HALIMA MDEE NA ESTER BULAYA WANAHITAJIKA SANA TU BUNGENI DODOMA
Wabunge Halima Mdee wa Jimbo la Kawe na Ester Bulaya wa Bunda Mjini wamejikuta wakiangukiwa na adhabu ya Bunge kwa kile kinachodaiwa kudharau mamlaka ya Spika, na sasa watalazimika kuwepo nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja huku wakipokea nusu mshahara.
Adhabu hiyo kwa wabunge hao imetokana na kumuunga mkono mbunge wa Kibamba John Mnyika wakati alipotolewa nje na askari wa Bunge kwa kitendo cha kutaka Spika amchukulie hatua mbunge aliyewasha kipaza sauti na kumwita Mnyika ‘mwizi’ lakini kwa bahati mbaya Spika hakusikia kabisa neno mwizi ambalo wabunge wa upinzani walilisikia.
Tayari wabunge wa upinzani wamejitokeza kutetea wenzao kwamba adhabu iliyotolewa kwao na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ni kubwa na haikutenda haki kwani hawakupewa nafasi ya kujitetea.
Hili la kutopatiwa nafasi ya kujitetea naona lina mashiko kwani kila anayetuhumiwa kwa kosa lolote ni vyema naye akapatiwa nafasi ya kujitetea kwa sababu nchi yetu ni ya kidemokrasia. Tukumbuke kwamba bungeni ndipo mahala pekee ambapo kuna uhuru wa kutosha wa kuzungumza chochote madhali mtu havunji sheria za nchi.
Ibara ya 100 (1 na 2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imeweka wazi uhuru huu wa wabunge wawapo ndani ya Bunge, ibara hii inasema kuwa.
“Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.”
Kipengele cha pili cha Ibara hiyo kinasema, “Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo”.
Walioweka kipengele hiki katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawakukosea hata kidogo kwani kipengele hiki kinalenga kumweka huru mbunge na uhuru huu ndio unaowezesha yeye kuwa na mawazo mapana yatakayowezesha nchi yetu kusonga mbele.
Ukweli ni kwamba tunahitaji wabunge ambao wanaweza kuwakilisha vilivyo majimbo yao, wenye uwezo mpana wa kufikiri na pia walio huru kusema lolote bungeni kwa maslahi ya Taifa.
Tukirejea kwenye kiini cha kosa lililowaadhibu Bulaya na Mdee tunaona lilianzia kwa mbunge wa Kibamba John Mnyika ambaye alitaka aliyewasha kipaza sauti wakati na kumtukana mwizi wakati anachangia hotuba ya bajeti ya Nishati na Madini 2017/18 achukuliwe hatua lakini kwa bahati mbaya Spika hakuwa amesikia neno mwizi na hivyo kushindwa kuchukua hatua.
Kwanza nimpongeze Mnyika kwa maana alijitahidi kusimamia alichokiamini kwamba alisikia kaitwa mwizi hivyo alitaka hatua stahili zichukuliwe japo haikufanyika hivyo na badala yake yeye ndiye akabeba adhabu.
Mbunge anapokuwa na uwezo wa kujitetea yeye ni wazi anaweza kuwatetea wananchi wake vizuri zaidi, kwahiyo alichofanya Mnyika kinastahili pongezi japo kimemgharimu yeye na wenzie wawili.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina wabunge 389 vyama vya upinzani wakiwa hawazidi 120 hivyo kwa vyovyote kile watakachoamua CCM kipite kitapita tu.
Mbunge kukaa nje mwaka mmoja inamaanisha miaka yake ya kuwatumikia wananchi sio mitano tena bali ni minne,hii sio sawa kwani ni kuwanyima haki wananchi waliowachagua.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment