WAFANYABIASHARA WA MADAWA YA KULEVYA WAIBUKA NA MBINU MPYA YA KUVUSHA MADAWA KWA NCHI JIRANI
Maafisa wa Marekani wanaoshika doria mpakani, wamegundua manati kubwa ambayo ilikuwa imefungamanishwa na ua ulio kwenye mpaka wa taifa hilo na Mexico.
Manati hiyo inaonekana kuundwa mahsusi kwa ajili ya kurusha dawa za kulevya hadi Marekani.
Marekani imekuwa ikikabiliana sana na walanguzi wa mihadarati kutoka Mexico pamoja na wahamiaji.
Rais Donald Trump ameahidi kujenga ukuta mrefu sana kuzuia hilo.
Manati hiyo kubwa iligunduliwa na maafisa kusini mashariki mwa Tucson, Arizona, wiki iliyopita.
Wanasema waliwaona wanaume kadha wakitawanyika na kutoroka walipogundua kwamba maafisa hao walikuwa wanafika.
Maafisa hao walipokagua eneo hilo, waligundua vifurushi viwili vya bangi, vilivyokuwa na bangi ya jumla ya kilo 21.
Vifurushi hivyo vilikuwa bado havijarushwa.
Manati hiyo ambayo ilikuwa imejengwa upande wa Mexico wa ua ilibomolewa.
Hakuna aliyekamatwa kuhusiana na kisa hicho.
Takriban umbali wa maili 650 kati ya maili 1,100 (1,770km) za mpaka wa Mexico na Marekani tayari kumejengwa ua au ukuta.
Trump ameahidi kujenga ukuta mrefu lakini walanguzi wamekuwa wakitumia ubunifu katika kutumia njia za kufikisha madawa Marekani.
Miongoni mwa njia hizi ni kutumia ndege ndogo zisizo na marubani na wakati mwingine kuchimba njia za chini kwa chini zinazofika hadi Marekani.
Mwezi Machi, maafisa waligundua njia ya chini kwa chini ya umbali wa mita 380 ambayo ilikuwa imetoka kwenye mgahawa mmoja Mexico hadi kwenye jumba moja California.
0 comments:
Post a Comment