NI miswada yenye ncha kali kwa nchi. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali kuwasilisha bungeni miswada mitatu kwa hati ya dharura ambayo inalinda rasilimali za nchi.
Kuwasilishwa kwa miswada hiyo kunatokana na kauli ya Rais Dk. John Magufuli aliyoitoa Juni 12, wakati akipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa dhahabu (Makinikia) iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Nehemiah Osoro.
Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema suala la mikataba ya madini litapelekwa bungeni hata kama ni kwa Bunge kuongeza wiki moja ili wabunge waweze kujadili na kupitia kifungu kwa kifungu sheria za madini na gesi.
Kutokana na ahadi hiyo jana Spika wa Bunge, Job Ndugai, alitangaza mabadiliko ya ratiba ya vikao vya Bunge ikiwemo kuongezwa hadi Julai 5, ili kuruhusu miswada mipya mitatu ukiwemo wa madini kujadiliwa katika Kamati za Bunge.
Miswada hiyo ilisomwa kwa mara kwanza jana bungeni na Bunge lilibadilisha ratiba ya awali ya kuahirisha Bunge kwa kuongeza siku tano ambapo sasa Bunge litaahirishwa Julai 5 mwaka huu.
Spika Ndugai aliitaja miswada hiyo kuwa ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali zenye upungufu uliojitokeza wa mwaka 2017 ambao utafanyiwa kazi na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria
Muswada wa mapitio, masharti hasi
Moja kati ya miswada ambayo iliwasilishwa jana ni ule wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika mikataba inayohusu maliasili za nchi.
Muswada huo wa sheria inayopendekezwa inakusudia kuweka utaratibu ambapo wananchi kupitia chombo chao cha uwakilishi yaani Bunge kupitia na kujadili makubaliano na mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi ambayo imefungana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujiridhisha endapo masharti, makubaliano na mikataba hiyo haikinzani na maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Muswada huo unakusudia kutekeleza masharti ya Ibara za 8, 9 na 27 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambazo pamoja na mambo mengine zinampa wajibu kila Mtanzania kuhakikisha kwamba anashiriki kikamilifu kulinda mali na rasimali za nchi kwa masilahi ya Watanzania na Jamhuri ya Muungano kwa ujumla.
“Kwa kuzingatia wajibu wa kila Mtanzania na kwa kutambua wajibu wa Bunge kama chombo cha uwakilishi, Sheria inayopendekezwa imelipa nguvu Bunge kupitia mikataba yote inayohusiana na maliasili za nchi ambayo imeingiwa na Jamhuri ya Muungano ilikujiridhisha kwa masharti yaliyomo katika mikataba hayo yamezingatia maslahi ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
“Muswada huu umegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya I inahusu masharti ya jumla kama vile jina la sheria na kuanza kutumika kwa sheria inayopendekezwa.
Sehemu ya II inalipa Bunge la Jamhuri ya Muungano nguvu za kisheria ili kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali iweze kupitia makubaliano na mikataba yote inayohusu maliasili za nchi ambayo imeingiwa na Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kujiridhisha na masharti yaliyomo katika mikataba hiyo.
“Kwa mujibu wa masharti yanayopendekezwa katika sehemu hii, baada ya kubaini masharti hasi katika mikataba hiyo Bunge linaweza kuitaka Serikali kufanya majadiliano upya na upande wa pili wa mkataba ili kuondoa masharti hayo.
“Sehemu ya III inaweka utaratibu wa namna ya kuanzisha majadiliano na upande wa pili wa mikataba ili kuondoa masharti hasi kama yalivyobainishwa na Bunge kwa mujibu wa ibara ya 6(2) ya Muswada,” inasema sehemu ya maudhui ya muswada huo.
Sheria inayopendekezwa imeainisha masharti ambayo kwa taswira yake ni masharti hasi na hayapaswi kuwemo katika mikataba inayohusu maliasili za nchi.
Muswada Sheria Mbalimbali wa 2017
Muswada huu unakusudia kupendekeza kutungwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambazo ni Sheria ya Madini, Sura ya 123, Sheria ya Petroli, Sura ya 392, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148 na Sheria ya Bima, Sura ya 394.
Marekebisho yanayopendekezwa yanalenga kuimarisha mifumo ya udhibiti na uwajibikaji katika sekta ya madini na petroli. Pia marekebisho katika Sheria za Kodi na Bima yanalenga kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yanayohusiana na sekta ya madini na Petroli.
Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Kuu Saba. Sehemu ya I inahusu masharti ya jumla kama vile jina na kuanza kutumika kwa Sheria inayopendekezwa, matumizi na tafsiri ya misamiati mbalimbali.
Sehemu ya II na ya III ya Muswada huu unapendekeza kufanyia marekebisho Sheria za Madini ya mwaka 2010 na Sheria ya Petroli ya mwaka 2015. Malengo ya marekebisho ni kuweka masharti yatakayowezesha wananchi na Taifa kuweza kunufaika na maliasili ya madini, petroli na gesi asilia.
Ili kuwezesha kuwepo kwa manufaa haya, maudhui ya mapendekezo yameweka masharti yatakayowezesha, kutambua na kuweka Umiliki wa Madini, Petroli na Gesi Asilia kwa wananchi chini ya Usimamizi wa Rais kwa niaba ya wananchi.
Kutambua haki na dhamana ya Serikali juu ya bidhaa zote na masalia yanayotokana na uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini, kuweka ulinzi mahsusi wa maeneo yote ya uchimbaji wa madini.
Kutambua ushiriki wa Serikali katika shughuli zote za uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini na ununuzi wa hisa katika kampuni za uchimbaji madini, kuweka utaratibu wa Bunge kufanya mapitio na maridhio yamikataba ya uchimbaji na uendelezaji wa madini, kufanyia mapitio madaraka ya Waziri na Kamishina wa Madini.
Sehemu ya IV ya Muswada inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 332 inapendekezwa kufanya marekebisho katika kifungu cha 8 na Jedwali la Kwanza la Sheria ya Kodi ya Mapato ili kujumuisha kama sehemu ya mapato ya biashara ya faida yoyote inayopatikana kutokana na haueni ya kodi kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara.
Ambapo katika sehemu hiyo inapendekeza kurekebisha vifungu vya 65M na 65N kwa lengo la kuondoa mgongano baina ya Sheria za Kodi na Sheria za sekta ya madini na mafuta. Mgangano huo umekuwa ukisababisha Serikali kupoteza mapato.
Sehemu ya V ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Bima Sura ya 394. Marekebisho yanayopendekezwa katika Sheria hiyo yanalenga kumpa nguvu za kisheria Kamishina wa Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta ya Bima (TIRA) kuainisha viwango vya
chini vya ada ya Bima (Premium) kwa aina mbalimbali za Bima zitolewazo na kampuni za Bima. Marekebisho haya yanakusudiwa kuondoa utaratibu wa sasa ambapo kila wakala wa bima hujipangia kiwango cha ada anachotaka.
Sambamba na marekebisho katika kifungu cha 72 inapendekezwa kufutwa kwa kifungu cha 134 na 137 na kuboresha masharti ya kifungu cha 133 ili kuondoa kasoro zilizopo sasa katika mfumo wa ukusanyaji wa ada ya bima (Premium) kupitia kwa mawakala wa bima.
Kwa mujibu wa marekebisho yanayopendekezwa, bidhaa zotezinazoigizwa nchini zitakatiwa bima na kampuni za bima za Tanzania.
Katika Sehemu ya VI, ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 3(3) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi sura ya 438 ili kurekebisha tafsiri ya kodi kwa lengo la kutambua kodi inayotokana na ongezeko la faida. Inapendekezwa kurekebisha kifungu cha 54(1) ili kuongeza aya ndogo ya (i) kwa lengo la kubainisha tarehe ya kulipa kodi inayotokana na ongezeko la faida.
Sehemu ya VII inapendekeza kurekebisha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148. Kurekebisha kifungu cha 68 cha Sheria hiyo ili kuweka masharti ya kuthaminisha madini kila baada ya muda fulani kwa lengo la kupatia thamani yake halisi kwa wakati husika.
Hiyo itasaidia kujua na kutambua stahili ya nchi kwa kuzingatia thamani halisi ya madini kwa wakati husika. Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017:
Muswada huu unapendekeza kutungwa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili, 2017 kwa kuweka masharti yanayohusianisha misingi iliyomo katika mikataba na itifaki mbalimbali ambazo Jamhuri ya Muungano imetia saini na kuridhia.
Baadhi ya masharti yanayopendekezwa katika Muswada huu yanatokana na Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 523(VI) la Januari 12 , 1952 na Azimio Namba 626(VII) la Desemba 21, 1952, Azimio Namba 1314(XIII) la Desemba 12, 1958.
Azimio namba 1515(XV) la Desemba 15, 1960 Azimio Namba 1803 (XVII) la Desemba 14, 1962, Azimio Namba 2158(XXI) la Desemba 6, 1966, Azimio Namba XXV la Desemba 11, 1970 na Azimio namba 32 la Desemba 12, 1974.
Kwa kuzingatia masharti yaliyomo katika mikataba hiyo, Muswada huu unakusudia kuweka masharti yatakayohakikisha kwamba hatua yoyote inayochukuliwa kuhusu uwekezaji wa rasilimali za Taifa inatambua na kuzingatia haki ya Jamhuri ya Muungano kama Taifa huru na lenye mamlaka kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa masilahi ya Taifa.
Muswada huu unakusudia kutekeleza masharti ya Ibara ya 27 ya Katiba ambayo, pamoja na mambo mengine, inamtaka kila Mtanzania kulinda na kusimamia kikamilifu rasilimali za nchi kwa masilahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hatua zinazopendekezwa katika Muswada huu zinalenga kulinda mali na rasilimali za Taifa na kuondoa aina yoyote ya upotevu au ubadhirifu wa rasilimali za nchi.
Muswada huu umegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya I inahusu masharti ya jumla kama vile jina, tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria, matumizi ya sheria na ufafanuzi wa misamiati.
Sehemu ya II inaainisha mahitaji ya msingi katika kuhakikisha kwamba mamlaka ya nchi juu ya rasilimali za Taifa yanatambuliwa na kulindwa.
Sehemu ya III inatambua na kulinda mamlaka ya Jamhuri ya Muungano juu ya rasilimali na inampatia mamlaka Waziri ya kutengeneza kanuni.
Spika Ndugai agawa kazi
Kutokana na miswada hiyo Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali zenye upungufu uliojitokeza wa mwaka 2017 utafanyiwa kazi na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mohammed Mchengerwa.
Alisema mingine miwili ambayo itafanyiwa kazi na kamati ya pamoja itakayoongozwa na Dotto Bitteko ambayo ndani yake kuna kamati nne ni Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa mwaka 2017.
Muswada mwingine ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017.
“Kamati ya pamoja itakuwa na kamati nne ndani yake, kamati hizo ni Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Ardhi, Kamati ya Sheria Ndogo na Kamati ya Sheria na Katiba.
“Kwa niaba yenu nimepokea hati ya dharura kutoka kwa mheshimiwa Rais, Kamati ya Uongozi ilikaa jana (juzi) kubadilisha ratiba, Bunge litaahirishwa Julai 5 badala ya Juni 30 kama ilivyokuwa.
“Miswada mitatu mipya ya sheria imeshasomwa kwa mara ya kwanza, itapelekwa katika kamati za Bunge, kamati zitafanya kazi kuanzia leo(jana) itapanga jinsi ya kukutana na wadau mbalimbali, kisha taarifa itawasilishwa bungeni.
“Kanuni inaeleza kwamba hati ya dharura itakayoletwa na Rais itakuja hati yenyewe yenye saini yake. Hati ya dharura imekuja kuna haja ya kulifanyia jambo hili kazi, tulijadiliana na kamati ya uongozi tukakubaliana suala hili lisonge mbele.
“Wakati Rais Magufuli akipokea ripoti ya pili ya makinikia, kwa niaba yenu nilikubali kama kuna mambo yenye maslahi mapana kwa nchi tutayafanyia kazi,”alisema.
Ndugai alisema kuna haja kwa Bunge kuwa na nafasi fulani katika masuala ya maadini na gesi ili kuzuia nchi kutumbikia katika mikataba mibovu.
Hata hivyo Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) alipoomba mwongozo alipinga miswada hiyo mitatu mipya kuwasilishwa kwa hati nya dharura badaa yake alipendekeza hati hiyo iondolewe.
Alisema kazi ya Bunge ni kutunga sheria na kwamba wabunge wawakilishi wa wananchi hivyo aliomba ijadiliwe katika Bunge lijalo ili wapate muda wa kukusanya maoni kwa wanaowawakilisha.
“Hii miswada mitatu kwa umuhimu wake na maslahi yake kwa wananchi, sisi wawakilishi tulitakiwa kukutana na wananchi, ni bora ikasomwa leo kwa mara ya kwanza hati ya dharura ikaondolewa, miswada ikaletwa katika Bunge lijalo.
“Kwa maelezo uliyotoa mheshimiwa Spika, wadau wataitwa kwa dharura wafike Dodoma kujadili, sisi wabunge vile vile, miswada mitatu inaletwa tuichaambue, mheshimiwa spika huu ni mtego wa kutufanya tushindwa kuishauri Serikali kwa kazi yetu ya kibunge,” alisema Mnyika.
Akitoa maelezo ya Serikali Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama alisema masharti ya kutunga sheria na masharti ya jumla yamewekwa katika fasihi ya nane ya kanuni za Bunge, masharti yameongezwa na kanuni ya 80 na kanuni nyinginezo.
“Miswada ambayo imeletwa imekuja kwa hati ya dharura, ili Bunge liridhie kama miswada hii inastahili kujadiliwa na Bunge ama la, kanuni ya 80(4) inasema muswada wowote wa dharura hautaingizwa katika shughuli za Bunge bila kuwa na hati iliyowekwa sahihi na Rais kuthibitisha kwamba muswada huo wa dharura.
“Kanuni zinaendelea kusema iwapo kamati inaona muswada wa sheria wa Serikali uliowasilishwa kwa hati ya dharura haustahili kamati hiyo ya uongozi itaishauri Serikali.
“Kanuni zinaendelea kusema, muswada wowote uliokabidhiwa kwako spika utaonekana unastahili ama laa, utatoa picha baada ya kujadiliwa na kamati.
“Sisi kama Serikali tumeshatimiza masharti yote ndani ya Bunge lako tukufu, tumeshakamilisha hatua zote za kufikisha miswada hiyo kwa hati ya dharura,”alisema Mhagama.
Alisema wanaoweza kulishauri Bunge baada ya kuona uzito wa kazi iliyoletwa na Serikali ni kamati husika itakayopewa kazi ya kujadili miswada hiyo.Mtanznia
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ BUNGE LAKABIDHIWA RUNGU KUJADILI KUJADILI NA KUPITISHA SHERIA ZA GESI NA MADINI DODOMA
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment