
Na mwandishi wetu, Morogoro.
Mji wa Ifaraka ulikumbwa na taharuki, hofu na wasiwasi kufuatia uwanja wa siasa kugeuzwa kuwa uwanja wa vita kwa muda wa saa 22 baada ya watu sita kupigwa na kujeruhiwa vibaya akiwemo askari polisi aliyepigwa jiwe katika paji la uso huku kundi la vijana la Changausile likitajwa.
Matukio ya kujeruhiwa kwa watu hao kunadaiwa kutekelezwa na kundi hilo wakati wa uchaguzi mdogo wa serikali ya kitongoji cha Mbasa Mlimani na serikali ya kijiji cha Kikwawila wilaya ya Kilombero mkoa wa Morogoro.
Kundi hilo limetajwa kuanzisha vurugu usiku wa April 22 mwaka huu na siku yenyewe ya uchaguzi huku likidaiwa kuwalenga watu waliokuwa wanakiunga mkono Chadema katika uchaguzi huo.
Wakati vitendo vya uvunjifu wa amani ukitokea katika uchaguzi huo, kundi hilo hilo lilimvamia mwandishi wa gazeti la Mwananchi (Juma Mtanda) na kumweka chini ya ulinzi mkali kisha kumpora vifaa vyake vya kazi katika eneo la Malale City alipoenda kwa ajili ya kupata chakula cha mchana.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi huyo ambaye alizungumza na watu mbalimbali kujua chanzo na visa vya kupigwa, kujeruhiwa na kuporwa vifaa vya kazi, imebaini ukweli wake.
Mwenyekiti mteule wa serikali ya kitongoji cha Mlimani kijiji cha Mbasa Chadema, Majuto Mnasi alieleza kwa kusema kuwa jumla ya watu sita wamejeruhiwa na mmoja kati yao ni askari polisi, WP Huruma Mkisi wa kituo cha polisi Ifakara.
Mnasi alieleza kuwa WP Huruma alipigwa jiwe kichwani eneo la paji la uso na kukimbizwa hospitalini alikoshonwa juzi tano wakati akitekeleza majukumu ya kulinda amani eneo la kituo cha kupigia kura na mmoja wa vijana aliyedai kutaka kupora sanduku la kura.
“Ni kundi la vijana la Changausile ndilo lililotekeleza vitendo vya kiuhalifu kwa kumpiga jiwe askari WP Huruma kisha kudhuru watu wengine kwa kuwapiga kwa silaha za jadi zikiwemo mapanga, mawe na fimbo usiku wa uchaguzi na siku yenyewe huku kundi hilo likiwazuia watu kwenda kupiga kura kituoni.”alieleza Mnasi.
Mnasi alidai kuwa kundi hilo la Changausile ni kundi lililoratibiwa na kufadhiliwa na CCM likiwa na lengo la kuwadhibiti watu wote wanaounga mkono Chadema kwa namna moja ama nyingine ili Chadema isiweze kushinda kwenye uchaguzi huo wa Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbasa Mlimani.
“Dalili za CCM kushindwa katika uchaguzi waliziona mapema na njia waliona inafaa kutudhoofisha sisi kwa kutumia kundi hilo la Changausile kupiga watu wanaokiunga mkono Chadema.”alieleza Mnasi.
Mnasi aliwataja baadhi ya watu waliojeruhiwa na kupata (PF3) kisha kwenda kutibiwa baada ya kujeruhiwa kuwa ni Selemani Kandama, Nasibu Kilawilo na Mkoka Selemani.

CHANZO CHA KUPIGWA KWA ASKARI POLISI.
WP Huruma Mkisi alipigwa jiwe kichwani lililorushwa na mmoja wa kijana wa kundi hilo na kutua katika paji lake la uso kisha kudondoka chini wakati akiwa na wasimamizi wa uchaguzi huo, mawakala, wagombe na askari wawili.
“Tulikuwa katika boma la nyumba ambayo haijaisha kujengwa na chumba kimoja ndicho kilichotumika kuhesabia kura na wakati tunasubiria kutangazwa matokeo, vijana wa lile kundi lilisogea karibu zaidi wakitaka kuanzisha vurugu na kurusha jiwe lililotua kichwani kwa askari.”alieleza Mnasi.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa moja kasoro jioni na baada ya askari huyo kupigwa jiwe, askari walifyatua mabomu ya machozi kutawanya kundi hilo lililodaiwa kutaka kupora sanduku la kura.alieleza Mnasi.
Mnasi aliendelea kueleza kuwa muda mfupi baada ya askari kujeruhiwa, mkuu wa upelelezi wilaya ya Kilombero, Prosper Ngowi aliwasili eneo hilo na kutoa shinikizo la kutangazwa kwa matokeo vinginevyo angeondoa askari kutokana na kucheleweshwa kutangazwa matokeo.
Hatua ya mkuu huyo wa upelelezi ilizaa matunda na Msimamizi Msaidizi wa chaguzi kituo cha Mbasa Mlimani, Asmina Lewis kutangaza matokea huku Chadema kupitia, Majuto Mnasi akiibuka mshindi baada ya kupata kura 346 huku mgombea wa CCM, Mohamed Isihaka akipata kura 321 na Ezekiel Mbata wa NCCR-Mageuzi akiambulia kura nne.
“Ucheleweshwaji wa kutangaza matokeo ulichangiwa na msimamizi wa uchaguzi na ndio sababu ya askari kuingia kwenye mkumbo wa kupigwa kwani vijana wale walikuwa na kazi maalum waliopewa na CCM.”alieleza Mnasi.
CCM iliweza kuibuka kidedea kwa kushinda katika uchaguzi wa serikali ya kijiji cha Kikwawila kata ya Kibaoni huku Chadema ikishinda katika uchaguzi wa serikali ya kitongoji cha Mbasa Mlimani.
Shabaan Salahange alipata kura 557 na kuiwezesha CCM kushinda huku Odrick Matimbwa wa Chadema akipata kura 528 na Bakari Mkungundile wa NCCR-Mageuzi aliambulia kura mbili.
Chadema ilitangazwa mshindi katika uchaguzi wa kitongoji cha Mbasa Mlimani kupitia, Majuto Mnasi aliyepata kura 346 na kumshinda mpinzani wa CCM, Mohamed Isihaka kwa kupata kura 321 na NCCR-Mageuzi ikipata kura nne kupitia kwa Ezekiele Iginas.
Mkazi wa Mbasa Mlimbani mtaa wa Maendeleo, Winfrida Mbembe (24) alieleza kuwa amepetwa na wasiwasi kwa askari kujeruhiwa akilitumikia taifa.
“Hakuna mtanzania asiyefahamu kazi nguzu wanazofanya askari wetu tena usiku na mchana alafu leo hii mtu anachukua jukumu la kumjeruhiwa tena akiwa kazini jambo hili sio la kufumbia macho na mamlaka husika zinapaswa kuwasaka ili sheria ifuate mkondo wake.”alieleza Winfrida.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilombero, Abdallah Kambangwa alieleza kusikitishwa kwake na matukio yaliyojitokeza kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji cha Mbasa Mlimani na mwenyekiti wa kijiji cha Kikwawila uliofanyika April 23 mwaka huu.
Kambangwa alieleza kuwa kunawezekana kumefanyika jambo kwa nembo ya CCM na CCM haina desturi ya kufanya vurugu za namna yoyote.
“Tatizo limetokea na linapaswa kutatuliwe ili siku nyingine yasijitokeze haya mambo yaliyojitokeza lakini nalaani kwa nguvu zangu zote kwa niaba ya chama vitendo vilivyojitokeza ikiwemo watu kujeruhiwa na mwandishi kupokonywa vitendea kazi ikiwemo kamera na simu aina ya ipad.”alieleza Kambangwa.
Tabia za uwepo wa makundi yenye kujihusisha na uhalifu sio jambo linaloweza kukubaliwa na CCM lakini chama hakijaadhimia kuwa na kundi lolote katika uchaguzi huu.alieleza Kambangwa.
“Nafanya uchunguzi kwa matukio yote yaliyofanyika katika uchaguzi huu na kusababisha askari kujeruhiwa, mwandishi kupokonywa vifaa vyake vya kazi kwa kundi Changausile likitajwa na nitatolea ufafanuzi na kuchukua hatua.”alieleza Kambangwa.
Kambanga alieleza kuwa sio dhambi mwandishi wa habari kuwa karibu na viongozi wa vyama vya siasa sehemu yoyote ile…kwani kazi ya mwandishi habari ni kuunganisha habari ndogo ndogo ili kupata habari kamili na suala la hisia na dhana linatoka wapi?.alihoji.
Kaimu Katibu wa CCM kata ya Mbasa, Aziz Nyama alieleza kuwa Chadema wamekuwa wakitengeneza matukio ya kukichafua chama cha mapinduzi ili kichukiwe na wananchi.
“Chadema wametengeneza propaganda za kisiasa kwa kuwahadaa wapigakura kwa matukio ya kutengenza ili wananchi wasitupatie ridhaa ya kuongoza kitongoji cha Mlimani.”alisema Nyama.
