WAKATI madai ya kutekwa na kutishwa kuuawa kwa wabunge yakiibua mjadala mzito bungeni, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amedai anao ushahidi kuthibitisha kuwa Idara ya Usalama wa Taifa inahusika.
Akifafanua kuhusu madai yake wakati akichangia bungeni mjini Dodoma jana, Zitto alisema ni Usalama wa Taifa ndio wanaohusika katika kupotea kwa Ben Saanane, msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye hajulikani aliko kwa zaidi ya miezi minne sasa.
Alisisitiza kuwa anaweza kutoa ushahidi huo popote pale atakapohitajika.
Aidha, Zitto alidai kuwa anaweza pia kutoa ushahidi kuthibitisha kuwa mtu aliyemtolea bastola waziri wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, anatoka katika idara hiyo ya Usalama wa Taifa.
Zitto aliyasema hayo wakati Bunge lilipokuwa likijadili utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka huu wa fedha na makadirio ya bajeti ya ofisi hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.
CHANZO CHA TUHUMA
Kabla ya kuanza kwa mjadala huo na Zitto kutoa madai hayo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, aliomba mwongozo akihoji kitendo cha Naibu Spika kuitupa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge na kujadili kadhia ya kutekwa kwa watu nchini iliyotolewa juzi bungeni na wabunge wawili; Hussein Bashe wa Nzega Mjini (CCM) na Joseph Mbilinyi 'Sugu' wa Mbeya Mjini (Chadema).
Katika kujenga hoja yake, Msigwa alisema huenda Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alikataa kuruhusu hoja hiyo ijadiliwe na kupatiwa ufumbuzi na Bunge kwa kuwa yeye ana walinzi, tofauti na hali ilivyo kwa wabunge na wananchi wa kawaida ambao alidaia kuwa hivi sasa wanaishi kwa hofu.
Msigwa ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, alisema Jeshi la Polisi ndiyo linaloruhusiwa kukamata watu kwa mujibu wa sheria huku akikumbusha kuhusu kauli ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kwamba "aliyemtishia kwa bastola Nape, si polisi".
"Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wabunge ni wawakilishi wa wananchi na katika kipindi hiki wabunge tuko katika taharuki kubwa ya watu kutekwa na watu ambao hawajapewa mamlaka hayo … na kwa siku mbili hizi wabunge wameomba kujadili suala hili lakini mwongozo huo umekataliwa," alisema.
"Naibu Spika ana walinzi, Watanzania wengi huko mitaani hakuna walinzi… chombo pekee kinachoruhusiwa kukamata ni Jeshi la polisi.
Tumeona watu, hata Wizara ya Mambo ya Ndani imesema siyo polisi. Watu waliokwenda kuteka Cluods Tv siyo polisi. Halafu chombo kikubwa kama Bunge hatujafanya kitu,” alisema Msigwa na kuongeza:
"Waziri wa Katiba na Sheria amekaa kimya, sasa hili ni Bunge gani linakaa kimya? Tunafanya nini hapa? Roma (Mkatoliki) kisaikolojia bado ametekwa… sasa mnampeleka pale (kuzungumza na waandishi wa habari). Waziri wa Mambo ya Ndani kimya, wabunge kimya. Tunaomba miongozo mnatuzuiya."
Kabla ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kutoa mwongozo wa Kiti kuhusu suala hilo, Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisimama na kuwataka wabunge wanaozungumzia mambo ya kutekwa na kupotea kitatanishi kwa watu, wawasilishe ushahidi wao ili ufanyiwe kazi.
"Wanaozungumzia mambo haya, kama wana ushahidi, wafanye utaratibu ili tuweze kulimaliza jambo hili vizuri na kuzingatia mfumo wa taratibu na sheria. Sisi wabunge wote tupate nafasi nzuri ya kupata uthibitisho wa mambo haya na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa kufuata taratibu zilizopo," alisema Jenista kabla ya kuongeza: "Kwetu sisi wabunge ambao tumekuwa tukilieleza jambo hili, tuchukue nafasi yetu kama wawakilishi wa wananchi kulisaidia taifa kuleta uthibitisho mezani kwako."
Baada ya maelezo hayo, Zungu alisema Kiti cha Spika kinalichukua suala hilo na kitalitolea uamuzi baadaye.
UFAFANUZI WA ZITTO
Alipopewa nafasi ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Zitto alisema maelezo yaliyotolewa na Waziri Mhagama hayaendani na kupokewa na Zungu, hayaendani na Kanuni za Kudumu za Bunge.
Mbunge huyo alisema suala la kupotea kwa Saanane linapaswa kuchukuliwa uzito wa juu na halipaswi kuchukuliwa kisiasa kwa kuwa taarifa alizonazo zinaonyesha simu ya mwanachama huyo wa Chadema ilipatikana kwa mara ya mwisho Novemba 15, mwaka jana akiwa katika maeneo matatu tofauti.
"Leo (jana) asubuhi, kuna mwongozo umetolewa na 'Chief whip' (mnadhimu) wa serikali ametoa maelezo ambayo wewe umeyakubali… hayaendani na kanuni za Bunge," Zitto alisema.
"Mtanzania aliyepotea, Ben Saanane ni suala ambalo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa juu, siyo suala linalopaswa kuchukuliwa kisiasa. Si suala linalopaswa wabunge wabebe uthibitisho walete mezani.
"Kwa sababu taarifa zilizopo sasa na ziko Jeshi la Polisi, zinaonyesha kwamba Novemba 15, Ben Saanane kwenye mawasiliano yake ya simu kuanzia asubuhi alikuwa maeneo ya Tabata, akaenda maeneo ya Mikocheni, akatumia muda mwingi sana maeneo ya Mwenge, akapelekwa ama akaenda Mburahati saa nne usiku ya mwezi Novemba.
"Simu yake ikapoteza mawasiliano. Tangu hapo hajawahi kuwa 'traced' tena. Na haya maelezo yako polisi na ukifuatilia Jeshi la Polisi, wanakwambia tumefikia mwisho.
"Lakini mwelekeo wetu unaonyesha kuwa waliomchukua Ben Saanane ni Usalama wa Taifa na Mwenyekiti (Zungu), wewe 'ume-save' (umefanya kazi) katika Kamati ya Usalama na Mambo ya Nje, unafahamu Sheria ya Usalama wa Taifa kifungu namba tano kifungu kidogo cha pili kinapiga marufuku Usalama wa Taifa 'ku-enforce laws'.
"Usalama wa Taifa hawana mamlaka ya kukamata hata wakimuona mwizi, sheria inakataa kwa sababu ya kuepuka haya mambo ambayo tunayo na sasa hivi kumekuwa na matatizo hatuyapatii ufumbuzi.
Ninyi mnafahamu aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, (Absaloum) Kibanda alikamatwa, akateswa, akaumizwa na leo jicho lake moja halioni. Lakini hadi leo hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa kulingana na tukio kama hilo.
"Katika mazingira kama haya, hatuna namna na katika historia ninyi wenyewe ni mashahidi ambao mmekaa bungeni muda mrefu, haijatokea Bunge hili kujadili Usalama wa Taifa, kwa mara ya kwanza tunaivuka hiyo 'taboo' (miiko), watu wamechoka."
Zitto pia alitumia nafasi hiyo kulitaarifu Bunge kuwa atatumia Kanuni ya 120 ya Bunge kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili kuundwe kamati teule ya kufanya uchunguzi wa matukio yote ya kupotea kwa watu, mauaji na matukio yote yanayojenga taswira hasi dhidi ya Usalama wa Taifa.
Alisema anazikumbusha kamati za kudumu za Bunge kuwa kuna masuala ambayo kamati hazipaswi kupelekewa na Spika bali zinapaswa kufanya zenyewe ndiyo maana Bunge lina utaratibu wa taarifa maalumu kutoka kwa kamati.
Hata hivyo, wakati Zitto akiendelea kuchangia mjadala huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisimama na kumpa taarifa mbunge huyo kwamba Kanuni za Bunge zinazuia masuala ya Idara ya Usalama wa Taifa kuongelewa bungeni.
"Nafahamu kuwa Zitto anafahamu kanuni vizuri sana…ana uwezo wa mkubwa wa kusoma. Anafahamu kuwa hili analolijadili, haliruhusiwi kujadiliwa humu na kwamba anazungumzia suala la Usalama wa Taifa ambalo haliruhusiwi kujadiliwa na Bunge," alisema.
"Lakini Zitto anautuhumu Usalama wa Taifa kwamba umeshiriki katika vitendo vya utekaji. Je, anaweza kulithibitishia Bunge hili? Kwa sababu anafahamu ni makosa kufanya hivyo, 'it is taboo', lakini anasema imebidi tuvuke mipaka na sasa anauingiza Usalama wa Taifa katika kuutuhumu kwa jambo ambalo sina uhakika kama ana ushahidi wa kutosha.
Kwa hiyo, nimuombe tu Zitto alete ushahidi wa kulithibitishia Bunge hili kwamba Usalama wa Taifa ndiyo waliomshikilia Ben Saanane."
BASHE ATUHUMU PIA USALAMA WA TAIFA
Wakati Simbachawene akimbana Zitto awasilishe ushahidi kuhusu suala hilo, Mbunge wa Jimbo la Nzega, Hussein Bashe (CCM), alisimama na kuomba kutoa taarifa na kuruhusiwa na Zungu ambaye pia alimshukuru Simbachawene na kumwambia kuwa ameshaeleweka.
Katika taarifa yake, Bashe ambaye alikuwa anazungumza huku anatetemeka kwa kile kilichoonekana kuumizwa na taarifa aliyokuwa akiitoa, alisema: "Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Simbachawene, waziri kwamba mimi Hussein Mohamed Bashe, nilikamatwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa."
"Acheni unafiki, acheni unafiki, 'we are all Tanzanians (sisi sote ni Watanzania). 'In this' (katika hili), hamjawahi kunyanyaswa ninyi, acheni, mimi ni mwanaCCM, 'I don’t care' (sijali). Mkitaka nifukuzeni ubunge. Mimi nimekamatwa na usalama, nimeonewa 'in this country' (katika nchi hii), acheni unafiki.
Tunavumilia mambo mengi, acheni… hamjawahi kuwa 'humiliated' (kunyanyaswa),” alisema zaidi Bashe, lakini akakatishwa na Zungu.
Baada ya taarifa hiyo, Zitto aliendelea kuchangia mjadala huo, safari hii akimkumbusha Waziri Simbachawene kuwa waliokwenda kuvamia kituo cha televisheni ya Clouds jijini Dar es Salaam siyo polisi huku akidai kuwa anaweza kuthibitisha walikotoka.
Ndipo pia Zitto akasema hata aliyekwenda kumtolea bastola Mbunge wa Jimbo la Mtama (CCM), Nape, alitoka Usalama wa Taifa.
"Aliyekwenda kumtolea bastola Mbunge wa Mtama ni ofisa usalama na ninaweza kuthibitisha. Kama Bunge linaweza kuunda chombo cha kutaka nikathibitishe hayo, niko tayari kuthibitisha," alisema Zitto.
RIDHIWANI ATAKA KAULI YA MWIGULU
Awali, akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), aliishauri serikali kutatua changamoto iliyoibuka ya matukio ya kupotea na kutekwa kwa watu kwa kutoa tamko, hasa kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.
"Kumekuwa na malalamiko mengi sana. Tumeshuhudia malalamiko mengine ambayo yanahitaji majawabu kama siyo majibu ya haraka ili kuondoa hizi sintofahamu walizonazo wananchi," alisema.
"Nikuombe sana… hakuna sababu ya mtu kama Waziri Mwigulu (Nchemba) kuendelea kukaa kimya wakati wananchi wanalalamika juu ya hali ya kiusalama katika maisha yao. Mimi binafsi niishauri serikali yangu, unapojibu jambo lolote lile, unawatoa wananchi wasiwasi na wanapata amani," alisema.
NKAMIA AMSHUKIA DK. MWAKYEMBE
Mbunge wa Nchemba, Juma Nkamia (CCM), alikosoa kitendo cha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kushiriki katika mkutano wa msanii Ibrahim Mussa 'Roma Mkatoliki' ambaye alikuwa akielezea kuhusu mkasa wa kutekwa kwake na watu wasiojulikana.
Nkamia ambaye alikuwa Naibu Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, alisema kitendo cha Dk. Mwakyembe kushiriki mkutano huo kimetoa taswira kwamba huenda serikali imehusika na kutekwa kwa msanii huyo na wenzake watatu.
"Serikali lazima iwe 'active', lakini siyo kuwa 'active' kwa kukosea. Nitoe mfano, samahani sana, jana (juzi) nilikuwa naangalia mkutano wa waandishi wa habari wa yule bwana anaitwa Roma Mkatoliki, hivi Waziri wa Habari alienda kufanya nini?" Nkamia alihoji.
"Unajua wakati mwingine unaweza kuambiwa ukweli ukachukia, lakini ni afadhali uambiwe ukweli. Waziri wa Habari alikwenda kwenye mkutano wa Roma Mkatolini, anampisha na kiti. Anayeongoza mkutano ni Zamaradi Kawawa, ofisa wa serikali.
"Hivi kesho mtu akikwambia wewe ndiye ulimteka Roma, utakataaje? Ni vizuri uchukue ukweli hata kama unauma, lakini 'you take it' (unauchukua), 'at the end of the day' (mwisho wa siku) unaweza ukafanya marekebisho, wakati mwingine mnamgombanisha Mheshimiwa Rais na wananchi bila sababu ya msingi… mimi sikuona 'logic' kabisa. Mimi siyo mwanasheria, nimesoma uandishi wa habari na uhusiano wa kimataifa, lakini 'is not applicable' (haifai).
"Kwa hiyo, serikali wakati mwingine mnaingia kwenye mtego wenyewe bila kujua, hebu liangalieni hili. Ilitokea wapi mpaka waziri akakosa kiti, halafu huyu mtu binafsi anafanya 'press conference' (mkutano na waandishi wa habari), wewe unaenda kufanya nini?
KIKAO WABUNGE CCM
Wakati wabunge wakicharuka kuibana serikali kuhusiana na matukio ya utekaji, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walitarajiwa kukutana jana usiku katika kile kilichoonekana kuwa ni kukumbushana juu ya mambo mbalimbali.
Tangazo lililosomwa na Zungu kabla ya kuahirishwa kikao cha mchana, ilielezwa kuwa wabunge hao walitakiwa kukutana saa 2:00 usiku.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment