MWANAMKE MJANE ALIVYOPATA UJASIRI NA KUTUMIA DAKIKA 13 KUWALIPUA VIGOGO KWA RAIS MAGUFULI
MAMA mjane aitwaye Swabaha Mohamed alitumia takribani dakika 13 kumshitakia Rais John Magufuli juu ya watu mbalimbali aliodai kuwa wana nguvu kubwa kifedha na kutumia rasilimali zao kumpora haki yake kwa kughushi nyaraka za mirathi.
Huku akibubujikwa machozi, Swabaha alimueleza Rais Magufuli namna anavyotishiwa maisha kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa wabaya wake na pia kuzungushwa kila anakokwenda kwa nia ya kudai haki.
Tukio hilo lililowaacha katika huzuni kubwa baadhi ya mashuhuda kutokana na namna Swahaba alivyokuwa akilielezea kwa hisia kali, lilitokea jana wakati Rais Magufuli alipomaliza hotuba yake kwenye sherehe ya Siku ya Sheria jijini Dar es Salaam.
Awali, Swabaha aliyekuwa mahala pa sherehe kitambo, alisubiri Rais Magufuli amalize hotuba yake na ndipo ghafla, akatoa bango la kitambaa lililokuwa na ujumbe uliokuwa ukimsihi Rais Magufuli amsaidie asidhulumiwe haki yake inayotaka kunyang’anywa na Polisi, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mahakama.
Sehemu ya bango hilo la kitamba aliloliinua juu ili Rais apate ujumbe uliopo, lilisomeka: “Rais Magufuli naomba unisaidie. Polisi, DPP, Mahakama wanataka kuninyang’anya haki yangu”.
Awali, kitendo hicho cha nje ya utaratibu kilimponza Swabaha baada ya wanausalama kadhaa kumzonga na kujaribu kumtoa eneo hilo.
Ni hapo ndipo Rais Magufuli alipoamuru mama huyo (Swabaha) apewe nafasi ili amueleze shida yake, huku (Rais) akisema kuwa kufanya hivyo ni sahihi kwa sababu “ndiyo siku yenyewe ya mahakama”.
DAKIKA 13
Baada ya kupata nafasi hiyo, huku akilia kwa kwikwi, Swabaha alianza kusimulia kwa kueleza kuwa mumewe aitwaye Mohammed Shosi alifariki mwaka 2012 na kwamba, tangu wakati huo amekuwa akizungushwa katika Mahakama ya Wilaya mkoani Tanga kuhusiana na mirathi. Alieleza kilio chake kwa takribani dakika 13.
Swabaha alimtuhumu wakili mmoja (jina tunalo) kuwa ndiye aliyeshiriki katika kuandaa wosia bandia wa mumewe kwa nia ya kufanikisha dhuluma dhidi yake.
Alidai wakili huyo amekuwa akishirikiana na watu wenye fedha ambao wamekuwa wakitumia nguvu zao kiuchumi kukwamisha haki yake hata pale alipofuatilia kwenye maeneo yote muhimu ya kufuatilia haki yake kuhusiana na jambo hilo.
Alisema yeye ana cheti halali cha ndoa kilichotolewa mkoani Tanga, lakini kuna mbinu zimefanyika kwa nia ya kupotosha taarifa kwa kukigeuza cheti hicho kionekane ni batili.
Aidha, katika kufuatilia jambo hilo, Swabaha alisema amejaribu kufika katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ofisi ya Waziri wa Sheria na Katiba, Ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na pia katika Ofisi ya Jaji Mkuu, lakini bila ya kupata msaada wowote.
Swabaha alidai kuwa mojawapo ya mbinu nyingine za dhuluma zinazofanywa dhidi yake kwa nia ya kumdhulumu ni pamoja na kumuweka msimamizi wa mirathi ambaye ni mpangaji wa marehemu, na pia kuweka majina ya wanawake ambao siyo wa ndoa katika mirathi.
Mama huyo mjane alisema marehemu mume wake alikuwa na wanawake wawili wa ndoa na kwamba yeye na huyo mke mwenzake, kila mmoja ana cheti halali cha ndoa.
Alisema awali, alishinda kesi hiyo katika mahakama ya mwanzo, lakini baada ya kuona hivyo, watu wanaotaka kumdhulumu walikata rufani katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga na mwishowe ikatolewa hukumu iliyodai kuwa wao wameshinda kupitia hakimu aliyefahamika kwa jina la Dakika Tatu -- ambalo ni la uongo na halipo.
Alisema kutokana na kufuatilia mara kwa mara, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakimtishia kumuua kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms).
Aidha, alisema hata yeye (Rais Magufuli) alimtumia ujumbe kutoa kilio chake na akaelekezwa kwa IGP ambako licha ya kwenda huko, bado hajapata haki yake bali anapata vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu waliopania kumdhulumu.
“Mimi leo nimeamua kuja hapa nikijua kama kufungwa na nifungwe, na lolote na liwe… Mheshimiwa Rais naomba unisaidie.” Alisema Swabaha, akiomba watu hao wenye fedha wasiachwe wamdhulumu haki yake, yeye mjane kwa sababu ya umasikini wake.
MAGUFULI AMPA FARAJA
Baada ya mjane huyo kumaliza maelezo yake, Rais Magufuli alimwambia amemsikia na hapo hapo akaanza kuchukua hatua kwa kumuita IGP Ernest Mangu na kumuuliza kama anafahamu kuhusu suala la mama huyo.
IGP Mangu alikiri kulifahamu na kuongeza kuwa marehemu (mume wa Swabaha) alikuwa na wake wawili na kwamba, pia kulikuwa na mgogoro wa kifamilia, hali ambayo mwishowe imesababisha kuwapo kwa kesi za jinai.
“Kesi anazozingumzia mama huyo bado zinaendelea mkoani Tanga na nilimkabidhi DCI (Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai), ambaye naye alizungumza na Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP) kwa kuwa upelelezi ulikuwa umekamilika,” alisema Mangu.
Kuhusu mama huyo kutumiwa ujumbe wa vitisho, IGP Mangu alisema DCI bado anaendelea na uchunguzi wake.
“Ni kesi ambayo ni complex (yenye utata), inahusisha idara ya Mahakama, DPP, Polisi … na mawakili ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kuleta mgogoro huo na pia kuna wosia feki uliotengenezwa,” alisema IGP Mangu.
Mara baada ya IGP Mangu kutoa maelezo yake, ndipo Rais Magufuli alipotoa maagizo yake kuhusiana na suala hilo, na ambayo kwa kiasi kikubwa yalijaa mwanga wa matumaini juu ya kupatikana suluhu ya jambo hilo.
Mosi, Rais Magufuli alimtaka IGP kumhakikishia ulinzi wa saa 24 mjane huyo ili asidhuriwe; pili, Rais Magufuli alizitaka ofisi za DPP, AG na Jaji Kiongozi kulishughulikia kwa haraka suala hilo; tatu, Swabaha alielekezwa aende kwa Jaji Kiongozi aliyekuwapo mahala hapo pia ili apewe namba ya simu atakayokuwa akiwasiliana naye moja kwa moja kuhusiana na suala hilo; na nne, Rais Magufuli alitaka kesi ya mjane huyo ihamishiwe haraka kutoka Mahakama ya Wilaya na kupelekwa katika mahakama za juu.
“Ofisi ya DPP, AG na Jaji Kiongozi shughulikieni suala la huyu mama.
Kama kesi ipo Mahakama ya Mwanzo kule muivute haraka haraka…ishughulikiwe haraka na IGP pia uishughulikie,” alisema Magufuli.
FURAHA, KICHEKO
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata mwanga wa matumaini kutoka kwa Rais Magufuli, Swabaha alisema amefurahi mno kwa sababu alijiandaa kwa lolote ikiwamo kufungwa akipigania haki yake, lakini kilichotokea ni jambo asilokuwa ametarajia hapo kabla.
“Mimi nimewaambia, leo ni kufa au kupona… nimetoka Tanga hadi Dar kuja kumwona Rais ili nipate haki yangu. Nimemshukuru Rais Magufuli. Sijawahi kuona Rais mwelewa kama yeye, maana polisi walikuwa wananibana,” alisema na kuongeza:
“Kuna kina mama wengi Tanga wamedhulumiwa nyumba na wengine viwanja… lakini wanaogopa kuja,” alisema Swabaha. Mbali na Rais Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi, viongozi wengine waliokuwapo katika sherehe hiyo ya Siku ya Sheria jana ni Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma; Spika wa Bunge, Job Ndugai; Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrisson Mwakyembe; IGP Mangu na Kaimu DCI, Robert Boaz.
0 comments:
Post a Comment