WAZIRI MKUU AMWAGIA SIFA KEDEKEDE MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO ANNA MGHWIRA KWA KUCHAPA KAZI
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amempongeza na kumsifu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kwa kudhibiti usafirishaji mahindi nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa amekamata malori zaidi ya 103 ambayo yalikuwa yakisafirisha mahindi kwenda nchi jirani tangu Sikukuu ya Idd hadi jana.
Majaliwa alisema amemsifu Mghwira kutokana na kitendo hicho cha kutekeleza agizo alilitoa kwenye Baraza la Idd lililofanyika mkoani Kilimanjaro la kupiga marufuku kusafirisha mahindi nje ya nchi. Alisisitiza msimamo huo wa Serikali wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Ritta Kabati (CCM) aliyetaka Serikali iruhusu kusafirisha mahindi nje ya nchi kwa mikoa iliyozalisha ziada.
“Hakuna kusafirisha mahindi nje ya nchi, ikiwa lazima basi kibali kitolewe na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kusafirisha unga,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza: “Kama kuna ulazima ya kuuza chakula nje, basi mtu anayetaka kufanya biashara lazima apate kibali kutoka wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ya kuuza unga wala si mahandi.”
Waziri Mkuu alisema kwa kuuza unga, tayari viwanda vya kukoboa na kusaga vitakuwa vimepata kazi, wananchi watapata ajira na pumba itabaki kwa ajili ya matumizi ya mifugo.
Alisema serikali inadhibiti chakula ili kukidhi mahitaji ya ndani kutokana na kwamba baadhi ya maeneo mvua haikunyesha na vizuri kati ya mwezi Novemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu baadhi ya maeneo yalikosa mvua, na hivyo nchi baadhi ya maeneo kupatwa na ukame.
“Serikali imedhibiti usafirishaji wa chakula kutokana na kwamba kuna maeneo hapa nchini kama Mwanza, Geita, Sengerema alikotembelea siku za hivi karibuni yana uhaba wa chakula,” alisema.
“Hivi sasa mahindi ndicho chakula kikuu kwa kuwa baadhi ya makabila kama Wahaya, Wachaga na Wamasai ambao walikuwa wakila vyakula vingine sasa wanakula ugali kama chakula kikuu,” alisema.
Serikali inadhibiti kutokana na ukweli kwamba wanaofika kununua mahindi hapa nchini katika maeneo ya Karatu, Kibaya na Kongwa na mahali si wananchi wa maeneo mengine bali ni watu wa kutoka nje.
Alisema hata nchi jirani ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Sudani Kusini na Somalia zinaomba chakula kutoka Tanzania, hivyo tusipodhibiti, nchi inaweza kuwa na uhaba wa chakula.
Aliwaomba wabunge waunge mkono msimamo huo wa serikali kutokana na kwamba chakula hakitoshi na lazima tuwe na akiba kwa ajili ya maeneo mengine nchini.Habarileo
0 comments:
Post a Comment