HUYU NDIYE TUNDU LISSU MWENYE MIPANGO YA KWENDA GEREZANI KUFUNGWA !!
MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, amebisha hodi gerezani!
Hivyo ndivyo inavyoweza kuelezwa kutokana na andiko lake kupitia mitandao ya kijamii lililokuwa na ujumbe mahsusi kwenda kwa mawakili wenzake akiwataka wampigie kura huku akidai kuwa yeye anakwenda ‘mahabusu’ au gerezani.
Lissu aliashiria hayo kupitia andiko lake hilo ikiwa ni muda mfupi kabla ya kukamatwa na polisi mishale ya asubuhi wakati akiwa nyumbani kwake, eneo la Area C mjini Dodoma, jana.
Katika andiko lake hilo lililosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Lissu alidai kwamba alikuwa mbioni kukamatwa na askari waliomfuata nyumbani kwake.
Akalihusisha tukio hilo na joto la uchaguzi wa Chama cha Wanasheria (TLS) unaotarajiwa kufanyika kesho jijini Arusha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alithibitisha madai ya Lissu kuwa yuko mbioni kukamatwa baada ya kukiri kuwa ni kweli walimtia mbaroni jana saa 5:00 asubuhi na kisha kumsafirisha kwenda jijini Dar es Salaam alikokuwa akitafutwa na jeshi lao katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Awali, kabla ya uthibitisho wa Kamanda Mambosasa, Lissu alieleza kupitia andiko lake kuwa amefuatwa na askari na kwamba, yuko mbioni kukamatwa ili mwishowe kwenda gerezani au mahabusu.
Hata hivyo, aliwasihi mawakili wenzake kuwa hata kama atakamatwa na kwenda huko mahabusu au gerezani, wasiyumbishwe bali wajitokeze kwa wingi kwenda Arusha ili aongoze TLS.
“Ninawapa taarifa kwamba nimefuatwa nyumbani na askari wawili kutoka ofisi ya RPC Dodoma. Sijazungumza nao bado, lakini ni wazi wana maagizo ya kunikamata na kunizuia kuja Arusha kwenye uchaguzi,” alisema Lissu katika sehemu ya ujumbe wake huo.
Aidha, aliwasihi mawakili wenzake wampigie kura na pia kuwachagua wagombea wengine wenye msimamo kama wake wa kutokubali kujipendekeza bali kupigania haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia.
“Wameshindwa kuzuia uchaguzi wetu mahakamani. Wito wangu kwenu mawakili wa Tanzania, nendeni Arusha mkachague viongozi wa TLS watakaopigania haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia,” alisema Lissu kupitia ujumbe wake huo.
Aliongeza kuwa hata mkewe amemtaka aende Arusha kushiriki uchaguzi huo wa TLS ili ashinde na kuwa kiongozi wa chama hicho na pia kuwezesha kuchaguliwa kwa viongozi wengine wenye msimamo kama wake.
“Nendeni mkapige kura…mimi naenda mahabusu, au gerezani. Nawaombeni kura zenu ili niwaongoze katika kipindi hiki kigumu,” alisema Lissu.
Katika uchaguzi huo wa TLS, Lissu ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya urais, wagombea wengine wakiwa ni Lawrence Masha, Victoria Mandari, Francis Stola na Godwin Mwapongo.
ALIVYOKAMATWA DODOMA
Awali, baada ya kuona kile alichokiandika Lissu, Nipashe ilimuuliza Kamanda Mambosasa juu ya taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Katika ufafanuzi wake, Mambosasa alikiri kukamatwa kwake kutokana na maelekezo waliyopewa kutoka jijini Dar es Salaam.
“Tumemkamata Lissu muda wa saa 5:00 asubuhi (jana). Na hivi sasa tayari tumemsafirisha kwenda jijini Dar es Salaam,” alisema Kamanda Mambosasa.
Akieleza zaidi, Mambosasa alisema polisi walianza kwa kupiga kambi katika nyumba ya Lissu na baada ya kumkamata, walimfikisha katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Dodoma kabla ya kumpakia kwenye gari na kumsafirisha kuelekea Dar es Salaam.
KAMANDA SIRRO ATAJA SABABU 3 ZA KUMKAMATA
Akizungumza na Nipashe kuhusiana na kukamatwa kwa Lissu jana, Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Sirro, alisema ni kweli wao ndiyo waliotoa maelekezo akamatwe.
Akieleza zaidi, Kamanda Sirro aliainisha sababu tatu za kuamuru kukamatwa kwa Lissu, ambazo ni pamoja na kutaka afikishwe mahakamani; kukosekana kwake hata kupitia simu yake ya mkononi baada ya kufanya jitihada kubwa za kumtafuta na pia, kumkamata kwa kutoonekana baada ya kutakiwa aripoti polisi juzi (Machi 15, 2017) kutokana na kesi yake inayohusiana na uchochezi.
Akifafanua mambo hayo yaliyowalazimu kuagiza Lissu akamatwe akiwa Dodoma, Kamanda Sirro alisema kuwa juzi mbunge huyo alitakiwa kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam baada ya kupewa dhamana katika kesi ya uchochezi, lakini hakufanya hivyo.
Alisema kuwa awali, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuta kesi hiyo ya uchochezi dhidi yake, mbunge huyo alirudishwa polisi na kupewa dhamana na ndipo alipotakiwa kuripoti polisi juzi ili taratibu nyingine ziendelee, lakini hakutokea.
“Ni kweli tumetoa amri ya kukamatwa na kuletwa Dar es Salaam ili tumfikishe mahakamani kwa sababu jana (juzi) ilikuwa siku yake ya kuripoti na leo (jana) afikishwe mahakamani… lakini hakufanya hivyo,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema kuwa awali, baada ya Lissu kushindwa kufika kituoni, walijaribu kumtafuta ikiwamo kupitia simu, lakini simu zake zilionyesha kuwa zimezimwa.
“Leo (jana) tulipoona kimya, ndipo tukawasiliana na wenzetu (Polisi Dodoma) kuwataka wamkamate na kumleta Dar es Salaam ili afikishwe mahakamani,” alisema Kamanda Sirro.Nipashe
0 comments:
Post a Comment