CHANZO CHA WATOTO WA KIKE KUPATA MIMBA ZA UTOTONI CHATAJWA
SERIKALI, imevitaja vyanzo vya ndoa na mimba za utotoni, kuwa ni umaskini na mila zilizopitwa na wakati.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18.
“Mimba na ndoa za utotoni bado ni kikwazo katika kufikia maendeleo ya nchi yetu. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, kiwango cha ndoa za utotoni nchini ni cha asilimia 37.
“Mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinyanga yenye asilimia 59, Tabora yenye asilimia 58, Mara yenye asilimia 34, Dodoma yenye asilimia 51 na Lindi yenye asilimia 48.
“Kwa hiyo, ili kukabiliana na vitendo hivyo, Serikali na wadau mbalimbali, wameendesha program na kampeni mbalimbali za kupinga ndoa hizo ili kupunguza tatizo hilo.
“Kwa upande wa Mkoa wa Shinyanga, kampeni hiyo iliwafikia wananchi zaidi ya 800 na kuokoa watoto wa kike 102 waliokuwa katika hatua za kuozeshwa,”alisema Mwalimu.
Kuhusu huduma za kibingwa, alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji wa utoaji wa huduma hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, aliishanga Serikali kushindwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya nchini.
0 comments:
Post a Comment