BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MAGUFULI AMTAKA RC MAKONDA KUZIBA PAMBA MASIKIONI ILI ACHAPE KAZI

RAIS John Magufuli amemkingia kifua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Paul Makonda kwa kumwambia achape kazi, huku akiwataka Watanzania kuacha udaku na kujielekeza katika masuala ya kimaendeleo.

Rais Magufuli ametoa tamko hilo baada ya kuwapo kwa taarifa katika mitandao ya kijamii ikimwomba Rais Magufuli kumtumbua Mkuu huyo wa Mkoa kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili.

Baadhi ya tuhuma hizo ni madai ya Mkuu huyo wa Mkoa kufoji vyeti vyake vya taaluma na kuvamia chombo cha habari akiwa na askari waliobeba bunduki.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema Watanzania wanatakiwa kujielekeza katika masuala ya maendeleo na siyo udaku kwani yanapoteza muda.

“Mnaangaika, mnaposti kwenye hivyo viposti vyenu mara hili mala hili mpaka watu wengine wanaingilia uhuru wangu wa kuniambia nifanye hivi," alisema Rais Magufuli. "Mimi ukiniambia nifanye hivi na ukiingilia ndiyo umenipoteza kabisa."
"Mimi huwa sipangiwi mambo, mimi ni Rais ninayejiamini.

“Mimi sipangiwi na mtu, sipangiwi na mtu maana hata siku ya kuchukua fomu nilipanga mwenyewe; hakuna mtu aliyenishauri. Niliamua mwenyewe kuwa ninafaa kuwa Rais.... nafikiri wamenielewa sasa Makonda chapa kazi.”

Alisema Watanzania wanatakiwa kuondokana na umasikini na kujenga uchumi wa viwanda pamoja na kusimamia miundombinu ya barabara na siyo kupiga umbea katika mitandao.

Rais Magufuli alisema udaku unaofanywa katika mitandao ya kijamii hautoi matatizo ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam wala shibe, hayasaidii kwenda mjini, hayasaidii kununua nguo, kununua mchicha, wala hayasaidii kupeleka watoto shuleni, wala kupata dawa hospitali.

“Ninafahamu wana Dar es Salaam mna uhuru wa kuzungumza chochote, lakini mjielekeze katika masuala ya maendeleo na ustawi wa Watanzania," alisema Rais Magufuli.

"Tujiwekeze katika mambo ya maendeleo, tutajenga nchi yetu vizuri.”

Rais Magufuli alisema yeye ndiye anayeamua nani anatakiwa kuwa wapi, akae wapi na kwama suala la kuandikwa katika mitandao siyo tija kwake kwa sababu hata yeye ameandikwa sana kwenye mitandao hivyo haoni sababu ya mkuu huyo wa mkoa kumtumbua.


Alisema muda huu viongozi wanapaswa kuwahudumia ambao wanashida ya huduma za kijamii kama vile maji, barabara, elimu, afya.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: