Kila mmoja atakubaliana kwamba mahusiano baina ya wapendanao yalikusudiwa kuwa ya upendo, maelewano, kuaminiana, na urafiki wa hali ya juu, kwa bahati mbaya hali halisi siyo hiyo katika mahusiano ya wengi.
Wengi wetu wameumizwa kwa mpenzi mmoja au mara nyingine wote kutokuwa waaminifu katika mahusiano yao.
Kutokuwa mwaminifu hapa namaanisha hali ya mpenzi mmoja kuwa na mahusiano yasiyo rasmi na mpenzi au wapenzi wengine pembeni.
Zifuatazo ni alama 11 za mpenzi asiye mwaminifu:
Kuongezeka ghafla kwa hali ya kujipenda
Yawezekana mpenzi wako alikuwa amezoea kuvaa kawaida, hapa simaanishi kutopendeza, na wewe ulikuwa umemzoea katika hali fulani ya mavazi au mitindo mara ghafla anabadilika na kuwa mtanashati zaidi, ana badilisha mavazi, anapenda mavazi ya garama, labda alikuwa hatumii manukato lakini gafla anaanza kupenda manukato tena ya garama, anakuwa mtu wa kujijali zaidi ya kawaida yake kiasi ambacho hukumzoea
Kuanza kuchelewa kutoka kazini mara kwa mara
Sio kwamba kila mtu anapochelewa kutoka kazini basi anakuwa sio mwaminifu, lakini zaidi ya asilimia 75 ya ambao wamekuwa na mahusiano nje wamekuwa wakitoa visingizio vinavyohusiana na kazi, vikao, mikutano na safari za kikazi, yamkini wewe ni shahidi wa hili.
Kupenda kutembea na mipira ya kinga “condoms” mara kwa mara
Yamkini ni kweli kunakujali na labda katika mahusiano yenu hili sio la kushtua kwa sababu mnajali afya zenu au mnatumia kondomu kwa sababu zaidi ya moja, lakini inakuwaje pale unapogundua kuwa ile kondomu uliyokuwa unaiona haipo tena na yamkini wewe hukuhusika katika kuitumia.
Mazingira tatanishi ya simu
Inawezekana mpenzi wako sio mtu wa kupokea simu au kupiga simu sana, na hivi ndiyo ulivyomzoea, mara gafla simu zinaanza kumiminika mpaka mida ya usiku.
Yamkini pia alikuwa yuko huru hata simu yake inapolia waweza ichukua na kumpatia lakini gafla anakuwa na hofu kubwa na kuificha simu yake, nimeongea na wengine ambao wanakwenda na simu hadi bafuni isije ikasikika.
Harufu ambazo hujazizoea
Kwa kuwa wapendanao huwa wamezoeana, mara nyingi hata aina ya manukato mmoja anayotumia yanakuwa yanajulikana kwa mwenzake, hata kama mmoja hajui jina la manukato anayotumia mpenzi wake lakini basi atajua walao jinsi yanavyonukia.
Sasa hembu fikiri unamkuta mpenzi wako ametokea na ana harufu ya tofauti kabisa na uliyoizoea, yamkini umeisikia harufu hiyo akiwa amerudi toka kazini wakati asubuhi alipoondoka alikuwa na harufu ile uliyoizoea.
Tabia za kuanza kukufuatilia sana au hata kukuganda
Kuwa macho sana na tabia za mpenzi wako kukuchunguza sana unapotoka, ulipokuwa, ulikuwa na nani, mlifanya nini, nani alikuwepo mwingine, unaenda wapi, kwa muda gani. Yawezekana yote hii ni hali ya kujilinda au kujihisi mdhambi (guilty conscious) inayomsumbua.
Mabadiliko katika tendo la ndoa
Jambo hili laweza kujidhihirisha katika picha mbili tofauti. Kwa kawaida wapenzi huwa na mazoea fulani katika tendo la ndoa, kwa muda waliokaa pamoja kila mmoja humfahamu mwenzake kwa kiasi fulani. Inawezekana likawa jambo la kushangaza pale ambapo ghafla unamuona mpenzi wako anapoteza kabisa hamu ya tendo la ndoa, au hata mnapokuwa katika tendo hilo humuoni akifurahia bali anakuwa kama anayelazimishwa au kutohamasishwa na chochote.
Marafiki wa mpenzi wako kukukwepa
Ni hali ya kawaida kuwa karibu au kuzoeana na marafiki wa mpenzi wako, mara nyingine mtawasiliana nao kutaka kujua aliko mpenzi wako au kinachoendelea kwao.
Inabidi ujiulize sana pale inapotokea ghafla wale marafiki wa mpenzi wako uliowazoea, uliokuwa unawapigia simu wakati wowote leo wana kukwepa na hata simu hawapokei na mara nyingine wakipokea hawakupi taarifa yakueleweka au wanakudanganya.
Kuzungumza sentensi za kutatanisha.
Wapenzi wengi hujuana kwa mengi, ikiwemo pia namna ya kuzungumza au kuonyesha hisia. Unaweza kukuta katika mapenzi yenu mpenzi wako anaanza kuwa na sentensi ngumu na zisizo kuwa na msingi kwa mfano anasema.
“kwa jinsi hii sidhani kama tutafika” “mi siamini kama mapenzi yanadumu” “yani ndio maana watu wanashindwa kukaa na mpenzi mmoja” na mara nyingine anaweza kukuuliza baadhi ya maswali moja kwa moja ili kukuona utajibuje.
Kuzidi kwa tabia za kutoonekana au kuponyoka.
Yawezekana mpenzi wako alikuwa na tabia ya kuwepo nyumbani mida isiyokuwa ya kazini au wikiendi, muda mwingi alipenda kuwa na wewe na akiaga basi atasema anakwenda wapi na akimaliza hurudi mapema kwa sababu ana kiu ya kuwa na wewe, mara gafla siku hizi haagi anakwenda wapi, ukiuliza inawezakuwa vita.
Tabia za kuficha fedha
Japokuwa hili ni tatizo kwa wengi lakini wako wapenzi ambao wamekuwa na tabia ya kuambiana kwa uwazi matumizi na mapato yao.
Hakuna kitu wamefanya kuhusu fedha zao pasipo kuambiana na hivi ndivyo mlivyozoeshana, mara ghafla mmoja anaanza kuwa na siri kuhusu fedha zake au matumizi yake, na wala hapendi kuulizwa ulizwa kuhusu suala hilo.
Makala haya yameandikwa na DK Chris Mauki ambaye ni Mtaalamu wa mahusiano na ushauri wa kisaikolojia.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment