Changamoto hiyo imeibuka siku chache baada ya serikali kutoa katazo la bodaboda kuonekana barabarani kwenye baadhi ya kata za wilaya hiyo inapofika saa moja usiku.
Kata zilizoamriwa kufuata utaratibu huo ni Mkamba, Nyamato na Kimanzichana, ikiwa ni moja ya mikakati ya kukabiliana na matukio ya ujambazi yaliyokithiri katika maeneo hayo.
Wakizungumza na Nipashe kwenye vijiji vya kata hiyo juzi, madereva hao walisema zuio hilo limesababisha ukata na wengi wao kupoteza ajira kutokana na kunyang'anywa pikipiki na 'mabosi' wao.
Shaban Jafar, dereva wa bodaboda, alisema baadhi ya madereva wenzake wamevunjiwa mikataba na wamiliki kutokana na kutowasilisha kiwango cha fedha walichokubaliana katika mikataba hiyo.
Alisema: "Ukikamatwa umebeba abiria baada ya saa moja usiku, unapigwa na polisi, chombo chako kinachukuliwa na unalipishwa faini ya sh. 40,000 na risiti huku hatupewi."
"Kiukweli tunafanya kazi katika mazingira magumu sana. Mkataba unakutaka utoe kila siku Sh. 10,000, lakini kutokana na kuzuiwa kufanya kazi usiku, unajikuta mtu unaambulia Sh. 5,000 au 4,000. Hii imesababisha watu kuvunjiwa mikataba.
"Si bodaboda wote ni wezi, kinachotakiwa waachiwe wafanye kazi mpaka saa tano usiku. Kwanza hilo tangazo hatujui nani aliyelitoa, tuliona magari ya matangazo yakitangaza marufuku bodaboda usiku na hatujui ni kauli kutoka kwa nani.
"Haki itendeke, sisi siyo watu wanaojihusisha na ujambazi, lakini cha kushangaza kata za Mkamba, Kimanzichana na Nyamato tunazofanyia kazi ndizo zimetakiwa kutoendelea kutoa huduma hiyo ifikapo saa moja usiku."
Aidha, uamuzi huo wa serikali umedaiwa kusababisha adha kwa baadhi ya wananchi kushindwa kurejea katika makazi yao na kuwalazimu kulala kwenye nyumba za wageni kutokana na kukosa usafiri wa bodaboda usiku kwenda kwenye maeneo ambayo daladala hazifiki.
"Ukienda kutafuta riziki jijini Dar es Salaam, ukachelewa kurejea nyumbani, inakubidi ulale nyumba za wageni ili usubiri pakuche uende kijiji kwa sababu hakuna bodaboda wa kukubeba usiku," alisema Almas Hemed, mkazi wa Kimanzichana.
Alisema kuwa tangu utaratibu huo uanze, hali imekuwa mbaya hasa kwa wakazi wa maeneo ya vijiji ambavyo viko mbali na barabara kuu ya Kilwa na hawawezi kutembea kutokana na umbali mrefu.
Mkazi mwingine wa Kimanzichana, Jumanne Jabir, alisema si vijiji vyote ambavyo magari (daladala) yanafika, hivyo watu wanalazimika kutumia usafiri wa bodaboda.
Alisema kuzuiwa kwa usafiri huo inapofika saa moja usiku, kumewafanya waishi kwa shaka kwa kuwa ukionekana upo katika chombo hicho baada ya muda huo, unapigwa na polisi.
Mkazi mwingine wa Mkuranga, Zuwena Jumanne, alisema kitendo cha kuwazuia bodaboda kufanya kazi usiku kinawapa wakati mgumu pale kunapotokea mtu kuhitaji huduma za dharura, ukiwamo ugumu wa kuzifikia hospitali pale panapohitajika matibabu kwa mgonjwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Gilberto Sanga, akizungumza na Nipashe mjini hapa juzi, alisema hana taarifa juu ya zuio hilo.
Alisema halmashauri ilikuwa haijaazimia utekelezaji, lakini akakiri kuwa waliishakaa vikao kwa ajili ya utekelezaji huo.
Alisema huenda agizo la kuzuia bodaboda kufanya kazi usiku limetolewa na ngazi za juu kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya bado halijatoa tamko kuhusu suala hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lianga, pia alisema hana taarifa za askari wake kupiga madereva wa bodaboda huku akidai hamjui aliyetoa agizo la kuzuia bodaboda kufanya kazi baada ya saa moja usiku.
Amri kama hiyo imetolewa pia jijini Dar es Salaam ambako Polisi Kanda Maalumu imetaka madereva wa bodaboda kuacha kufanya shughuli hiyo ifikapo saa sita usiku ili kupunguza uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 24, mwaka huu, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema jeshi hilo limebaini wahalifu wengi hutumia mwanya katika muda huo kutenda uhalifu; ikiwa ni pamoja na kuwadhuru waendesha pikipiki.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment