TUNDU LISSU: SITANYAMAZA KUIKOSOA SERIKALI LABDA NIWE NIMEKUFA
MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusema kuwa atanyamaza tu baada ya kufariki dunia.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alipata dhamana jana baada ya mahakama hiyo kubaini hoja za Serikali za kumnyima haki hiyo hazina mashiko.
Baada ya kutoka mahakamani, alikwenda katika ofisi za Chadema zilizopo Kinondoni, ambako pamoja na mambo mengine, alisema ataendelea kuikosoa Serikali hadi pale atakapokufa.
“Hakuna gereza litakalotunyamazisha, watu wakipelekwa mahabusu watazungumza wakiwa mahabusu, wakifungwa watazungumza wakiwa kifungoni, hivyo ili wanyamaze itabidi kwanza wafe… tutanyamaza tukiwa wafu kwa sababu wafu hawasemi,” alisema.
Lissu alisema kuna haki ya kuwasema na kuwakosoa wale waliopewa madaraka na wananchi.
Alisema katika sheria ya uchochezi ya mwaka 1953, kutoa kauli yoyote yenye lengo la kukosoa matendo ya Serikali, sera si kosa na wala kumkosoa rais na Serikali yake si kosa.
“Sasa ukisema wanakukamata, wanakushtaki kwa uchochezi, wanakupiga, wanakupeleka central (kituo kikuu cha polisi) au Oysterbay wakikupeleka sio kosa, bali unatumia akili zako kuikosoa Serikali,” alisema Lissu.
KUKATAA KUPIMWA MKOJO
Akizungumzia kuhusu kupimwa mkojo, Lissu alisema alipelekwa na askari kwenye nyumba iliyo karibu na Ocean Road, lakini alikataa kutekeleza hilo.
“Niliwaambia nyie maaskari mimi nimeshtakiwa kwa uchochezi, unathibitishaje uchochezi kwa kupima mkojo?” alisema Lissu.
Alisema askari hao walimjibu kuwa kuna vitu wanavitaka, akawaeleza: “Nendeni mkanishtaki, hamjapata oda ya hakimu, hamtaona mkojo wangu.”
Baada ya kauli hiyo, alisema askari hao walimwambia kuwa wao wana mamlaka.
“Nikawaambia mimi ni Rais wa Mawakili (TLS). Siku ukikamatwa, ukaambiwa kupimwa damu, mkojo waambie hutaki hata kama wamekushtaki.
“Ukitoa mkojo na usiposaini hakuna dili, walichokuwa wanatafuta wapate dili ya kutengeneza ‘headline’ (kichwa cha habari), ‘huyu anasema hivi kwa kuwa anatumia dawa’, nani asiyejua polisi wanabambika? Nikakataa, nikawaambia mnataka twende kunisachi twendeni.”
AKUTANA NA RUGEMELIRA SEGEREA
Lissu alisema akiwa Segerea alikutana na wafanyabiashara James Rugemalira na Harbinder Singh Sethi wanaokabiliwa na kesi ya uhuhumu uchumi na utakatishaji fedha.
“Mwaka jana nilisema hawa lile dili (kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow) watu lazima wawajibike, waliowapa hela, waliosaini BoT (Benki Kuu ya Tanzania), walioruhusu hizo fedha kwa kusema James Rugemalira na Harbinder Singh wapewe wako wapi?” alihoji.
Lissu alihoji wapi walipo waliopewa mgawo wa fedha za Escrow.
HOJA ZILIZOMTOA LISSU
Kabla ya kutoa uamuzi wa dhamana jana, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri, alipitia hoja za pande mbili zilizokuwa zinapingana, zilizowasilishwa mahakamani hapo mwanzoni mwa wiki.
“Hii kesi ina dhamana, hoja kwamba anakabiliwa na kesi nyingi zenye viashiria va uchochezi haina mashiko kwa sababu hakuna taarifa kuwa aliwahi kuruka dhamana.
“Kwangu mimi hiyo haitoshi kumuweka mahabusu, hoja ya kwamba aendelee kuwepo rumande kwa usalama wake, hakuna taarifa kwamba akipewa dhamana maisha yake yatakuwa hatarini.
“Mshtakiwa anawakilishwa na mawakili 18 wanaomuombea dhamana, wanafanya hivyo kwa upendo walionao dhidi ya mshtakwa, hivyo haiwezekani akipewa dhamana atadhurika.
“Mahakama inakubali maombi ya dhamana, mshtakiwa atadhaminiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili, watasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja na mshtakiwa hatakiwi kusafiri bila kibali cha mahakama,” alisema.
Baada ya kutoa masharti ya dhamana, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi kwa nusu saa ili watafutwe wadhamini hao ambao walipatikana kwa juhudi za Wakili Peter Kibatala aliyetoka nje ya mahakama kuwatafuta.
Awali wadhamini hao walishindwa kuingia eneo la mahakama kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi kulikotokana na kuwapo kwa kesi za ugaidi mahakamani hapo.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu, Simon Wankyo, alidai mahakamani kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu kwa kuanza usikilizwaji wa awali.
Lissu alidhaminiwa na wadhamini wawili walioweka dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja.
ULINZI MKALI
Akitoka eneo la mahakama baada ya kutimiza masharti ya dhamana Lissu alisindikizwa na askari wengi kuelekea katika gari lake na hakuruhusiwa kuzungumza hata na wafuasi wa chama chake waliofika mahakamani hapo.
Hali hiyo ilimkuta pia wakili wake, Fatma Karume ambaye alipata wakati mgumu wakati wa kuingia mahakamani.
Fatma alichelewa kuingia na alitakiwa kuondoka eneo hilo harakaharaka kama alivyofanyiwa Lissu.
Awali, Lissu alifika mahakamani saa mbili asubuhi, akiongozana na watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi za ugaidi, huku wakisindikizwa na magari zaidi ya sita yaliyokuwa yamebaba polisi wenye silaha.
HATI YA MASHTAKA
Katika hati ya mashtaka Lissu anakabiliwa na shtaka la kutoa lugha ya uchochezi Julai 17, mwaka huu maeneo ya Ufipa wilayani Kinondoni.
Anadaiwa kusema kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.Mtanzania
0 comments:
Post a Comment