BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAGOMBEA CCM KUANZA KUINAMISHA VICHWA CHINI BAADA YA KUPIGWA X NA VIKAO VYA JUU


Unaweza kusema kuwa wanachama wa CCM waliozoea utamaduni wa zamani wa uchaguzi, leo wanaanza “kuisoma namba” wakati vikao vya juu vitakapoanza kukutana kuchuja wagombea wa ngazi ya wilaya.

Watakaopitishwa pia watakuwa na wakati mgumu wa kujua mustakabali wao hadi watakapotangazwa mbele ya mkutano wa uchaguzi, ikiwa ni staili mpya ambayo inaweza kung’oa wengi.

Kulingana na ratiba ya vikao hivyo vitakavyofanyika jijini Dar es Salaam chini ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli, Kamati Kuu ndiyo inayofungua dimba kwa kukutana leo na kesho wakati Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itakutana Jumamosi na Jumapili ijayo.

Kama ilivyokuwa katika ngazi za mashina, matawi na kata, uchaguzi huo unatarajiwa kuwa mchungu kwa wagombea watakaoteuliwa kwa kuwa watatakiwa kwenda mbele ya wapigakura na kukutana nao kwa mara ya kwanza siku ya uchaguzi badala ya ytamaduni uliozoeleka wa kujitangaza kwa kufanya kampeni.

Vilevile, staili hiyo ya uchaguzi ambayo ni ngeni ndani ya chama hicho, inaweza kuwaangusha wagombea wengi au kubatilisha chaguzi kwa watakaokwenda kwa mazoea ya miaka mingi ya kutegemea fedha na umaarufu kama mtaji wao.

Uchaguzi huo ngazi ya wilaya unakuja baada kukamilika ule wa mashina, matawi na kata ambao katika baadhi ya maeneo, ulikumbwa na vitendo visivyofaa na baadhi yake kufutwa na kuagizwa kurudiwa upya.

Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, katika hatua hizo za awali, tayari mashina 220,801 kati ya 222,126 yamekamilisha uchaguzi, pia matawi 22,447 kati ya 23,246 pamoja na kata 3,726 zimeshapata viongozi wake.

Hata hivyo, chama hicho kilibatilisha chaguzi katika kata 44 kutokana na kubainika mambo yaliyopigwa marufuku kama kuwa na makundi, kupanga safu na kuweka mapandikizi au wasaliti.

Mambo mengine yaliyojitokeza ni kupitisha wagombea ambao ni watuhumiwa wa ubadhirifu wa mali za chama; wasio wakazi wa maeneo husika; waliopitishwa baada ya wengine kuonewa katika uteuzi na kuwapo mgombea mmoja tu aliyepitishwa.

Si hayo tu, pia lilijitokeza tatizo la kutolewa taarifa zisizo sahihi kuhusu wagombea zenye lengo la kupotosha vikao vya juu.

Kwa maana hiyo vikao hivyo vya juu vitapitia taarifa za mienendo ya waliojitokeza kugombea kama walijitangaza wakati wa kuchukua fomu, kufanya kampeni au kuwa na madoa ya rushwa na usaliti kwa chama hicho na kuwaengua watakaobainika.

Katika mahojiano na maalumu na Mwananchi hivi karibuni, mwenyekiti wa CCM mkoani Kigoma, Dk Amani Kaborou alisema ndani ya chama hicho kuna watu ambao hawajaukubali mfumo huo mpya wa uchaguzi.

Alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakipanga safu kwa kutoa fomu kwa watu wanaotaka wagombee au kuwanunulia kadi za uanachama ili baadaye waweze kuwachagua na wengine huficha fomu na kuwapa wagombea wao.

“Matatizo tunayokumbana nayo katika uchaguzi yanaweza kusemekana yanaanzia na uchaguzi huu, kwa kuwa umekataza kabisa kabisa kupanga safu, yaani kuteua watu ambao baadaye watakuja kukupigia kura wewe katika awamu yako,” alisema Dk Kabourou.

“Hilo la safu kwa kweli naona watu wengi walikuwa hawajaliafiki. Naona hilo limekuwa kila mahali tangu ngazi ya tawi na kata.”

Vikao vya leo

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Poleple ametaja ajenda moja ya vikao hivyo kuwa ni kujadili, kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho wa wanachama wanaoomba uongozi ngazi za wilaya.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameeleza masuala mengine yanaweza kuzungumzwa katika vikao hivyo ambavyo pia vitasuka timu mpya ya Rais Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza mabadiliko katika mfumo na uongozi wa chama hicho.

Miongoni mwa masuala hayo ni mjadala mzima wa hali ya kisiasa, kuhusu masuala yanayoendelea nchini.

Vikao hivyo vya juu pia vinafanyika katika kipindi ambacho kumekuwa na matukio yaliyolistua Taifa, huku misuguano ikiendelea bungeni kati ya uongozi wa mhimili huo na upinzani.

Suala lililotikisa nchi ni kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, tukio ambalo wapinzani wamelielezea kuwa ni la kisiasa.

Suala hilo lililoibua mjadala wa usalama wa wanasiasa pia linaongezwa nguvu na matukio mengine ya kushambuliwa kwa risasi kwa brigedia mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na kulipuliwa kwa ofisi za wanasheria.

Pia kwenye vikao yanaweza kujitokeza masuala mengine kadhaa yanayowaathiri wananchi kama mgogoro wa Zanzibar, bomoabomoa na hatima ya kesi ya uchaguzi wa jimbo la Longido na hali ya kiuchumi.

Maoni ya wachambuzi

Akizungumzia vikao hivyo, mjumbe wa Baraza la Umoja wa Wanawake (UWT) wa Manispaa ya Iringa, Mariam Fundi alijikita kwenye uteuzi wa wagombea, akisema mtindo wa uchaguzi bila wagombea kujinadi umepunguza vitendo vya rushwa kwa kiwango kikubwa.

“Jina langu nilikwenda kulisikia ukumbini tu, kwa hiyo ni mazingira ambayo mtu huwezi kutoa rushwa kwa sababu huna uhakika umo au haumo. Hii imeleta usawa kwa maskini na matajiri,” alisema.

Mariam aliyewahi kuwa katibu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Iringa, alisema uchaguzi huo umerejesha heshima kwa chama hicho.

Alisema majimbo na mitaa mingi ilipotea kwenye chaguzi zilizopita kutokana na makundi yaliyokuwa yakizalishwa kwa rushwa.

“Wanaposema CCM imezaliwa upya hiyo ndiyo maana yake,” alisema.

Kada mwingine wa CCM katika Jimbo la Ubungo, Martine Lucas alisema kuna athari kwa wagombea kutojitangaza kwa kuwa hawawezi kujulikana mapema kwa wapigakura.

“Ukienda kumjua mgombea ukumbini utampimaje sasa? Utajuaje kama atajenga au kubomoa chama chetu? Ni kweli imepunguza rushwa lakini imetunyima nafasi ya kuwajua,” alisema.

Alisema mianya ya rushwa ingezuiwa wakati wagombea wanajulikana kwa kuwa hata waliochukua fomu na kuzirejesha hawajulikani.

Alisema hali hiyo inaongeza hofu kwa wagombea kwa kuwa si ajabu waliotarajia kuona majina yao wakakuta yamekatwa bila maelezo.

Utaratibu huo mpya pia ulizungumziwa na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana ambaye alisema ni njia muafaka ya kupambana na rushwa.

“Rushwa ililalamikiwa kupita kiasi ndani ya CCM,” alisema Profesa Bana. “Ni mapema mno kukosoa utaratibu huu. Hebu tuangalie matokeo yake japo naamini watakaopatikana ni viongozi waadilifu wasio na mawaa.”

Alisema kujinadi kwa kuzunguka huko na kule au kutumia mitandao, kunaweza kusababisha mianya ya rushwa na matokeo yake chama hicho kupata viongozi wasio waadilifu ambao walikuwa wakitumia mwanya huo kama msitu wa kuficha maovu.

“Mradi wenye chama chao wameona inafaa, nadhani ni sahihi, wanaCCM wote ni sawa hivyo aina hii ya uchaguzi inaleta usawa,” alisema.

Hata hivyo, Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga alisema chama hicho kinapaswa kufuata miongozo na kanuni za uchaguzi zilizo kwenye katiba yake.

Alisema kidemokrasia, wanachama walizoea kuwajua wagombea wao mapema, kuwapima na kuwachuja kabla ya kuwapigia kura.

Hata hivyo, Dk Sanga alisema faida pekee ya kuwapata wagombea bila kujinadi ni kuepuka vitendo vya rushwa huku hasara ikiwa kuwachagua watu wasiojua sifa zao licha ya kuwa vikao vya juu vinakuwa vimeshawachuja.

“Cha msingi, ni wao wenyewe kujiridhisha kama kweli watakaochaguliwa wataweza kukivusha kwenye chaguzi zijazo,” alisema.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: