MOTO WA MADAWA YA KULEVYA WAZIDI KUSAMBAA KWA KASI, VITA YAHAMIA MIKOANI
MOTO dhidi ya dawa za kulevya umezidi kusambaa kwa kasi nchini, baada ya watu 247 kukamatwa katika mikoa ya Dodoma na Lindi.
Mkoani Dodoma, watu 168 wamekamatwa na Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Dodoma kwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi na cocaine.
Mkuu wa wilaya hiyo, Christina Mndeme, alisema jana kuwa kati ya watuhumiwa hao waliomakatwa, 140 ni wanaume na wanawake ni 28.
Aliwataka viongozi wa ngazi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ikiwa na pamoja kufanya msako kwenye maeneo yote watakayoyabaini kuna dawa hizo.
Alisema katika Manispaa ya Dodoma maeneo ambayo yamekuwa kinara kwa matumizi ya dawa hizo ni kata za Makutupora, Veyula, Msalato, Majengo, Chadulu, Miyuji, Zuzu, Mbabala na Chinangali West. Zingine ni Madukani, Hazina, Mlezi na Airport.
“Ninawaomba zoezi hili liwe kwa watu wote na lisiwe l Jeshi la Polisi peke yake, hivyo basi nyinyi wa mitaa vaeni silaha zote za kuingia kwenye mapambano haya mkizingatia kuwa hapa ni mkoa ambao upo katikati na ninaamini dawa hizi zinaweza kuwa sehemu ya njia zinakopitishwa,” alisema Mndeme.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Manispaa ya Dodoma, Matwiga Kyalya, alisema watahakikisha wanashiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya ambayo ilianzishwa na Rais John Magufuli kwa maelezo kuwa ni janga la taifa.
Kyalya alisema pamoja na changamoto kubwa walizonazo wenyeviti hao, lakini watahakikisha wanashiriki katika kuwabaini wanaojihusisha na dawa hizo ukizingatia kuwa watumiaji wengi wanaishi kwenye mitaa ambayo wanaiongoza.
Naye, Mkuu wa Polisi Dodoma Mjini, Daniel Shilah, alisema wapo tayari kupokea taarifa juu ya watu wanaojihusisha na dawa hizo hata kama wamo askari wake.
79 MBARONI LINDI
Mkoani Lindi, watu 79 walikamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali, ikiwamo kujihusisha na dawa za kulevya.
Tuhuma nyingine ni uuzaji utengenezaji gongo, kukutwa noti bandia na silaha katika operesheni maalum ya kupambana na dawa za kulevya.
Kamanda wa polisi mkoani Lindi, Renatha Mzinga, alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni hiyo iliyoanza Januari Mosi 2017 hadi Februari 13 katika wilaya za Lindi na Kilwa.
Alisema walikamata aina mbali mbali za dawa za kulevya zikiwamo heroin gramu 50, gongo lita 734, mitambo 14 ya kutengenezea pombe hiyo, bangi kilo 49 na gramu 987, kete (124), puli 81 na mbegu za bangi gramu 200.
Mzinga alifafanua kuwa watuhumiwa 73 walikamatwa na pombe, mitambo 14 ya kutengenezea gongo, watatu na bunduki aina ya SMG namba 763529 na magazine mbili zikiwa na risasi nane. Alieleza kuwa watatu ni raia wa Somalia wanaodaiwa kuingia nchini kinyume cha sheria.
Aliongeza kuwa walikamata Sh. 25,835,000 na kuwa kati ya hizo Sh. 780,000 zilitolewa na watuhumiwa wakitaka kuwahonga askari ili wawaachie, na kwamba Sh. 175,000 zilikuwa fedha bandia.
Pia alisema walikamata Sh. 24,880,000 ambazo zilikuwa kati ya Sh. 70,000,000 zilizoibwa kutoka Chama cha Ushirika cha Msingi Nahuka Huka Amcos, zilizotakiwa kulipwa kwa wanachama.
KASI YA KUKAMATA
Kamata kamata imetangazwa pia katika mikoa kadhaa nchini kuhusiana na watuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya huku wengine wakiendelea kusakwa.
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limetangaza kwamba limeshawatia mbaroni watu 17 wanaodaiwa kujihusisha na dawa hizo.
Mkoani Iringa, Jeshi hilo limesema limewatia mbaroni watuhumiwa 21 katika Manispaa ya Iringa, na kwamba saba wanatuhumiwa kujihusisha na utumiaji wa heroine na wengine 14 wakituhumiwa kujihusisha na utumiaji wa aina nyingine.
Watuhumiwa 47 wametajwa na kutiwa mbaroni mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya wakati katika mkoa wa Mwanza mtu mmoja alikamatwa jijini Mwanza Februari 2, mwaka huu akituhumiwa kukutwa na dawa aina ya heroine pinchi 240 na ndogo mbili, huku Jeshi la Polisi likisema kuwa linausaka mtandao wote.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao umekuwa kitovu cha vita hiyo iliyochochewa na mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda, orodha ya majina ya watuhumiwa 184 ilikabidhiwa na Makonda mwenyewe kwa Jeshi la Polisi na kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, sambamba na kuwataja baadhi yao kwa majina.
Orodha ya kwanza ya majina 22 na ya pili ya majina 65 alizikabidhi kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na ya tatu ya majina 97 alikabidhi kwa Sianga. Miongoni mwa aliowataja Makonda ni wanasiasa, viongozi wa dini na wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Kamishna Sirro alisema kuwa jeshi hilo limeshawatia mbaroni watuhumiwa 311 na kwamba baadhi yao walikutwa wakiwa na vidhibiti vya kete za dawa hizo, akiwamo msanii Wema Sepetu ambaye ameshafikishwa mahakamani. Aliongeza kuwa watuhumiwa 100 wanaendelea kusakwa.
0 comments:
Post a Comment