By Jackline Masinde, Morogoro
Morogoro. ‘Mji kasoro bahari’ ndivyo wanavyouita wenyeji na wageni waingiapo ndani ya mkoa huu wenye vivutio vingi ikiwamo mbuga za wanyama Mikumi na Selous.
Sasa umepata kivutio kingine kikubwa kinachokusanya watalii na watu mbalimbali kutoka mikoa na nchi jirani kuja kujionea maendeleo yanayotajwa kuwa ya kipekee kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kivutio hiki si kingine bali ni kituo kipya cha Mabasi cha Msamvu kilichobatizwa jina la ‘Msamvu Airport’. Kituo ni kizuri na cha kisasa kilichojengwa kwa mtindo wa kipekee.
Mbaraka Mwinshehe wakati wa uhai wake aliwahi kuimba wimbo uliobamba kipindi cha miaka ya 80 akiusifia mji huu wa Morogoro namna ulivyopendeza kwa kutiririsha maji kutoka Milima ya Uluguru.
Baadhi ya mistari ya kibwagizo cha wimbo huo ilisema; “...Jamani Morogoro, Morogoro....njooni Morogoro mjionee ooh! Maji yatiririka milimani...mjini kati Moro wapendeza...jamani Morogoro yapendeza...”
Lau angekuwapo leo angetuimbia wimbo mwingine tena unaosifia kituo hiki adimu kilichojengwa na Kampuni ya Msamvu Property Limited (MPL) kwa ubia wa Serikali ya Halmashauri ya Morogoro na Mfuko wa Pensheni wa LAPF. Hadi kukamilika kituo hicho kitagharimu zaidi ya Sh40 bilioni.
Ramani ya jengo la kituo limebuniwa na Kampuni ya OGM Consultants huku kampuni za ujenzi zipatazo sita zikishiriki kujenga kituo hicho.
Namna kilivyo
Saa nane mchana Januari 12 mwaka huu, ndiyo siku niliyowasili ndani ya kituo hiki murua kwa mara ya kwanza.
Msamvu niijuayo kabla haijawa hii mpya, muda kama huo utakapowasili utakutana na jua kali, vumbi na upepo, kelele za wapiga debe, honi za magari, kuzongwa na madereva teksi na bodaboda, kuvutwa huku na kule na wakati mwingine kutolewa lugha chafu.
Nilipofika mara hii haya yote sikuyakuta. Nilistaajabu huku nikihisi pengine si Msamvu niijuayo. Nikiwa ndani ya gari ikanilazimu kufungua dirisha ili kuona vizuri.
Hakika pamependeza, hewa safi na utulivu wa hali ya juu ulizidi kinistaajabisha. Wakati nashuka ndani ya basi nilipokelewa vizuri na madereva wachache wa teksi na bodaboda ambao walivalia sare huku muziki laini ukitumbuiza ndani ya kituo hiki.
Nilijiona kama nashuka uwanja wa ndege wa kimataifa, jengo lililopo mbele yangu linapendeza machoni, watu waliokuwa wakisubiri ndugu zao walikaa eneo katika eneo maalumu. Ninaona migahawa ikiwa katika mazingira safi, wahudumu waliovalia sare na walikuwa wasafi.
“Dada karibu hapa ndiyo Msamvu ‘Bus Terminal’ kama unatoka nje geti lile pale ukifika hapo unaonyesha tiketi yako,” anasema kijana mmoja bila shaka alikuwa dereva wa bodaboda.
Ilinilazimu nikae kwanza kama dakika 45 kushangaa mazingira ndani ya kituo hiki. Kuna milango mitatu ya kuingia na kutoka ndani ya kituo hiki kwa abiria na wasindikizaji.
Pia, kuna milango miwili ya kuingilia mabasi na kutoka. Kwa upande wa mlango wa kutokea mabasi kuna kituo cha trafiki ambacho hukagua magari kabla ya kuendelea na safari.
Katika milango ya kuingilia na kutokea abiria, kuna vyumba viwili ambavyo wanakaa watu ambao wanashida maalumu ya kuonana na mtu aliye ndani ya kituo.
Watu wanaoingia kituoni hapo hulipia Sh200 kwa wale ambao si wasafiri, kama ni msafiri anapaswa aonyeshe tiketi ya basi. Pia katika eneo hilo kuna chumba maalumu cha kuwadhibiti watu wanaofanya fujo mfano wanaogoma kulipa ushuru au kufanya vurugu.
Vyakula, matunda na vinywaji vimewekwa katika hali ya usafi, mawakala na wapiga debe wamevaa sare na vitambulisho. Pia, kuna maduka ya nguo na bidhaa zingine.
Pikipiki, magari ya abiria na teksi zimejipanga katika mpangilio mzuri, wafanyabiashara ndogondogo hawakuonekana kabisa ndani ya kituo. Bodaboda na teksi zinazoegeshwa nje ya kituo pia ziko katika mpangilio mzuri.
Abiria na watu wanaokuja kusindikiza na kupokea ndugu zao wanakaa kwa amani na raha huku wengine wakisoma magazeti na vitabu na wengine wakiangalia na kuwasiliana na simu zao. Wapo wanaopata vinywaji baridi na wengine chakula kwa utulivu.
Hali ya hewa ya ndani ya kituo hiki ni ya asili, ilinifanya nijione kama niko ufukweni mwa bahari, licha ya kuwa Morogoro hakuna bahari. “Mwee Morogoro town isipokuwa bahari”.
Wasemavyo wananchi
Rose Muhondwa mkazi wa Magubike nje kidogo ya mji wa Morogoro, ninamkuta akiwa amekaa eneo la kusubiria abiria, ananiambia amekuja kumpokea ndugu yake.
“Nina muda mrefu sijafika hapa Msamvu, leo nimekuta mabadiliko ambayo kwa kweli yamenifurahisha. Najihisi niko nchi fulani nzuri na siyo Morogoro niliyoizoea,” anasema.
Muhondwa anatoa pongezi kwa Serikali na wadau walioamua kuibadilisha Morogoro na kwamba isiishie Msamvu pekee bali iboreshe na vituo vingine vya mabasi nchi nzima.
Zida Mussa mkazi wa mjini Morogoro anasema, mazingira ya ndani na nje ni mazuri, wapigadebe wamekuwa na nidhamu na nadhifu siyo kama zamani.
“Kabla hapajatengenezwa ulikuwa ukiingia ndani ya stendi unavamiwa na wapigadebe, wanakuvuta huku na kule, wengine wanakunyang’anya mizigo na kukuibia,” anasema.
Zida anasema mbaya zaidi mazingira yalikuwa machafu, vumbi jingi na hakukuwa na mpangilio mzuri, kwa sasa hata ikitokea mpiga debe kakutukana au kukubughudhi kwa namna yoyote ile anapigwa faini ya Sh50,000.
“Kuna kamera zinamulika kila kona ya kituo hiki, ikionekana abiria anabughudhiwa, hatua zinachukuliwa. Usalama upo na walinzi wapo kila sehemu wanaangalia,” anasema Zida.
Baada ya kushangaa, nilikwenda kujipumzisha kisha saa mbili usiku nikajongea tena eneo hilo kujionea yanayojiri muda huo.
Utulivu ulizidi kutawala, ndani ya kituo kulionekana kama mchana. Taa zenye mwanga angavu zilipendezesha eneo hilo.
Watu walikaa kwa makundi na kutazama taarifa ya habari katika runinga zilizo ndani ya kituo hicho. Wengine walikuwa wanapata chakula cha usiku.
Mabasi yanayotoka mikoani nayo yaliendelea kushusha abiria, hakukuwa na vurugu za kugombania abiria kwa madereva teksi na bodaboda kama ilivyozoeleka.
Nyuma ya eneo la kituo hiki ninakuta kundi la watu wapatao 100 wakitazama mpira kwenye televisheni kubwa iliyowekwa ukutani.
Ilipofika saa nne usiku walikuja walinzi na kuanza kuzuia watu kuingia ndani ya kituo hicho.
“Ikifika saa nne huku ndani huwa kunafungwa hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia hata mabasi hayaruhusiwi. Huu ni utaratibu tu uliowekwa kwa sababu kituo hakijakamilika lakini kikikamilika kitakuwa kiko wazi usiku kucha,” anasema mmoja wa wasimamizi wa kituo hicho ambaye pia ni mhasibu wa MPL, Salum Chuma.
Alfajiri na mapema naamka na kwenda kituoni hapo, nakuta usafi ukifanyika kwenye migahawa na katika maduka. Pia, nakuta baadhi ya ofisi za kukatia tiketi zimefunguliwa.
Nilitembelea baadhi ya ofisi hizo na kuzungumza na Katibu wa Chama cha Mawakala wa Mabasi Msamvu, Hamis Mkingiye ambaye anasema:
“Kituo ni kizuri, walau sasa kimeleta heshima hata kwa mawakala, maana wanakaa katika ofisi nzuri na wanavaa sare safi. Mtu anajua kabisa sasa anakwenda kazini ofisi yenye mwonekano mzuri,” anasema.
Anasema mbali na hilo pia imesaidia kuondoa ulanguzi wa tiketi na wapigadeba matapeli. Mkingiye anasema kampuni zimewekewa kiwango cha wapigadebe kulingana na idadi ya mabasi iliyonayo kampuni husika, mwenye gari mbili anatakiwa kuwa na wapiga debe wasiozidi watano.
“Pia, tumeweza kudhibiti wapigadebe wanywa viroba, kwa kuweka sheria kuwa mtu haruhusiwi kunywa pombe akiwa kazini na awe katika mwonekano mzuri ambao utamshawishi abiria kupanda gari analohudumia.
“Tukimkamata mpigadebe ambaye ameajiriwa na kampuni akiwa amekunywa viroba au kumbughudhi abiria, anapigwa faini ya Sh50,000 na kama siyo mwajiriwa tunampeleka kituo cha polisi kwa hatua zaidi,” anasema.
Mkingiye anasema pamoja na uzuri wa kituo hicho bado kuna changamoto ya uhaba wa ofisi za kukata tiketi. Anasema ofisi zilizopo ni 44, lakini mahitaji ni 50 au 60.
Mkingiye anasema changamoto nyingine iliyopo ni usafi, bado ni tatizo ukiingia chooni haufanyiki. Watumiaji wenyewe siyo wastarabu wanachafua vyoo kwa kutupa chupa za maji.
“Uongozi unasema wanatatufa kampuni ya kufanya usafi na walisema ingeanza kazi wiki hii lakini bado hatujaona, pia kuna tatizo la maji,” anasema.
Wapigadebe
Mmoja wa wapigadebe, Tazani Mdeme anasema kwa sasa kuna utaratibu mzuri, wapigadebe wamepewa sare na vitambulisho na kwamba vurugu zimepungua.
“Mwanzoni tulikuwa tunapigana hadi ngumi, jasho lilikuwa linatutoka kwa sababu ya jua kali na vumbi na kugombania abiria lakini sasa kama niko ndani ya kiyoyozi na najisikia kweli niko kazini,” anasema.
“Sasa hivi naamka kwenda kazini nikiwa na uhakika kuwa naenda na nitarudi salama kuliko zamani, kwa kweli nimefurahi kuboreshwa kituo hiki,” anasema.
Waendesha bodaboda walalamika
Pamoja na mabadiliko hayo, kuna makundi yameumizwa hasa Machinga, madereva taksi na bodaboda. Kilio chao kikubwa ni kukosa wateja na kulipia ushuru wa kuingia ndani.
“Stendi ndiyo ni nzuri, lakini imekuwa gharama kwetu sisi tunaoendesha bodaboda, maana haturuhusiwi kuingia ndani mpaka tulipe Sh200 kufuata abiria,” anasema Athuman Abdalah.
Silvano Gaitarn anasema: “Eneo tulilopangiwa kukaa ni vigumu kupata abiria na kwa siku unaweza kutumia Sh2,000 hadi Sh3,000 kwa kuingia ndani wakati zamani ilikuwa bure.”
“Kungewekwa utaratibu bodaboda tungekuwa tunalipa hata Sh500 kwa siku au Sh1,000 ili tuwe tunaingia ndani kutafuta abiria. Hivyo hatutakuwa tunatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuingia kituoni,” anasema Abdalah.
Anasema wanalipa ushuru wa Sh1,000 kwa siku kwa baadhi ya bodaboda wanaoegesha, lakini hawapati abiria hivyo wanalazimika kulipia Sh200 kuingia ndani kuchukua abiria, hivyo kama ataingia mara 10 maana yake atakuwa amelipa Sh2,000 ukijumlisha na ada ya maegesho kwa hivyo kwa siku atakuwa ametoa Sh3,000.
“Tuwekewe utaratibu mzuri, ili nasi tunufaike na maendeleo haya,” anasema.
Machinga hawana nafasi
Machinga wanaotembeza bidhaa mbalimbali wakitafuta wateja wanasema zamani gari zilikuwa zinakaguliwa nje na wao waliruhusiwa kuingia ndani hivyo iliwasaidia kuuza bidhaa zao, lakini sasa hawaruhusiwi hata kusogelea geti.
“Machinga wa Msamvu ni kama tumetelekezwa, hatuuzi kabisa. Ukijitahidi unabahatisha mteja mmoja kwa siku ambaye pia anaweza asikulipe maana gari zikitoka ndani ya kituo zinaondoka moja kwa moja hazisimami,” anasema mmoja wa wamachinga, Issa Jumanne.
Uongozi wa kituo
Meneja wa MPL (Kampuni inayosimamia kituo hicho), Stanley Mhapa anasema Kituo cha Mabasi Msamvu kina hadhi ya ‘airport’ na ni kituo cha kwanza kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“Kituo chetu kina jengo kubwa la utawala ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 90, ndani ya jengo hili kuna kituo chenyewe cha mabasi, maduka 26, ofisi za kukatia tiketi 44 na maduka madogo 19.
Pia kuna ATM na ofisi za benki mbili; CRDB na NMB lakini pia kutakuwa na stendi ndogo ambayo pia itakuwa nzuri na ya kisasa itakayokuwa inatumiwa na magari yanayokwenda nje ya mji wa Morogoro kwa maana ya wilaya za mkoa huo.
Mhapa anasema kuna sehemu ya migahawa ambapo abiria wanaposhuka kwenye magari watajipatia chakula, pia kuna eneo la kusubiria abiria na ofisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (LAPF). Kadhalika kipo chumba cha kuhifadhia mizigo.
Anasema pia kipo chumba maalumu cha kusimamia mitambo ya kamera zilizofungwa eneo la kituo kwa ajili ya kuangalia usalama. Pia, chumba hicho kina mitambo ya kutolea matangazo.
Mhapa anasema kwa baadaye kituo kikishakamilika watakuwa na programu ya GPS.Watu watakuwa wanapewa matangazo kuhusu basi analotaka kupanda sehemu lilipo na muda litakaowasili kituoni.
Mhapa anasema ujenzi wa kituo hicho umekamilika kwa awamu ya kwanza ambao ni jengo la utawala na stendi ya mabasi. Awamu ya pili watakamilisha jengo la biashara na awamu ya tatu watajenga hoteli ya kisasa ya ghorofa kumi.
Anasema, mbali na vitu hivyo kituo hicho pia kitakuwa na duka kubwa la dawa za binadamu ambalo pia litatumika kusambaza dawa katika Hospitali za Mkoa wa Morogoro na mikoa jirani, pia kutajengwa ‘supermarket’ kubwa na ya kisasa.
Mhandisi aliyechora ramani
Mhandisi aliyebuni ramani ya kituo hiki Oswald Modu anasema haikuwa kazi rahisi kuchora ramani, ni kazi aliyoikamilisha kwa miezi sita.
“Haikuwa kazi ya siku moja, ilikuwa ni kazi ambayo ukilala usiku unawaza ramani iweje, ramani inaweza kuja kichwani ukaamka na kuchorachora kesho tena inakuja nyingine unaendeleza pale ulipoishia,” anasema.
“Sisi tulivyoshinda zabuni tukakutana na wahusika wakatueleza jinsi wanavyotaka stendi iwe,” anasema.
“Kazi yetu ilikuwa ni kuwasikiliza na kunakili, pale palipohitaji ushauri tulishauri na mwisho tukatoka na kitu kimoja. Pia, baada ya kukubaliana tuliamua kufanya utafiti kwa nchi zingine ili kuona jinsi wanavyowajibika na kuangalia ramani za vituo vingine,”
Anasema walienda India pia walifika Dubai ili kuona na kujifunza. Walibaini majengo yao hayaendani na kile wanachokitaka wao, hivyo walirudi na kuendelea na mchoro walioubuni wao.
Changamoto
Wakati wa ujenzi walikuta sehemu ya ardhi ya Msamvu imeinuka na nyingine iko chini, hivyo kuwawia vigumu kwani ramani iliyochorwa awali ilizingatia utafiti wa awali ambao ulionyesha iko sawa.
“Taarifa tulizokuwa nazo kuhusu eneo hilo la Msamvu, awali zilionyesha ardhi iko sawa, lakini tulipotaka kuanza ujenzi tukakuta mabadiliko, hivyo ikatulazimu kubadili baadhi ya michoro ili kuendana na eneo,” anasema.
RC Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kebwe Stephen Kebwe anasema ujenzi wa stendi hiyo ni malengo ya mkoa na kwamba hiyo ni awamu ya kwanza bado kuna awamu ya pili na watajenga vibanda 70 vya biashara ndogondogo. Anasema awamu ya tatu watajenga kituo cha mafuta na hoteli ya kisasa.
“Tumejipanga vyema, lengo ni kutaka kupandisha hadhi ya manispaa yetu kuwa jiji...Tumepata mradi mkubwa wa maji. Serikali ya Ufaransa imetusaidia zaidi ya Sh70 milioni kwa ajili ya mradi wa maji ambao utasaidia mji mzima kupata maji ya uhakika.”
Anasema kituo hicho kimetoa fursa na mapato yamepanda kwani kabla hakijajengwa walikuwa wanakusanya Sh8 milioni kwa mwezi, lakini sasa wanakusanya Sh54 milioni kwa mwezi.
“Kwa kweli stendi yetu mbali na kuingiza mapato mengi. Pia, imekuwa kivutio na imetutangazia mkoa wetu. Wananchi watunze mandhari na miundombinu ya stendi yetu,” anasisitiza.
0 comments:
Post a Comment