MKUU WA SHULE KUU YA SHERIA AKOSOA TABIA YA MIHIMILI MITATU KUSHUTUMIANA HADHARANI
MKUU wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hamudi Majamba, amekosoa tabia inayoanza kujitokeza nchini ya mihimili mitatu ya serikali kushutumiana hadharani.
Prof. Majamba alisema Bunge, Mahakama na Serikali kwa pamoja vimekuwa vikishutumiana hadharani kiasi kwamba hali hiyo ikiachwa iendelee, nchi haitakwenda vizuri.
Mkuu huyo alikuwa akizungumza shuleni hapo juzi wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alipofanya ziara na kuzungumza na wanajumuiya mambo mbalimbali ya kisheria.
Majamba alisema nchi inashuhudia Bunge, Mahakama na Serikali vikivutana hivyo kuleta tafsiri mbaya kwa wananchi.
“Sidhani kama ni sahihi Mahakama ikaanza kusiginwa (kukosolewa) hadharani, tutakosa imani nayo," alisema Majamba bila ya kutoa mifano ya hali hiyo.
Hata hivyo, wakati akikabidhiwa rasmi kazi ya kuongoza vita dhidi ya dawa za kulevya na Mkuu wa Dar es Salaam, Paul Makonda Jumatatu:
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, alisema taasisi yake itawashtaki kwa Jaji Mkuu, Majaji ambao waliachia watuhumiwa wa biashara ya mihadarati kinyume na sheria.
Sianga alisema wapo baadhi ya mahakimu na majaji ambao walishiriki kwa namna moja ama nyingine kuvuruga kesi za dawa za kulevya.
Alimuagiza Kamishna wa Operesheni wa Tume, Mihayo Msikela kupitia mafaili yote ya kesi za dawa za kulevya aliyodai hayakutendewa haki mahakamani.
Mihayo, hata hivyo, alisema orodha ya majaji waliotibua kesi za mihadarati kwa makusudi tayari ameshaiandaa na ataiwasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya hatua nyingine zaidi.
Sianga alisema wameandaa orodha ya mafaili yote ya kesi za dawa za kulevya hizo na kwamba wataipeleka kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya hatua nyingine zaidi.
“Sheria iliyotungwa na Bunge inatakiwa itafsiriwe kama ilivyotungwa," alisema Sianga na kulalamika "kesi zetu zinachukua muda mrefu bila sababu."
"Mtu anakaa tu kwa sababu mimi ni jaji, anasema nitakaa katika kesi yangu nitaamua ninavyotaka".
Prof. Majamba, hata hivyo, alisema "kuna utaratibu wa kuweza kuzungumza masuala hayo (ya kukosoana) kiutu uzima bila kuficha mambo, bila hivyo nchi haitakwenda vizuri.”
TUMENYAMAZA KIMYA
Aidha, Prof. Majamba alisema yapo mambo ambayo hayaendi vizuri na kutolea mfano kitendo cha serikali kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa, na baadhi ya viongozi kutoa matamko ambayo kimsingi yanawachanganya wananchi.
“Katiba ipo wazi," alisema. "Mikutano ya kisiasa imesitishwa, (wanasheria) tumenyamaza kimya tu."
"(Kwingineko) baadhi ya viongozi wa serikali wanashutumu Bunge na Mahakama hadharani, tunapeleka ujumbe gani kwa wananchi?”
Prof. Majamba alisema wakati wa kuahirishwa kwa mkutano wa Bunge mapema mwezi huu, Spika Job Ndugai alielezea utaratibu unaotakiwa kutumika kabla ya kumkamata Mbunge, lakini wakati huohuo, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe alikuwa ameitwa akahojiwe.
Aliishauri Wizara ya Katiba na Sheria kuingilia kati kuweka muongozo ili viongozi wawe wanazingatia sheria na katiba katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akijibu hoja hizo, Dk. Mwakyembe alisema mikutano ya hadhara ya kisiasa ndiyo tu iliyozuiwa na kwamba nia ni kuruhusu serikali na wananchi wajikite katika kufanya shughuli za maendeleo badala ya kulumbana kwenye majukwaa ya kisiasa.
Alisema Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika wagombea walioshindwa huanza kuitisha mikutano ya hadhara na kushambulia kwa maneno watawala, na matokeo yake inakuwa vurugu zinazosababisha serikali kushindwa kutekeleza majukumu yake vizuri.
“Uchaguzi wa Marekani umefanyika juzi hapa, Clinton (Hilarry) alipata kura nyingi za ‘majority votes’ (wananchi) lakini Donald Trump akamshinda Clinton kwa kura za ‘electoral college’ (kete za urais); akatangazwa kuwa Rais," alisema Dk. Mwakyembe na kuuliza: "Lakini umeona hata siku moja Clinton akifanya mikutano ya wananchi kumpinga Trump?"Nipashe
0 comments:
Post a Comment