UHURU WA VYOMBO VYA HABARI BILA MASLAHI BORA KWA WAANDISHI WA HABARI INAWEZEKANA?
Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari ndo imepita, japokuwa siku hii naiona kama ni maadhimidhi ya siku ya Wamiliki wa Vyombo vya habari wanaotaka vyombo vyao viwe na Uhuru wa kuandika habari bila 'mipaka'.
Kwa kuwa dhana nzima ya maadhimisho ilitwishwa kwa waandishi, tumeshuhudia Waandishi wa habari kuwa ndio waliobeba msalaba wa kuwasilisha madai na mada mbalimbali kuhusu kudai uhuru huo wa vyombo vya habari wakati wa maadhimisho ya siku hiyo jana.
Sijui ni kwa sababu sikuona na kusikia tukio hilo Live kutoka jijini Mwanza, katika mada na hotuba zote ikiwemo ya Waziri mwenye dhamana ya habari, sikusikia kikitajwa kwa dhati na uzito wake kilio cha umuhimu wa kuwalazimisha wamiliki wa vyombo vya habari kuboresha maslahi ya waandishi wa habari ikiwemo mazingira bora ya kazi, mikataba ya kazi na kulipwa mishahara kwa wakati!
Bila shaka waandishi wa habari mnajua, ukiacha vyombo vya habari vya serikali, walimiki karibu wote wa vyombo binafsi kiukweli hawazingatii kikamilifu maslahi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wengine katika vyombo vyao.
Imeshakuwa ni kama jambo la kawaida kuwakuta waandishi wa habari wengi tu, wapo kazini kusaka habari lakini hawajalipwa mishahara kwa uhakika kwa miezi au miaka kadhaa, na hata akiamua kuacha kazi hapati pensheni zake kwa kuwa mwajiri hajapeleka makato ya pensheni hizo kwa miaka kedekede!
Wamiliki hawa hawatoi maslahi bora kwa waandishi na watumishi wao wengine kutokana na sababu mbalimbali, lakini binafsi nahisi ni kutosimamia vyema vyombo hivyo hasa upande wa menejimeti kwa kuwa vyombo hivi kama taasisi yoyote vinapaswa kuwa na menejimenti imara, zenye viongozi wenye uthubutu na weledi wa hali ya juu katika kuratibu na kusimamia wafanyakazi kimaslahi na kiutendaji, na pia wenye malengo na mikakati thabiti ya kibiashara badala ya kuwa na viongozi kina boraliende!
Hivyo basi hali hii ya maslahi duni inawafanya waandishi wa habari wa vyombo vingi hapa Tanzania ambao wengi wanao weledi wa kutosha kutaaluma, kutoweza kuutumia vizuri Uhuru wa kuandika habari hata uhuru huo ukiwepo kwa zaidi ya asilimia mia moja.
Hii ni kwa kuwa mazingira hayo ya kutopatiwa maslahi huwageuza bila hiari waandishi hao kuwa mateka wa watu wa mitaani wanaowalipa fedha ili kuandikiwa habari zinazolinda maslahi yao hasa wanasiasa pengine hata wsuza dawa za kulevya!
Katika mazingira hayo usitarajie kuona habari za kijamii na za kutetea na kulinda maslahi ya wanyonge na za kutetea na kulinda utaifa zikiripotiwa kwa kina na mwandishi wa kada hiyo.
Na kwa kweli katika mazingira ya njaa hakuna mwandishi kutoka vyombo visivyotoa maslahi ambaye anaweza kukwepa au kunusurika kutekwa. Maana adui wa kwanza duniani ni njaa, hata mwanajeshi shupavu aliyejificha handakini akitwangwa na njaa sawasawa anatoka nje.
Kwa hiyo, ikiwa waandishi wanataka kuwa salama na kuendana na weledi katika kazi yao hii adhimu, kwa kuwa jana walijifunga kibwebwe katika kufanikisha maadhimisho ya Siku ya uhuru wa vyombo vya habari, Sasa nashauri bila kulazimisha Wajipange kwa umoja wao watenge pia SIKU YA MASLAHI YA WAANDISHI WA HABARI.
Maana katika hali ya mazingira ya hali ya sasa, nionavyo mimi hata uhuru wa vyombo vya habari ungekuwa mkubwa kiasi gani mwandishi asiyepewa maslahi bora na Chombo husika bado uhuru huo hautakuwa na tija inayotarajiwa kwake.
Wakatabahu
BN 0789498008
0 comments:
Post a Comment