Juma Mtanda, Morogoro
Vinara wa kundi C, ligi daraja la pili Tanzania bara timu ya soka ya Cosmo Politan FC ya Dar es Salaam imeonja machungu ya ligi hiyo baada ya kujikuta ikitandikwa bao 3-1 kutoka kwa Burkina FC (Kisiki cha Mpingo) katika mchezo mkali uliofanyika kwenye uwanja wa jamhuri mkoani ya Morogoro.
Burkina FC yenye pointi 11 ilianza mchezo huo kwa kasi na kuzalisha mashambulizi katika lango la wapinzani wao na dakika ya 28, Baraka Juma aliandika timu yake kwa kufunga bao la kwanza wakati, Luwasa Tamba akifunga bao la pili dakika ya 41.
Kipindi cha kwanza Cosmo Politan FC ilishindwa kutengeneza mashambulizi katika lango la wapinzani wao na kwenda mapumziko wakiwa wamepachikwa bao 2-0 ambapo kipindi cha pili Burkina FC waliendeleza kasi yao na dakika ya 48, Hassan Mkota alifunga bao la tatu.
Cosmo Politan FC ilizinduka dakika 70 kwa kutandaza soka safi la kuonana na dakika ya 77 na Nuru Thabit alifunga bao la kufutia machozi na kufanya mchezo huo umalizike kwa Burkina FC kupata ushindi wa bao 3-1.
Mchezo huo ambao ulipangwa kufanyika (Jumamosi) ulishindwa kufanyika kufuatia shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuailisha kutokana na timu ya Cosmo Politan kupata dharura.
Akizungumz na MTANDA BLOG mjini hapa, Katibu wa chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) Charles Mwakambaya alisema alipokea simu ya kuahirishwa kwa mchezo huo kutoka kwa Afisa mtendaji mkuu wa bodi ya ligi, Boniface Wambura kutokana na timu ya pili.
Mwakambaya alisema kuwa baada ya kupigiwa simu saa 8:50 mchana (juzi jumamosi) hakuelezwa ni dharura gani ambayo timu ya pili waliipata na mchezo kusogezwa mbele.
Katibu mkuu wa timu ya Burkina FC, Gosbath Isack alieleza kusikitishwa kwake kwa kitendo cha kuahairisha mchezo bila kufuata taratibu na kanuni za ligi hiyo.
Isack alisema kuwa kuahairishwa kwa mchezo huo walipokea taarifa saa 9 alasiri wakati timu tayari imeingia uwanjani kwa ajili ya kupasha misuli.
“Tulipokea taarifa za kienyeji kuahairishwa kwa mchezo wetu na Cosmo Politan FC siku ya jumamosi saa 9 alasiri na ajabu lakini soka la Tanzania haya mambo yanafanyika, kikao cha mechi ile saa 4 hakuna kiongozi wao aliyeingia hata mchezo wa jana pia hakuna kiongozi aliyehudhuria.”alisema Isack.
“Tumelazimika kuingia gharama kubwa kwa kuihudumia timu ndani ya Manispaa ya Morogoro kutokana na sisi kuweka kambi wilayani Kilosa lakini na hawa bodi ya ligi wanapaswa kuiadhibu Cosmo Politan FC kwa kitendo cha kushindwa kuhudhuria kikao viwili kabla ya mchezo.”alisema Isack.
0 comments:
Post a Comment