MBUNGE ACHUKIZWA NA VITENDO VYA KUJERUHIWA ASKARI NA KUPOKONYWA VIFAA MWANDISHI WA HABARI.
Mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali akiuliza swali la nyongeza kwa naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi bunge mjini Dodoma kwa kustajabishwa na kitendo cha mwandishi wa habari gazeti la Mwananchi Communications Ltd alitekwa na wanachama na wafuasi wa CCM na kumporwa ipad, simu na kamera.
Katika uchaguzi ule askari WP Huruma Mkisi alipigwa jiwe na wanachama wa CCM kisha kushonwa juzi tano, waziri niambie kama CCM wanaruhusiwa kufanya vurugu na kuachiwa huru ?.alihoji Lijualikali.
“Mwandishi baada ya kutekwa na kumpora Ipad, Simu na kamera alienda polisi kulalamika na polisi waliwatafuta watu wa CCM na kumrudishia lakini wanachama hao hao wa CCM walimpiga askari, WP Huruma Mkisi kama CCM na taifa bado lipo na kuwaachia huru.”alieleza Lijualikali.
Akijibu Swahili hilo, Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alieleza kuwa unapozungumzia tuhuma kuwa hao ni wafuasi wa chama fulani inahitaji udhibitisho wa moja kwa moja.
Ninachoweza kusema kwamba uhalifu wa aina yoyote utakaofanywa na mtu yoyote wa chama chochote dhidi ya raia yoyote wakiwemo waandishi wa habari na jeshi la polisi ndio kabisa limekuwa likilinda usalama wetu na hawawezi kukubali kamwe wacheze na jeshi la polisi.
“Waandishi wa habari wamekuwa wakitoa taarifa kutoa habari kwa umma lakini hatuwezi kukubali au jeshi la polisi na raia mungine yoyote kufanyiwa matukio ya uhalifu, hatua kali litachukuliwa dhidi yao”.alieleza Naibu Waziri Masauni.
MWANDISHI ALIVYOKUMBWA NA MKASA WA KUPOKONYWA KAMERA, IPAD.
Kundi la vijana zaidi ya 10 walimvamia mwandishi wetu aliyekuwa amebeba begi mgongoni, kamera na simu aina ya Samsung Ipad eneo la Malale City kwa lengo la kupata chakula cha mchana.
Vijana hao waliokuwa na jazba, hasira na walionekana kukosa busara baada ya kumzingira na kumtuhumu kwa kuwapiga picha kupitia simu na kurekodi sauti zao wakiwa wamekaa na wengine wamesimama jambo ambalo halikuwa sahihi kwa madai yao.
“Ni tukio lililonishanga kuona vijana wale wamepandwa na jazba na hasira za haraka haraka bila ya kuchokozwa lakini kumbe lengo lao ni kunipokonya vifaa vya kazi lakini mmoja wao alisikika akieleza kuwa nilionekana na watu wa Chadema.”alieleza mwandishi wetu katika kisa hicho.
Mwandishi huyo alionekana na viongozi wa Chadema wakiwa na baadhi ya makada waliojeruhiwa na vijana wa kundi hilo la Changausile linalodaiwa kumilikiwa na CCM kwa dhana za jadi usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi huo.
“Matukio ya uvunjifu wa amani katika uchaguzi ule yalikuwa mengi lakini nilistushwa na kushangazwa kusikia askari amejeruhiwa na watu watano wakiwa miongoni waliojeruhiwa lakini kundi la vijana la Changausile lilitajwa kuhusika katika matukio yote.”alieleza mwandishi wetu.
Kamera iliweza kupatikana kwa msaada wa mmoja wa vijana ambaye hakufurahishwa na kitendo cha mwandishi kupokonywa vifaa vyake vya kazi huku akimtaka mwandishu huyo aondoke eneo hilo kwani sio salama kwake na simu haikuweza kupatikana siku hiyo.
Simu hiyo iliweza kupata siku ya pili katika ofisi ya CCM Tangani wilaya ya Kilombero majira ya saa 7:30 mchana baada ya Katibu Mwenezi wa CCM wilaya hiyo kumkabidhi.
“Ile simu ilikuwa imefutwa sehemu kubwa ya programu na mafaili yake yanayosaidia kufanya kazi kama kupiga simu, kusoma ujumbe mfupi na haikuweza kuwa na mawasiliano yoyote na kukosekana huduma ya internet.”alieleza.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alieleza kuwa wahalifu wote waliohusika kufanya uhalifu wakati wa uchaguzi mdogo wa serikali ya kijiji cha Kikwawila na serikali ya kitongoji cha Mbasa Mlimani katika mji wa Ifakara watasakwa wote na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
0 comments:
Post a Comment