza kuona kama idadi ya wagonjwa hao ni ndogo, lakini kiukweli idadi ni kubwa kwa kuwa hata takwimu tunazozitoa ni kutokana na idadi ya wagonjwa wanaofika kuripoti hospitali huku idadi kubwa bado wanabaki katika maeneo yao wakitibu kwa njia ambazo siyo sahihi kutokana na (wao) kutokujua.”
SABABU ZAIDI ZA SARATANI
Alisema sababu nyingine ya kuwapo kwa wagonjwa wengi zaidi wa saratani ni ongezeko la idadi ya watu nchini, akisema linachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa.
Alisema hivi sasa kuna ongezeko la wastani wa asilimia 2.5 kwa mwaka.
Alisema sababu nyingine ni athari za baadhi ya michubuko wanayoipata kina mama kwenye via vya uzazi, ikiwamo pia wakati wa kujifungua.
Alisema sababu nyingine ni kuenea kwa kansa kutokana na kina mama kushiriki tendo la ndoa na mwanaume mwenye uhusiano na wanawake wengi.
"Jambo (hili) linapelekea kupata kansa ya shingo ya kizazi ambayo hutokana na kirusi cha HPV (Human Papilloma Virus) ambacho huambukizwa kwa njia ya kujamiiana," alisema.
Dk. Kahesa alisema michubuko katika via vya uzazi pia hujitokeza kwa wanawake wengi wanaoanza mapenzi katika umri mdogo kutokana na sehemu kubwa ya viungo vyao kuwa bado havijawa tayari kwa tendo la ndoa.
“Mara nyingi kina mama wengi hujikuta wanaugua ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kutokana na ukweli kuwa wanaume ndiyo wamekuwa wakibeba kirusi cha Papiloma kutoka kwa mwanamke mmoja kwenda kwa mwanamke mwingine,” alisema Dk. Kahesa.
Akinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Kahesa alisema ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ya pili inayoongoza kwa kusababisha vifo duniani baada saratani ya damu.
Aidha, daktari huyo alisema takwimu zinaonyesha saratani ya shingo ya kizazi na matiti ndizo zinaongoza kwa kusababisha vifo vingi vya wanawake duniani huku saratani ya shingo ya kizazi ikiongoza kwa kusababisha vifo zaidi barani Afrika, hasa katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania.
DAR KINARA SARATANI
Dk. Kahesa alisema takwimu katika taasisi ya Ocean Road zinaonyesha kuwa mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi nchini ukifuatwa na mikoa ya Kanda ya Ziwa na Mbeya.
Dk. Kahesa aliwataka Watanzania kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara kwa kuwa magojwa ya saratani hayana dalili zinazoonekana moja kwa moja na mgonjwa huathirika kwa kiasi kikubwa ikiwa atachelewa kufika hospitalini.
Aliongeza kuwa baadhi ya saratani zinaweza kupungua endapo wagonjwa watawahi hospitalini huku akiwataka wananchi kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ya mwili kusaidia kuondoa sumu zinazoingia mwilini kutokana na baadhi ya vyakula.
Tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma, katika mwaka huu wa fedha, Dk. Kahesa alisema serikali imetoa kipaumbele kwenye magonjwa ya saratani kwa kutenga bajeti ya Sh. bilioni saba kwa ajili ya dawa.
Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga Sh. bilioni 251 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment