HAMISA MOBETO AMBURUZA DIAMOND MAHAKAMANI KISA MATUNZO YA MTOTO
Mwanamitindo Hamisa Mobeto, amemburuza Mahakama ya Watoto msanii Nasib Abdul maarufu Diamond Platinumz, akidai matunzo ya mtoto wake wa kiume aliyezaa na msanii huyo.
Katika madai yake Hamisa, kupitia mawakili wake Abdullah Lyana na Walter Godluck wa Kampuni ya Uwakili ya Century Attorneys, anaomba Diamond amuombe msamaha kwa umma kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake na pia amkubali mtoto huyo kuwa wake kwa masharti ya wazi.
Msanii huyo alitumiwa wito Septemba 14, mwaka huu akitakiwa mahakamani hapo kwa ajili ya mwafaka wa madai yaliyofunguliwa dhidi yake ambapo hakujibu, kutokana na hali hiyo, Hamisa kupitia mawakili wake hao akafungua kesi Namba 234, mwaka 2017 kwa mujibu wa Sheria ya watoto ya mwaka 2009.
Anadai Diamond amlipe Sh milioni tano kwa mwezi kwa ajili ya matunzo yake na mtoto au zaidi kama mahakama itakavyoamua kutokana na hali yake kutotengamaa tangu amejifungua ambapo amekuwa akijihudumia mwenyewe.
Hamisa anadai alipwe Dola za Marekani 15,000 kama gharama za mtoto hadi sasa.
Katika madai hayo, Hamisa pia anadai maombi hayo yakishindwa kutimizwa ndani ya siku saba baada ya mlalamikiwa kupokea wito huo, watafungua madai mapya dhidi yake ambayo yanajumuisha uamuzi wa baba wa mtoto.
Aidha, katika madai hayo atalazimika kudai fidia kutokana na matusi na maneno yasiyofaa dhidi yake yaliyotolewa na Diamond na mpenzi wake Zari ambayo yamemsababishia maumivu.
0 comments:
Post a Comment