NJAA IPO, DEBE LA MAHINDI SASA NI SH 20,000/, SPIKA WA BUNGE AMDOKEZEA WAZIRI MKUU
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amemchomekea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiitaka serikali ishughulikie suala la njaa.
Ndugai alisema hayo jana kwenye Chuo cha Maendeleo Vijijini maarufu Chuo cha Mipango Dodoma wakati wa kikao maalumu cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa, alipopewa nafasi ya kutoa salamu, ambako aliiuliza hadhara iliyokuwepo mkutanoni kuhusu bei za vyakula.
“Debe la mahindi ni shilingi elfu kumi na mbili eeh,” alihoji Ndugai huku hadhara iliyokuwemo mkutanoni ikimjibu Spika Ndugai kuwa “Hapana, ni shilingi elfu ishirini.”
Hali hiyo ilimfanya Waziri Mkuu Majaliwa kucheka huku wananchi wakishangilia.
Awali, kabla ya kuchomekea suala la njaa, Ndugai aliipongeza serikali kwa kutimiza uamuzi wa kuhamia makao makuu Dodoma ambapo leo limetekelezwa.
“Katika kuhakikisha Dodoma si kila mtu anayekuja ni mtu mwema kutakuwa na panya road, vibaka, majambazi, jambo linalotakiwa kufanyika ni kuimarisha kamati za ulinzi na usalama kwani suala la ulinzi ni jukumu la kila mtu,” alisema Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa mkoani Dodoma.
Pia alitaka wananchi kupanda miti, kwani nyumba nyingi zimejengwa hazina miti na kutaka kuhamasishwa kuanzishwa kwa bustani za kisasa kwa ajili ya kupumzikia.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu alisema serikali itaanza kusambaza kiasi cha tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu uliopita katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza kasi ya ongezeko la bei ya vyakula nchini.
Alisema katika msimu uliopita kulikuwa na zaidi ya tani milioni tatu na hivyo baada ya wabunge kushinikiza serikali kuruhusu kuuza vyakula nje kiasi cha tani milioni 1.5 na hivyo kubakiwa na tani milioni 1.5. Pia alisema serikali ndio yenye jukumu la kutangaza hali ya chakula, kama ni mbaya au nzuri.
“Tanzania bado haina tatizo la chakula, kelele zinazopigwa na baadhi ya vyombo vya habari na taarifa zinazotolewa sio sahihi, serikali ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza hali ya chakula na kwa maana hiyo basi bado tuna chakula cha kutosha,” alifafanua Waziri Mkuu.
Alisema pale serikali itakapokuwa na upungufu Watanzania watapata taarifa. Alikiri ni kweli kumekuwa na shida ya mvua, lakini sasa karibia maeneo yote mvua zimeanza kunyesha.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment