BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HABARILEO YACHEKELEA MAADHIMISHO MIAKA 10 KWA SHEREHE YA NGUVU


GAZETI la HabariLeo linalochapishwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), imetimiza miaka 10 tangu lianzishwe Desemba 21, mwaka 2006 chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

TSN pia inachapisha Daily News, Sunday News, HabariLeo Jumapili na gazeti mahiri la michezo nchini, SpotiLeo. Sherehe za maadhimisho hayo ya miaka 10 zilifanyika jana katika ofisi za TSN zilizopo eneo la Tazara, Dar es Salaam.

Pamoja na wafanyakazi na uongozi wa kampuni kushiriki hafla hiyo, aliyekuwa Mhariri Mtendaji wakati gazeti hilo likianzishwa, Isaac Mruma, alishiriki. Mruma kwa sasa ni Naibu Mkurugenzi wa Masuala ya Watumiaji Huduma za Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Akizungumza na wafanyakazi, mbali na kulipongeza HabariLeo kuwepo sokoni katika kipindi chote hicho, Mruma aliwataka wafanyakazi hao kuwa wabunifu katika kazi zao kuendelea kuzalisha gazeti lililo bora nchini.

“Kuwepo hapa inanipa kigugumizi kwa sababu nina furaha kubwa, naamini ndoto zetu huko tunakokwenda zinaendelea kutimia, hili ni gazeti pekee la kitaifa, ni gazeti pekee la Kiswahili la Serikali, mna nafasi kubwa sana ya kufanya kazi nzuri katika eneo hilo,” alisema Mruma.

Mruma aliwashukuru wafanyakazi waliokuwepo wakati gazeti linaanza kwa kuwezesha lianze na kueleza kuwa ana furaha kubwa kuona bado HabariLeo inafanya vizuri katika sekta ya habari na katika jamii kwa ujumla.

Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi, alisema gazeti la HabariLeo ni la kitaifa na linasomwa na watu wengi, ikiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali waliopo nchini.

Aliwaasa waandishi wa gazeti hili, kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, kuwa wabunifu na wawajibike kikamilifu.

“Leo ni siku ya pekee, kwa sababu tunakumbuka miaka kumi nyuma, na hii hatutasherehekea kimya kimya, tutaendelea kusherehekea mwezi mzima na kwa tija, na tuliona ni heshima kubwa tumualike kiongozi wetu (Mruma),” alisema Dk Yonazi.

Baadhi ya waandishi wa habari waliokuwepo wakati gazeti linaanza, walisema ni gazeti lililopitia kwenye mikikimikiki mingi ya ushindani katika soko.

“Tunashukuru kwamba bado tunaendelea kuzalisha gazeti hili kwa weledi na umahiri mkubwa,” alisema, Shadrack Sagati, ambaye pia ni Kaimu Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi, RAAWU tawi la TSN.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: