MIUJIZA INAYOTOKEA TANZANIA BAADA YA WACHIMBAJI KUFUKIWA NA VIFUSI MIGODI YA DHAHABU NDIO HII.
HAKIKA ni muujiza ya Mungu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya vikosi vya uokoaji kufanikiwa kuwatoa wachimbaji 15 waliofukiwa na kifusi katika mgodi wa RZ Union uliopo Nyarugusu mkoani Geita.
Wachimbaji hao walifukiwa na kifusi hicho kwenye mgodi huo wenye shimo linakokadiriwa kuwa na urefu wa futi 38 au mita 124. Waliokolewa jana wakiwa hai baada ya kukaa chini ya ardhi kwa saa 96 ambazo ni siku nne.
Kuokolewa kwao kulitokea saa 24 tangu walipojibu ujumbe uliotumwa kwao na wao wakajibu kuwa wako hai.
Walisema walichokuwa wakihitaji kupelekewa ni chakula, maji na sigara huku wakisema mwenzao mmoja alikuwa amejeruhiwa na msumari uliomchoma mguuni.
Wachimbaji hao walionokena wakiwa wamedhoofika kwa kiasi kikubwa hivyo ilibidi wapatiwe huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kwa matibabu zaidi.
Uchunguzi wa nini hasa kilisababisha ajali hiyo bado unaendelea na viongozi wa Serikali pamoja na timu ya waokoaji wamepiga kambi katika eneo hilo.
Mchimbaji wa kwanza alikolewa saa 3.00 asubuhi jana na kufuatiwa na wenzake ambao kila mmoja alionekana akiwa ametapakaa tope.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba migodi mingi nchini haikaguliwi mara kwa mara kiasi kwamba hali ya usalama ya migodi hiyo haikidhi viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, ukiwamo usalama wa uchimbaji.
Kwa mujibu wa wachimbaji hao, kwa siku nne ambazo walikuwa ndani ya shimo hilo ardhini, walikuwa wakila magome ya miti baada ya kukata tamaa ya kuendelea kuwa hai.
Wachimbaji waliookolewa
Wachimbaji waliookolewa jana ni Aniceth Masanja, Dickison Moris, Yona Kachungwa, Dotto Juma, Aman Sylvester, Mgarura Kayanda, Agustin Robert, Hassan Idd na Mussa Cosmas.
Wengine ni Raphael Nzumba, Rashidi Shiringap, Ezekiel Bujiku, Sheku Togwa, Sabato Philimon na Raia wa China, Meng Juping ambaye ni maarufu kwa jina la Mr. Mo.
Kampuni zilizoshiriki.
Kazi hiyo ya uokoaji haikuwa nyepesi na Serikali iliyaalika makampuni mbalimbali kuongeza nguvu ya uokoaji.
Kampuni zilizoshiriki kazi hiyo ni Geita Gold Mining (GGM), Busolwa Mine, Nyarugusu Mine na Mitchell ambao walichoronga mashimo na kufanikisha kuwatumia ujumbe wachimbaji na wao kujibu wakihitaji chakula.
Naibu Waziri apongeza.
Akizungumza baada ya kazi hiyo ya uokoaji kukamilika, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alisema Serikali itahakikisha wachimbaji wadogo wanaendelea kuwa salama.
Alisema serikali itaanza kupita katika baadhi ya maeneo kuyatambua yanayomilikiwa na wageni ili yakabidhiwe kwa wananchi.
Ndugu watoa neno.
Mariam Hassani, ambaye ni mama mzazi wa Hassan Iddi, mmoja wa wachimbaji walionusurika katika tukio hilo, aliliambia MTANZANIA kuwa kwa siku zote nne hakupata usingizi kwa kuwaza hatima ya mtoto wake.
“Mungu asante kwa uwezo wako … kwa siku zote mimi pamoja na familia yetu tulihamishia kambi hapa kujua mwisho wa mtoto watu kama atapatikana akiwa hai ama laa.
“Ila kwa uwezo wake Mungu ameokolewa akiwa hai…sina cha kusema zaidi ya kumshukuru Muumba wetu,” alisema Mariam.
RC ashukuru
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga, aliwashukuru wadau mbalimbali walioungana na Serikali katika uokoaji huo.
Mbunge atoa neno
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema), aliipongeza Serikali kwa kuwaokoa wachimbaji hao ikizingatiwa watu wengine walikuwa wamekwisha kukata tamaa.
“Limekuwa ni jambo la heri na serikali imejitahidi kwa kupanga mipango mizuri kupitia makampuni yaliyo jirani kushiriki kwenye hatua hii ambayo ilitaka kuleta simanzi lakini mioyo ya wananchi sasa ina furaha,” alisema Upendo.
Akizungumzia tukio hilo, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania, John Wambura, aliwaahidi wachimbaji wadogo kuwa shirikisho hilo litaendelea kuwapa ushirikiano.
Ni tukio kubwa la pili
Oktoba 5 mwaka 2015, wachimbaji wadogo watano katika mgodi wa Nyangarata, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, waliokolewa baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo ardhini kwa siku 41.
Wakizungumza katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama ambako walilazwa kwa matibabu, wachimbaji hao walisema waliishi siku zote hizo kwa kula wadudu kama mende na mizizi mbalimbali.
Kwa mujibu wa wachimbaji hao, walikuwa wakitumia kofia zao kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu, kwa ajili ya kunywa.
Wachimbaji hao walifukiwa Oktoba 5, 2015 saa 5.00 asubuhi wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji chini ya ardhi.
Watu walioshuhudia tukio hilo, walisema ardhi ya juu ya machimbo hayo ilititia na kuporomoka kutokana na mvua iliyonyesha, na hivyo kuwafunika wachimbaji hao.
Wakati huo jitihada za uokoaji zilifanikisha kuokolewa wachimbaji sita wakati wengine hawakuweza kufikiwa, ikizingatiwa pia kuwa zilikosekana taarifa sahihi za idadi yao na eneo halisi walikokuwa wamefukiwa.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema wachimbaji hao waliokolewa baada ya kugunduliwa na wazamiaji walioingia kwenye mashimo hayo kuiba mchanga.
Alisema wachimbaji hao walisikia watu wakiomba msaada katika mashimo hayo.
“Baada ya wachimbaji hao kusikia sauti, waliwasiliana na wenzao na kuanzisha jitihada za kuwaokoa,” alisema.
Kamanda Kamugisha alisema hatimaye waliweza kuwatoa katika mashimo hayo wakiwa wamekaa kwa siku 41 tangu Oktoba 5, mwaka huu.
Waliookolewa ni Chacha Wambura, Amos Muhangwa, Joseph Burulwa, Msafiri Gerald na Wonyiwa Moris.
Mchimbaji mmoja, Mussa Spana, alifariki dunia siku chache baada ya kufukiwa na kifusi kwa kukosa chakula.
Mmoja wa wachimbaji hao, Wambura, alisema awali walifukiwa sita, lakini bahati mbaya mwenzao Spana alifariki dunia siku chache baadaye baada ya kukataa kula mizizi.
Alisema hatua hiyo ilisababisha akumbwe na ugonjwa wa kuhara uliosababisha kifo chake.
“Tulikuwa tukitumia miti inayojengea kingo za mashimo kama chakula pamoja na wadudu wadogo ndani ya mashimo hayo, hasa mende.
“Pia tulikuwa tukitumia kofia zetu ngumu (helmet) kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu ya ardhi ingawa yalikuwa ni machafu.
“Mwenzetu Musa alifariki dunia baada ya kukataa kutumia vitu hivyo,” alisema Wambura.
0 comments:
Post a Comment