NYUKI WAMVAMIA MWIZI WA GARI NI MUDA MCHACHE BAADA TU KWENYE GARI KUIBIWA NA KWENDA KWA MGANGA WA KIENYEJI
Taarifa kutoka magharibi mwa Kenya zinasema kuwa mtuhumiwa wa wizi wa gari alijisalimisha kwa polisi baada ya kuvamiwa na nyuki akiliendesha gari hilo.
Mwandishi wa BBC, Wanyama wa Chebusiri kutoka Nairobi, anasema ripoti hiyo iliyoripotiwa mara ya kwanza kwenye gazeti la The Star la nchini Kenya, imewaacha wengi vinywa wazi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwenye gari aliamini kwamba mshukiwa alimuwekea dawa ya kulevya kwenye kinywaji katika hoteli moja na kumfanya apoteze fahamu.
Saa kadha baada ya kurejelewa na fahamu, alipata gari lake halipo.
Mwenye gari alitafuta msaada wa mganga wa kienyeji ambaye alimhakikishia kwamba mtuhumiwa atavamiwa na nyuki kabla ya kuondoka katika mji wa Bungoma ulioko magharibi mwa Kenya.
Punde si punde, nyuki walimvamia mshukiwa akiwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara moja maarufu mjini Bungoma.
Katika harakati za kutaka kujinusuru kutoka kwa makali ya nyuki, mshukiwa alichana mbuga akielekea kituo cha polisi cha Bungoma, huku akipiga kelele za niokoe lakini wapi, nyuki walikuwa naye 'hapa kwa hapa'.
Mwanamme huyo alijaribu kutoka katika kituo cha polisi lakini nyuki walimwandama unyonunyo kabla ya polisi kumuokoa kwa kumfungia ndani ya seli kwa mahojiano.
Mkuu wa polisi katika eneo la Bungoma David Kirui ameiambia BBC kwamba nyuki walikuwa wamezingira kituo hicho cha usalama huku mshukiwa akiwa anahojiwa kwa madai ya wizi wa gari.
Kisa hiki cha nadra kiliwastajabisha na kuwashangaza wakaazi wengi wakiachwa vinywa wazi, huku wengi wa kijiuliza, je, ushirikina ungalipo?.BBC
0 comments:
Post a Comment