JE WAJUA NYUMA YA PAZIA KILICHOMKUTA NAPE NNAUYE BAADA YA KUNG'OLEWA UWAZIRI ?.
KUONDOLEWA kwa Nape Nnauye katika wadhifa wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kisha saa chache baadaye kutishiwa bastola wakati akielekea kuzungumza na waandishi wa habari, kumejenga taswira pana.
Taarifa kutoka ndani ya mifumo ya Serikali zinaeleza kuwa awali Nape alisikika akilalamika kwa watu wake wa karibu, kwamba anajua Rais Dk. John Magufuli ana mpango wa kumwondoa kwenye baraza lake la mawaziri.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, malalamiko yake hayo yalianza kusikika hata kabla ya sarakasi za kiongozi mmoja wa Serikali kuvamia kituo cha televisheni na redio cha Clouds.
Watu wa karibu na Nape wanasema kuwa alipata kufikisha malalamiko yake hayo kwa baadhi ya viongozi wastaafu ambao wamepata kutumikia nyadhifa za juu serikalini.
Ingawa hakuna chombo chochote kilichokuwa tayari kuthibitisha hilo, lakini zipo taarifa zinazodai kuwa mwelekeo wa Nape kutenguliwa uwaziri ulitokana na mwanasiasa huyo kupishana misimamo na uongozi wake wa juu.
Taarifa kwamba Nape aliliona anguko lake, zinathibitishwa na maandiko yake mwenyewe kupitia akaunti yake ya twitter.
Andiko lake la hivi karibuni ni lile la Machi 20, mwaka huu ambalo linasomeka; “No longer at Ease!” (hakuna lisilo na mwisho).
Siku hiyo hiyo aliandika tena; “Each day is a day of decision and our decisions determine our desitiny!” (kila siku ni siku ya uamuzi, na maamuzi yetu huamua mwisho wetu)
Akandika tena “Mungu mkubwa!“ Na siku hiyo hiyo alituma ujumbe unaosemeka; “Majaribu huja ili kutuinua kutoka utukufu hadi utukufu. Kikubwa tusikate tamaa! Utukufu mkubwa upo mbele! Kwaresma njema.”
Machi 18, mwaka huu aliandika; “Chura akipigwa teke…” na Machi 14 akaandika “Brand hulindwa!”
Machi 9 aliandika; “Criticism may not be agreable but its necessary. It fulfils same function as pain in the body. It calls atention to an unhealthy state of things (ukosoaji unaweza usikubalike lakini ni muhimu. Unafanya kazi sawa na maumivu mwilini. Inakidhi kazi ile ile ya maumivu ya mwili. Ni wito wa tahafari kwa hali mbaya ya mambo)
Ni nyakati kama hizo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimfutilia Nape, wanasema ndipo alipoonekana hadharani kuikosoa Serikali tofauti na siku za nyuma.
Mfano mmojawapo ni wakati wa sakata la dawa za kulevya alipoonekana wazi kumkosoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliyeibuka hivi karibuni na orodha ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, wakiwamo wasanii.
Nape alishauri hatua zinazochukuliwa ziepuke kuharibu nembo ya biashara aliyojijengea msanii husika kwa sababu ni gharama kubwa kuirejesha.
Siku chache baadae, Rais Magufuli alisikika akisema vita ya dawa za kulevya haina umaarufu. Pasipo kutaja jina, alieleza kushangazwa na wale waliokuwa wakiwatetea watuhumiwa.
Ni tangu wakati huo inaelezwa kuwa Nape amekuwa akiandika ujumbe mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii na hivyo kuzua gumzo.
Ukiachilia mbali kuandika ujumbe kwenye akaunti yake ya twitter, pia Nape alionekana kutoa kauli nzito zenye kuashiria kukata tamaa kuitumikia nafasi hiyo.
KUVAMIWA CLOUDS
Tofauti na misimamo ya Nape katika siku za nyuma ambayo ilijiegemeza zaidi kuitetea Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika tukio la uvamizi wa kituo cha Clouds, alionyesha taswira nyingine kwa kukemea kitendo hicho na hata kuchukua hatua ya kuunda kamati kuchunguza.
Wakati Nape akichukua hatua hiyo, baadae siku hiyo hiyo Rais Magufuli alisikika akimtaka kiongozi anayetuhumiwa kufanya uvamizi huo achape kazi.
Siku moja baada ya Nape kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tukio hilo na kutanabaisha wazi kwamba anajua kutetea haki kuna gharama zake, hivyo yuko tayari kuzilipa, Rais Magufuli alitangaza kumwondoa katika nafasi yake ya uwaziri.
Watu wanaomfahamu Nape na ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa ukaribu, wameliambia MTANZANIA Jumapili kuwa mwanasiasa huyo alijua wazi anguko lake.
“Hebu nyinyi waandishi wa habari jiulizeni ni lini Nape alikuwa rafiki wa vyombo vya habari kama si sasa? Ni kwa sababu alijua. Huko nyuma hakuwa upande wenu, mnakumbuka kuhusu sheria ya huduma ya vyombo vya habari?” alihoji mbunge mmoja wa CCM ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
MUSWADA WA SHERIA YA HABARI
Nape alijipambanua vizuri kutetea msimamo wa Serikali wakati wa mchakato wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari ambao ulipitishwa na Bunge wakati kukiwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa habari.
Katika jitihada za kupitisha muswada huo, Nape alisimama kidete kuhakikisha mjadala wa kuupitisha hausogezwi mbele kama ilivyoombwa na wadau wa habari ambao walitaka kupata muda wa kuusoma ili waongeze maoni yao na kukosoa vipengele ambavyo vinaonekana ni kandamizi kwa tasnia.
Mwanzo wa uongozi katika wizara hiyo, Nape alinyooshewa kidole na wafuatiliaji wa mambo kuwa yeye ndiye aliyeongoza jitihada za Serikali za kuzuia televisheni nchini zisionyeshe vikao vya Bunge la 11 mubashara.
Wakati wa mjadala wa sakata hilo bungeni, Nape alitetea msimamo huo wa kulizuia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwamba lisionyeshe Bunge mubashara kwa kigezo cha kushindwa kuhimili gharama.
Katika ufafanuzi wake juu ya sakata hilo, Nape alisema msimamo wa kuifungia TBC isionyeshe Bunge mubashara umetolewa na Serikali, lakini akasema hajavizuia vyombo binafsi.
Kupitia maelezo hayo, alijitetea kwamba uamuzi wa kuzuia matangazo hayo ulifanywa na Bunge la Kumi wakati likipitisha uamuzi wa chombo hicho wa kuanzisha studio yake.
Siku chache baadaye, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa nchini Uingereza, alikazia hoja hiyo kwa kusema sababu ya kuzuia matangazo mubashara ya Bunge ni kutoa nafasi kwa wananchi kufanya kazi kwani walikuwa hawafanyi kazi.
Hata hivyo, tukio la sasa la Nape kupinga utendaji kazi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam limeonekana kufuta matukio yake ya nyuma ambayo baadhi ya watu, hasa upande wa upinzani, walikuwa wakiyachukulia kwa mtazamo hasi.
MKUTANO WAKE ULIVYOZUA HOFU
Upo mtazamo kuwa pengine kubadilika huko ghafla misimamo ya Nape kulichangia kwa kiasi kikubwa kuzuiwa kwa mkutano wake na waandishi wa habari saa chache baada ya Rais Magufuli kumwondoa katika wadhifa wake.
Hata hivyo, taarifa za kuzuiwa kwa mkutano huo hadi sasa ni za kukanganya, hasa baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Susan Kaganda kukanusha taarifa za Meneja wa Hoteli ya Protea aliyejitambulisha kwa jina moja la Suleiman kwamba alipata maelekezo kutoka kwake ya kutoruhusu kufanyika hotelini kwake.
Pamoja na hilo, tukio la kujitokeza mtu aliyetoa bastola hadharani kumtishia Nape ili arudi ndani ya gari, nalo lilijenga taswira hiyo hiyo.
0 comments:
Post a Comment