Rais John Magufuli akimsikiliza, Sobha Mohamed, aliyejitokeza kuelezea kero anazopata katika Mahakama kuhusu kesi yake ya mirathi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mahakama, Dar es Salaam jana. Kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Spika wa Bunge, Job Ndugai,
Rais Dk John Magufuli amewanyoshea kidole Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa ndio chanzo cha serikali kupoteza kesi nyingi kutokana na kupindisha na kuwasilisha ushahidi hafifu mahakamani.
Pia ameagiza mamlaka zinazohusika na kusikiliza kesi, mhalifu ambaye anakamatwa na vidhibiti, kesi yake isikilizwe siku hiyo na hukumu kutolewa siku hiyo hiyo badala ya ilivyo sasa waendesha mashitaka wanarefusha kesi hizo kwa kisingizio cha ushahidi kutokamilika.
Alitumia maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika Dar es Salaam jana kuwanyooshea kidogo majaji katika maamuzi yao waliyoyafanya kuhusu mahakimu 28 waliokuwa wanatuhumiwa kwa makosa ya rushwa kuachiwa huru wote.
Aliziagiza pia ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuhakikisha kwamba zinaacha kugombana, kwani nazo zimekuwa zinachangia kutengeneza ushahidi hafifu na hivyo kufanya serikali kupoteza kesi mahakamani.
Awapasha Polisi, Takukuru
Alisema Polisi na Takukuru ambao ndio wenye jukumu la kufanya upelelezi wamekuwa hawafanyi upelelezi na wamefikia hatua wanamkamata mtuhumiwa na vidhibiti, lakini mtuhumiwa anashinda kesi.
Alitoa mfano kuwa mtuhumiwa wa dawa za kulevya anakamatwa na dawa za kulevya, lakini akifikishwa mahakamani upande wa mashitaka unashindwa kuendelea na kesi kwa kisingizio kuwa upelelezi haujakamilika.
“Mtuhumiwa anakamatwa na jino la tembo, lakini wanadai upelelezi bado kukamilika, au kakamatwa na dawa za kulevya baada ya muda dawa hizo zikipelekwa kwa mkemia inabainika kuwa ni unga wa muhogo wa huko Sumbawanga,” alisema Rais Magufuli.
Alisema kutokana na ushahidi kutokuwepo, mahakama inalazimika kumwachia huru mtuhumiwa; hivyo akaonya kuwa umefika wakati vyombo hivyo vijitathmini na vibadilike.
Aliagiza kuwa mtu akishikwa na vidhibiti, siku hiyo hiyo kesi yake isikilizwe na imalizike, na kama kuna mtu atajitokeza kumtetea naye aunganishwe kwenye hiyo kesi wote waende jela. Serikali haijalipwa trilioni 7.5/-.
Alisema majaji watafute namna ambavyo wanaweza kutumia sheria watuhumiwa wa namna hiyo wahukumiwe kwenda jela, “sheria huwa inasema kifungo au faini, sasa nyinyi hawa wenye vidhibiti mnawahukumu vyote pamoja.”
Alibainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2016, serikali haijalipwa kiasi cha Sh trilioni 7.5 licha ya kushinda kesi za ukwepaji kodi zilizokuwa zinawakabili washitakiwa mbalimbali.
“Haiwezekani mwekezaji anachimba madini yetu, kodi halipi, anashitakiwa mahakamani anashindwa, halafu pesa haitolewi. Sasa tujiulize, kama utoaji haki unaakisi ujenzi wa uchumi wa nchi ni kwa kiasi gani kesi zenye thamani ya Sh trilioni 7.5 zimeathiri uchumi?” Alihoji Rais Magufuli.
Ugomvi wa AG, DPP
Rais Magufuli alitoboa kwamba ofisi hizo mbili muhimu katika utoaji wa haki nchini watendaji wake wamekuwa wanagombana, jambo ambalo linafanya serikali ishindwe kesi kutokana na ushahidi hafifu unaowasilishwa na watendaji wa ofisi hizo.
Alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP), Biswalo Mganga wamekuwa wakigombana wenyewe kwa wenyewe na akawataka watendaji wa ofisi hizo kujitathmini wenyewe, ni wapi wanakosea na wapi wanakwenda kwa kuendekeza ugomvi huo.
“Waziri unafahamu ugomvi wa ofisi hizi mbili, cha ajabu wote hawa wanatoka mkoa mmoja na yawezekana wilaya moja, sijui wanagombea nini. Kama ni madaraka wote ni wateuliwa wa Rais, kama ni kasima tafuteni suluhisho,” alisema Rais Magufuli.
Alionya kuwa bila kutafuta suluhisho, serikali itaendelea kupoteza kesi kutokana na ushahidi laini unaowasilishwa mahakamani.
Alisema wakati mwingine ushahidi unakuwa laini hadi kumfanya jaji aahirishe kesi kutoa nafasi kwa mawakili wa serikali kwenda na ushahidi mzito, lakini hawafanyi hivyo.
“Kwa hali unakuta ushahidi upo, lakini tunashindwa kwa sababu ushahidi unaopelekwa mahakamani ni mwepesi kutokana na matatizo yaliyopo katika ofisi hizi mbili,” alisema.
Ahoji mahakimu kutofungwa Katika hotuba yake, Rais Magufuli alihoji mahakimu 28 walishitakiwa kwa tuhuma za kupokea rushwa, lakini akashangaa kwamba katika kesi zote hizo hakuna hakimu hata mmoja aliyetiwa hatiani na kufungwa.
Alisema kwa hali ya kawaida raia ambao sio wanasheria wanakuwa na maswali mengi kuhusu maamuzi hayo ya mahakama. Alisema yawezekana upelelezi wa polisi haukufanywa vizuri au ushahidi ulikuwepo, lakini haukufikishwa vizuri mahakamani.
“Yawezekana mawakili wa pande zote walikula njama kuhakikisha hakuna ushahidi unaotolewa dhidi ya mahakimu hao au yawezekana majaji au mahakimu wenzao waliamua kuwaachia huru wenzao kuthibitisha ule usemi kuwa kesi ya ngedere unampelekea nyani,” alibainisha Rais Magufuli.
Alisema jambo hilo ni changamoto kwa Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma na alimtaka ashughulikie suala hilo kwani mbele ya wananchi maamuzi hayo ya mahakama yanaleta shaka na akawataka majaji wajipange kuondoa changamoto hizo wanapoanza mwaka mpya wa mahakama.
Alisema Watanzania wangefurahi hata mahakimu wawili wangefungwa.
Rais Magufuli pia alisema kuna madudu mengi yanafanywa ndani ya Idara ya Mahakama, lakini yamekuwa yanapita kimya kimya na akatolea mfano baadhi ya majaji kuhusishwa kupokea fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu (BoT), lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya majaji hao.
Alisema mambo kama hayo yanaumiza kuona yanafanywa na chombo ambacho kina dhamana ya kutoa haki ya kisheria kwa wananchi.
Alisema kuna majaji wachache sio waadilifu ambao wamekuwa wanaichafua sura ya mahakama “Yawezekana hapa asilimia 99.99 ni wasafi, lakini wanachafuliwa na hawa wachache ambao ni asilimia 0.00. Jaji Mkuu tafadhali chukua hatua dhidi ya watendaji hawa wachafu,” alisema Magufuli na kuongeza kuwa ameyasema hayo kwa sababu mahakama haiongozwi na malaika.
Alisema kuna majaji kutokana na uchafu wao, tangu waanze kusikiliza kesi, Serikali haijawahi kushinda kesi zinazofikishwa “Unajiuliza hivi kesi zote huwa hazina ushahidi? Ashangaa kuhusu ajira mpya.
Akijibu maombi ya Jaji Juma kutaka mahakama iruhusiwe kuajiri watumishi wapya wapatao 900, Rais Magufuli alishangaa kwani kwa sasa taasisi hiyo ina watumishi 6,500 ambao ni wengi kuliko idara nyingine serikalini na akahoji iweje watake kuongeza watumishi.
“Ninyi ndio wengi kuliko idara nyingine yoyote, kwa mfano mnataka walinzi wa nini, hivi polisi hawalindi mahakama, kama hawalindi kwa nini msitoe kwa kampuni binafsi za ulinzi?Angalieni nani anahitajika katika mageuzi haya mnayofanya,” alisema Rais Magufuli.
Pia aliishauri idara hiyo kuhakikisha kwamba inaunganisha baadhi ya shughuli ambazo zilikuwa zinafanywa na watu wanne ifanywe na mtu mmoja na aongezewe mshahara badala ya kutaka kuongeza watumishi wengine wapya.
Alisema inamuwia vigumu kuongeza ajira za umma kwa sababu Serikali inatumia Sh bilioni 600 kila mwezi kuwalipa wafanyakazi 546,166 kila mwezi na bado kuna kulipa madeni mengine jambo ambalo linafanya serikali inalemewa.
Alitoa mfano kuwa mwezi uliopita serikali ilifanya malipo ya mishahara na kulipa madeni yenye thamani ya Sh bilioni 955 wakati makusanyo kwa mwezi ni Sh trilioni 1.2. Alitahadharisha kuwa suala la kuongeza watumishi wapya linaweza kufanya Serikali ishindwe kuwalipa mshahara.
Alisema atawaruhusu mahakama kuajiri watumishi wa kada zinazotakiwa tu na akamtaka jaji mkuu kuhakikisha kwamba kwa nafasi ambazo sio muhimu wafanye mageuzi waangalie namna ya kuzijaza nafasi hizo kwa kutumia watumishi waliopo.
Ataka mawakili kuwa wazalendo Rais Magufuli pia aliwaagiza mawakili kuhakikisha wanakuwa wazalendo na wawatose watuhumiwa wabaya na wasiwatetee.
Alisema wahalifu hao wabaya wakitaka wawatetee, mawakili wachukue fedha zao lakini wakifika mahakamani wawaruke “Chukueni fedha zao, lakini mkifika mahakamani wageukeni,” aliwaambia.
Pia aliwataka mawakili hao kupitia chama chao, Tanganyika Law Society (TLS) kuacha kujihusisha na siasa badala yake wasiwe na vyama katika kutekeleza majukumu yao.
Alisema ndani ya TLS kumekuwa kama chama cha siasa, hadi kwenye kampeni za uchaguzi wanapigana mkumbo watu wenye mlengo tofauti wa vyama vya siasa. Alisema yeye hatakuwa tayari kuteua wakili kuwa jaji ambaye anashabikia vyama vya siasa.
“Jijengeeni heshima kwa kuwa neutral (msiwe na upande), hiyo itawajengea heshima,” alisema Rais Magufuli.
Mwanamama azua tafrani, aibukia kwa Rais
Katika hatua nyingine, mwanamke mkazi wa Tanga, Sobha Mohammed alizua tafrani baada ya kuibuka mara tu Rais alipomaliza hotuba yake akiwa na bango, lakini kabla ya kufika mbele ya meza kuu alikumbana na rungu la walinzi wa rais.
Mama huyo alirejeshwa nyuma kuondolewa eneo hilo huku watu waliokuwapo hapo wakishuhudia, na wakati huo Rais Magufuli alikuwa katika mazungumzo na Kaimu Jaji Mkuu, lakini baada ya muda mfupi kulitokea agizo la Rais la kutaka aachwe na apelekwe kwao atoe kilio chake.
Alipofika mbele, mama huyo alianza kutoa kilio, na akielezea madhila ya kudhulumiwa haki zake katika kesi iliyofunguliwa mkoani Tanga na kwamba amefika katika ofisi mbalimbali za wahusika wa masuala ya kisheria kuanzia Polisi hadi kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe.
Baada ya kumsikiliza mama huyo, Rais Magufuli aliagiza, “Ofisi ya DPP, AG na…. Jaji Kiongozi si ndio msimamizi wa kesi zote za chini chini, si ndio bwana. Shughulikie suala la huyu mama. Kama kesi iko Mahakama ya Mwanzo kule muivute huku haraka haraka, ishughulikiwe haraka.
Na AG pia mshughulikie, lakini na pia mumlinde ili asidhuriwe kwa kifo cha aina yoyote. Chukua jina lake, lakini pia mtafutieni Polisi ili amlinde. Lakini mhakikishe usalama wake. Jaji Kiongozi chukua simu yake. Na mama njoo uchukue simu ya Jaji Kiongozi, umpigie moja kwa moja.”
Kauli ya Rais ilipokewa kwa shangwe na nderemo. Profesa Lipumba apongeza Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kitendo cha Rais kuyasema mambo hayo hadharani hapo, kinaonesha kuwa anataka kupata nguvu ya kisiasa ili wananchi wajue kinachoendelea katika mfumo wa utoaji wa haki nchini.
“Kwa mfano, serikali imeshinda kesi na inatakiwa kulipwa shilingi trilioni 7.5, lakini hazijalipwa tatizo liko wapi? Alihoji Lipumba.
Profesa Lipumba alisema kuna haja ya watendaji ndani ya mfumo wa mahakama na vyombo vingine vya serikali kuhakikisha kwamba wanabadilika ili mapungufu aliyoyaainisha Tais yasiwepo tena.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ RAIS MAGUFULI AWATOLEA UVIVU POLISI, TAKUKURU NA MAHAKAMA KWA UTENDAJI MBOVU
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment