BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKAZI WA DAR ES SALAAM NA MIKOANI KUKOSA USAFIRI JUMANN BAADA YA CHAMA CHA WAMILIKI WA MABASI KUITISHA MGOMO

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (Taboa), kwa kushirikiana na Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Dar es Salaam, (UWADAR), wametangaza kuanza mgomo wa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kuanzia keshokutwa.

Mgomo huo unatarajia kuhusisha mabasi yote ya abiria yaendayo mikoani na nchi jirani na pia yale yanayosafirisha abiria jijini Dar es Salam, maarufu kama daladala, kwa lengo la kupinga mabadiliko ya Sheria ambayo Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeyafanya.

Wakati kukiwa na tishio hilo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano, aliiambia Nipashe jana kuwa wamiliki hao hawapaswi kugoma kwa sababu kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi zinazowataka kutoa notisi ya siku 30 kabla ya kufanyika kwa mgomo.

AZIMIO LA MGOMO
Jana, wamiliki wa mabasi ya mikoani na wenzao wa daladala, walikutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa dharura kujadili muswada wa sheria wanaohofia kuwa ukipitishwa, utawakandamiza kwa kiasi kikubwa.

Muswada wa sheria unaolalamikiwa na wamiliki hao ni ule uliotungwa na (Sumatra), ambao unatarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki ijayo kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya mwisho na kupitishwa kuwa sheria.

Kwenye Muswada ambao wamiliki hao walisema jana kuwa hawakushirikishwa kwa hatua yoyote, unasema kuwa iwapo dereva wa basi atafanya kosa, mmiliki wa basi naye atajumuishwa kwenye kesi hiyo.

Akitangaza maazimio ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alisema mwisho wa kukata tiketi za kwenda mikoani na nchi jirani itakuwa kesho (Jumatatu) na aliwaomba radhi abiria kwa usumbufu watakaoupata.

Alisema wamiliki wa daladala katika mkoa wa Dar es salaam, nao wameshiriki mkutano huo na wameazimia kwa kauli moja kusimamisha huduma ya kusafirisha abiria kuanzia siku hiyo ya Jumanne.

“Abiria watuwie radhi, lakini watambue kuwa athari watakazopata zinatokana na sheria kandamizi inayotaka kutungwa na Sumatra kuwakandamiza wenye mabasi na daladala… sheria hii ikipita hakuna mmiliki wa basi atakayeendelea na biashara hii hivyo kwa sauti moja tumeamua kugoma ili kupaza sauti zetu,” alisema Mrutu.

Mrutu aliwaomba wabunge wasikubali kupitisha muswada huo kandamizi ambao alisema iwapo utapitishwa na kuwa sheria utayumbisha biashara ya usafirishaji.

Pia aliiomba serikali kutoa muda zaidi wa majadiliano na wamiliki wa mabasi ili kuondoa baadhi ya vifungu vya muswada huo ambavyo wanaamini kuwa ni kandamizi kwa watu wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria.

“Baada ya majadiliano ya siku nzima, wajumbe wa mkutano mkuu waliokutana kwa dharura waliamua kwa sauti moja kusitisha huduma hiyo ili wakae mezani kujadiliana.

Sheria hizi wanazotaka kutunga kama kutukomoa zitawaondoa watu kwenye hii biashara na zitaporomosha uchumi,” alisema Mrutu.

Sheria hiyo mpya itaipa mamlaka serikali kutaifisha gari linapofanya makosa, adhabu ambayo Mrutu alisema ni kubwa kulinganisha na thamani ya gari na makosa ambayo yanatajwa katika muswada huo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam, (UWADAR), Kismat Jaffar, aliunga mkono mgomo huo akisema kuwa daladala zote za Dar es Salaam hazitatoa huduma yoyote ya usafiri hadi maelekezo mengine yatakapotolewa.

“Msimamo wa Taboa ndiyo msimamo wa UWADAR, na sisi kuanzia Jumanne tutasitisha huduma za usafirishaji abiria hadi hapo matatizo yaliyojadiliwa hapa yatakapopatiwa ufumbuzi, uonevu wanaofanyiwa wenye mabasi ya mikoani ni uonevu huo huo wanaofanyiwa daladala,” alisema.

UFAFANUZI WA SUMATRA
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano, alisema hana taarifa ya jambo hilo, ingawa alikiri kuwa anazo taarifa za kufanyika kwa mkutano huo wa Taboa na UWADAR

Alisema kama kuna mgomo wowote, wamiliki hao wanatakiwa kutoa notisi ya siku 30 na kwamba, ikiwa watagoma kesho kutwa wanakiuka sheria za nchi na adhabu ya kosa hilo ni pamoja na kuwanyang'anya leseni wamiliki wa mabasi hayo. 


Alisema wamiliki hao walishirikishwa katika kikao kilichofanyika mwezi uliopita na kwamba, waliwapa siku 14 kuendelea kutoa maoni yao ili kuboresha kanuni.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: