SABABU ZA SIMBA JIKE KUMNYONYESHA MAZIWA YAKE MTOTO WA CHUI HIFADHI YA NGORONGORO
Simba aliyepewa jina la Nosikito akiwa amejipumzisha huku mtoto wa chui akiendelea kunyonya.
Arusha. Wakati mtandao wa kimataifa wa SafariBookings.com umeitangaza Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika inayowavutia zaidi watalii, simba amekutwa Hifadhi ya Ngorongoro akinyonyesha chui.
Ni tukio ambalo halijawahi kutokea duniani, kwa simba kunyonyesha mtoto wa chui.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza imetokea katika eneo la Ndutu ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, eneo ambalo ni moja ya maeneo ya urithi wa dunia kutokana na maajabu yake.
Hili ni tukio la ajabu simba kunyonyesha mtoto wa chui ambao kwa kawaida ni maadui na tukio hili linaendana na jina la utafiti alilopewa simba huyu ambaye anaitwa Nosikito.
Nasikito ni jina la kimasai, likiwa na maana maziwa ya mwanzo, ambayo ng’ombe anatoa mara tu baada ya kuzaa na maziwa hayo huwa anakunywa ndama pekee.
Tukio la hili la simba Nosikito kunyonyesha mtoto, lilitokea Julai 11 muda wa jioni na wa kwanza kuona tukio hili na kulisambaza kwenye vyombo vikubwa vya habari duniani ni mtalii, Joop Van De r Linde ambaye amefikia katika Hoteli ya Ndutu Safari.
Muda mfupi baada ya kusambaza tukio hilo, maofisa wa mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kanda ya Ndutu, wakiongozwa na Mkuu wa Kanda hiyo, Edward Ngombei nao walifika kushuhudia.
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Fredy Manongi anasema tukio hili halijawahi kuripotiwa kwenye tafiti za masuala ya wanyamapori.
Anasema baada ya kupata taarifa hizo, wao kama mamlaka walianza uchunguzi na kubaini simba huyo, alikuwa amezaa watoto watatu kati ya Juni 27 hadi 28.
Hata hivyo, anasema baada ya kuzaa na kuwapeleka kuwahifadhi katika vichaka vya pango, inaonekana simba huyo aliwaacha pale watoto na kuondoka.
Anasema kwa siku kadhaa, simba huyo hakurudi kuona watoto wake na inawezekana amewatelekeza ama amesahau sehemu alipowaficha.
“Kawaida simba hata chui, wakizaa huwa wanaficha watoto ili kuwalinda kuliwa na wanyama wengine wakiwamo simba, chui na fisi,” anasema.
Anasema inawezekana simba huyo alipotoka eneo aliloficha watoto na kuwakosa, njiani alikutana na mtoto huyo wa chui. “Huyu mtoto wa chui pia, alikuwa na wiki kati ya tatu na mbili hivi tangu kuzaliwa hivyo, akaanza kumnyonyesha,” anasema.
Anasema tukio hili, halijawahi kutokea na ni la ajabu sana, kwani kwa kawaida simba hula chui watoto, hata watoto wa simba.
Simba Nosikito amewahi kuzaa kabla
Kabla ta tukio ya kunyonyesha mtoto wa chui, simba huyo mwenye umri wa miaka mitano, katika uzazi wa kwanza alizaa watoto wanne ambao aliwakuza vizuri.
Dk Manongi ni mtaalam wa masuala ya wanyamapori anasema huyu simba yupo katika utafiti na amefungwa kola yenye mtandao wa GPS (Global Positioning System) ambayo inafuatilia mwenendo wake.
“Simba huyu ni sehemu ya simba ambao wapo katika utafiti hivyo, imekuwa rahisi baada ya tukio hili kufatiliwa kwa karibu na kupata kumbukumbu zake,” anasema.
Nickson Nyanye ambaye pia ni mtaalamu wa wanyamapori, katika idara ya mahusiano Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, anasema tukio hilo la simba kunyonyesha mtoto wa chui litaingia katika historia ya uhifadhi duniani.
Anasema kitaalamu tukio hilo halijawahi kutokea, lakini simba kwa kawaida wakiwa kwenye makundi huwa mtoto anaweza kunyonya mama zaidi ya mmoja.
“Huwa hawana shida sana katika kunyonyesha wakiwa kwenye kundi, mtoto wa simba anaweza kunyonya jike lolote ambalo limezaa muda huo na wamekuwa hawadhuriani,” anasema.
Hata hivyo, anasema kwa tukio la simba kunyonyesha mtoto wa chui ni upendo wa simba mzazi, lakini hauwezi kudumu kwa muda mrefu.
“Kwa kuwa hawa wanyama sio marafiki sana, urafiki wa simba huyu Nasikito ni wake pekee na kama akijiunga na kundi la simba wengine ni lazima watamla huyu chui,” anasema.
Dunia ilivyoshangazwa na tukio hili
Vyombo vyote vikubwa vya habari duniani na pia mitandao ya kijamii, wameripoti tukio hili la aina yake, kuwahi kutokea duniani.
Daktari Luke Hunter, ambaye ni rais muhifadhi mkuu wa Panthera, shirika kuu la ufugaji wa wanyama aina ya paka aliambia BBC kwamba kisa hicho ni cha kipekee.
Anasema sio kitu ambacho nilijua ambapo simba angeweza kuwalea watoto wa simba mwengine.,...hiki ni kisa tofauti sana.
“Sina kisa chengine chochote nikijuacho kati ya familia ya mnyama paka kwa mfano pale ambapo mnyama mmoja amechukua mwana wa mnyama mwengine katika familia hiyo hiyo na kumnyonyesha,” anasema.
Simba wengi wa kike huwauwa watoto wa chui wanapokutana nao na huwaona kama wapinzani katika mapambano ya kutafuta chakula.
Daktari Hunter anasema Nosikito ana watoto wachanga walio na umri sawa na mwana huyo wa chui wakiwa na wiki mbili hadi tatu hivi. Simba huyo alikuwa kilomita moja kutoka nyumba yao ambapo kuna maficho ya watoto wake alipokutana na chui huyo mdogo.
Simba Nosikito aungana na wenzake.
Simba Nosikito juzi na jana ameonekana tena eneo la Ndutu lakini safari hii, akiwa katika kundi la simba wengine watano.
Dk Manongi anasema, haijafahamika bado ni kwa nini hajarudi kunyonyesha watoto wake na jana na juzi hakuonekana tena kuwa na chui mtoto.
“Tunafuatilia zaidi suala hili, kwanza kubaini watoto wa simba wapo wapi kwani kwenye lile pango hawaonekani, lakini pia tunafuatilia chui aliyetelekeza mtoto na mtoto yupo wapi baada ya kunyonyeshwa na simba,” anasema.
Tukio hili kuvuta watalii zaidi
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Manongi anasema, tukio hili ni sehemu tu ya maajabu yanayopatikana Ngorongoro na ana imani litavuta watalii na watafiti zaidi.
“Tukio hili kwanza linathibitisha kuboreshwa kwa uhifadhi kwani kuna utulivu sana Ngorongoro kwa wanyama wote na nadhani hili ni tukio ambalo linaongeza sifa ya Ngorongoro kama eneo la Urithi wa Dunia,” anasema.
Anasema Ngorongoro, itaendelea kuwa na maajabu zaidi kupitia wanyamapori, mazingira na utalii mpya ya kijiolojia ambao haupo maeneo mengi duniani.
Huyu ndiye simba Nosikito na sasa anaungana katika historia ya wanyama wa kipekee waliopo Ngorongoro, kuanzia Faru John ambaye baadaye alikufa na Faru Fausta ambaye bado yupo akiwa ndio faru mkubwa katika eneo huru la hifadhi kuliko faru yoyote kujulikana Afrika.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment