ZITTO, CHADEMA WAVURUGANA UPYA
IKIWA ni takribani miaka mitano tangu Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, avurugane na Chadema ambacho kilikuwa chama chake, sasa hali hiyo inaonekana kurudi tena kupitia uchaguzi wa ubunge wa Afrika Mashariki (EALA).
Tofauti na awali ambapo alikosana na Chadema na kufukuzwa uanachama kutokana na kile kilichodaiwa ni kuandaa waraka wa mabadiliko ya 2013, sasa hivi ubunge wa EALA unaonekana kumvuruga tena mwanasiasa huyo na Chadema, baada ya kuandika barua kwa Spika wa Bunge akitaka utaratibu uliotangazwa wa namna ya kupata wabunge ubadilishwe.
Utaratibu huo mpya uliotangazwa, unatoa nafasi kwa wabunge wa EALA kwa mwaka 2017 kulingana na idadi ya wabunge wa kila chama kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Mwongozo huo, kutokana na idadi ya wabunge wa vyama kwa kila chama, CCM imepata nafasi za wabunge sita kwenda EALA, Chadema mbili, CUF moja, huku ACT Wazalendo pamoja na NCCR Mageuzi, vikiwa havina nafasi hata moja kwenye Bunge hilo la Afrika Mashariki, kutokana na kuwa na mbunge mmoja kila kimoja, hivyo kutokidhi vigezo.
Kutokana na hali hiyo, Zitto ameliandikia Bunge barua kutaka Kamati ya Kanuni za Bunge ikutane kujadili uchaguzi wa wajumbe wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki.
Barua hiyo, ambayo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanadai inalenga kutaka utaratibu wa awali ubadilishwe ili chama cha Zitto (ACT Wazalendo), kimwingize mwanachama wake, Profesa Kitila Mkumbo kugombea ubunge huo, inasema mwongozo uliotolewa na Bunge umekwenda kinyume cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wanasema endapo hoja ya Zitto ikikubaliwa, ni rahisi zaidi wagombea wa Chadema wakakosa nafasi hizo na badala yake nafasi za upinzani kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki zikachukuliwa na wagombea wa ACT na wale wa CUF.
Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na wabunge wengi kwenye Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuwa ni wa CCM, hivyo ni rahisi kuweka msimamo wa kuwapigia kura wale wagombea wa ACT Wazalendo na wale wa CUF, badala ya wale wa Chadema kutokana na hali ya kisiasa iliyopo nchini kwa sasa.
Barua ya Zitto ya Machi 28 iliyoandikwa kutokana na Tangazo la Bunge kwenye gazeti namba 11 la Machi 17, lililotangaza uchaguzi huo na masharti yake, ilisema mwongozo wa uchaguzi huo unavunja kanuni mbalimbali na kwamba kitakachofanyika sasa kitakuwa ni uteuzi na siyo uchaguzi.
Alisema pia mwongozo huo, mbali na kuvunja Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unataka suala la jinsi lizingatiwe kwenye wabunge wanaokwenda kuiwakilisha nchi katika Bunge hilo.
Baada ya Zitto kuandika malalamiko hayo, Mwanasheria wa Chadema, John Malya, naye aliyajibu akirejea hukumu mbili za kesi ya Anthon Komu (kwenye Divisheni ya Mwanzo na Divisheni ya Rufani).
Malya aliandika kwamba, mwongozo wa Ofisi ya Spika wa Bunge wa kugawa idadi ya viti kwa vyama ni sahihi, kwa sababu Divisheni zote mbili za Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ziliamua.
Katika sehemu ya barua yake, alisema: “Mwenye kupaswa kubeba mzigo wa makundi ya Zanzibar, Bara na Wanawake (ukiachilia mbali kundi la vyama vya upinzani) ni chama chenye wabunge wengi (CCM)”.
Hoja hiyo ya Malya inachambuliwa na Ado Shaibu, ambaye aliandika ujumbe unaogusa hoja za kisheria ambazo alitumia Malya kukosoa malalamiko ya Zitto.
Shaibu alisema ni kosa kutumia kesi ya Antony Komu ambayo iliamuliwa na Divisheni ya Mwanzo ya Mahakama ya Afrika Mashariki, lakini baadaye Divisheni ya Rufani ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ikatengua hukumu hiyo kwa hoja ya kwamba Divisheni ya Mwanzo ya Mahakama haikuwa na mamlaka ya kuamua suala husika.
MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na Katibu wa Bunge, Dk. Kashilila, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wake juu ya malalamiko ya Zitto kuhusu kukiukwa kwa Ibara ya 50(1) ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki juu ya mwongozo wa uchaguzi wa wabunge wa EALA.
Katika maelezo yake, Dk. Kashililah alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo sasa, kwa sababu Zitto aliwaomba walitafakari jambo hilo.
“Aliomba tulitafakari suala hilo, tutalijibu baadaye tukishamaliza kutafakari. Tangazo nililolitoa kwenye gazeti la serikali baada ya majina kutangazwa jana (juzi), vyama vinaweza vikaleta malalamiko yao, maoni yao na mapendekezo yao na sisi tunaweza kuyatolea majibu, ndiyo maana hujasikia tumetangaza wagombea.
“Ingekuwa tumeshatangaza wagombea mngeweza kutuuliza, lakini mpaka sasa hatujatoa tangazo kama vyama vingine vimeleta majina ya walioshinda na waliokata rufaa wameshindwa. Kwa msingi huo, nafikiri kwamba bado ni mapema sana kuanza kuzungumzia hilo,” alisema Dk. Kashililah.
0 comments:
Post a Comment