Wabunge wa Chadema, Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) na Godbless Lema(Arusha Mjini) leo Jumapili wamemwaga ushahidi ambao unawatuhumu madiwani 10, kuhama katika chama hicho kwa kupewa rushwa na wameomba Rais John Magufuli kuchukuwa hatua ili kukomesha vitendo hivyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Nassari na Lema ambao kesho wataenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Valentino Mlowola kumkabidhi ushahidi huo, wamesema wamebaini madiwani waliohama walipewa rushwa.
Nassari amesema katika ushahidi wao, ambao wameuonyesha leo kwa wanahabari wamedai madiwani waliojizulu wamepokea rushwa ya fedha, ajira, posho za vikao vyote vilivyobaki na kiinua mgogongo cha udiwani miaka mitano na kulipiwa mkopo wa benki.
"Rais Magufuli amejipambanua kuwa anapiga vita rushwa hivyo kwa kuwa tuna ushahidi wote wa rushwa, tutakabidhi Takukuru na tuna imani watachukuwa hatua ili Rais asihusishwe na hii dhambi mbaya," amesema.
Nassari aliwataja viongozi waliorekodiwa kwa kamera za siri wakiwashawishi madiwani kujiuzulu kwa ahadi za rushwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri na watendaji wa idara kadhaa za serikali.
"Hawa viongozi tumetumia vifaa vya kisasa kuwarekodi kwenye ofisi zao na tuna kila kitu na leo tumetoa nusu tu, wakipinga tutatoa nyongeza zaidi...hili jambo sio dogo tunaweza kupigwa risasi na kupoteza maisha lakini tunataka dunia kujua nini kinafanyika," amesema.
Nassari amesema wanatarajia kuchukua hatua nyingine kadhaa kwa viongozi hao hasa kutokana na matamshi yao ya kudhalilisha wa Meru, ikiwepo kukaa na viongozi wa mila (washiri) na wananchi na kutangaza azimio la waMeru .
"Kama mlivyosikia sauti mkurugenzi anatudhalilisha waMeru, pia anasema katika chaguzi zijazo, madiwani waliohama watapitishwa kugombea kupitia CCM na hata kama wakishindwa watatangazwa kushinda kwani yeye anayelipwa mshahara na Serikali ya CCM hawezi kuwatangaza wapinzani kushinda," amesema.
Amesema tayari baadhi ya madiwani waliojiuzulu, wamepewa ajira serikalini za muda na kudumu, wengine miradi waliokuwa wameahidi kwenye kata zao imeanza kutekelezwa na mmoja ambaye shule yake na kituo cha yatima vilivyokuwa vimefungwa kutokana na mgogoro vimefunguliwa.
"Kuna diwani aliyejiuzulu ….alikuwa anataka kuoa na hana fedha za kutosha na kwenye video tumesikia katibu tawala akipewa jukumu la kusimamia ndoa yake na amefanya hivyo...kwa hiyo mambo mengi waliyoahidiwa yametekelezwa," amesema.
Nassari pia amesema katika ushahidi huo, wanatajwa viongozi wa juu wa CCM kuchukua sifa za madiwani waliojizulu ili kuwatafutia nafasi nyingine jambo ambalo ni rushwa.
Amesema katika picha ya video anaonekana, Mnyeti akimshawishi kuandika barua ya kujiuzulu na kuahidi kuongezea zaidi ya Sh 2 milioni alizopewa na akaahidiwa angekutana na Rais Septemba 23.
"Hapa wanamuhusisha Rais wetu kuja Arusha na hii dhambi, hapana tunaomba vyombo vichunguze na kuchukua hatua," amesema Nassari.
Katika ushahidi huo wa sauti, Nassari amerekodi sauti aliyeeleza ni ya mkuu wa wilaya akimpigia simu diwani mmoja siku moja tu baada ya kueleza ana ushahidi wa rushwa, akimuhoji kama alimrekodi.
"Vipi katika yale mazungumzo ulikuwa unanirekodi," alihoji mkuu huyo wa wilaya lakini hata hivyo diwani huyo alijibu kuwa hajawahi kumrekodi.
Hata hivyo, wakizungumza na Mwananchi leo kwa nyakati tofauti viongozi hao waliotuhumiwa na madiwani, walipinga tuhuma hizo na kueleza watajibu baada ya kuziona huku Mnyeti akisema yupo hospitali anaumwa.
"Muda huu nipo hospitali naumwa siwezi kujibu lolote juu ya hizo tuhuma," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri, Kizeri amesema hakuwa katika mazingira mazuri ya kujibu tuhuma ambazo zimetolewa.
"Nina kazi nafanya muda huu siwezi kujibu hayo unayouliza,"amesema.
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Makiba, Emmanuel Mollel alipotakiwa kueleza juu ta tuhuma hizo na yeye kuonekana akijadiliana na viongozi wa Serikali kuhusu kujiuzulu, alikanusha tuhuma za kupewa rushwa.
"Mimi nilikuwa diwani hivyo, kukaa pamoja na Mkuu wa Wilaya, ama mkurugenzi sio tatizo, Nassari amechukua picha za kuunganisha vipande vipande lakini naomba kwanza kutazama hiyo video halafu nitajua cha kusema,"amesema
Amesema Nassari anafanya propaganga akihoji mbona hasemi wamepewa fedha kiasi gani na katika hoja ya kulipwa kiinua mgongo aliomba waende wakaguzi wa mahesabu katika halmashauri kuchunguza kama kuna fedha zimetoka.
Kwa upande Diwani wa Kata ya Sambasha(CCM) Lengai Ole Sabaya ambaye pia ametajwa kuhusika katika njama za kurubuni madiwani hao, alisema bado anatathimini ushahidi huo wa Nassari.
"Kwa sababu nimetajwa nitafanya tathimini kuhusu hizo video na tutatoa majibu kwani ni haki yangu," amesema
Akizungumzia tuhuma hizo, Lema amesema mchezo uliofanyika Meru, ndio ambao umefanyika Arusha Mjini, Monduli, Iringa, Hai na maeneo mengine.
"Wote wanaojiuzulu barua zao zinasema wanamuunga mkono Rais Magufuli, sasa wanaacha kazi watawezaje kumuunga mkono Rais wakiwa nje ya kazi ya uwakilishi wa wananchi,"amehoji
Amesema mpango wa kununua madiwani ni hasara kwa Taifa kwani, wananunuliwa kwa fedha za umma lakini pia zitatumika fedha za umma kufanya chaguzi na kwa wastani uchaguzi wa kata moja unagharimu zaidi ya Sh 1 bilioni.
"Utaona kabisa hii ni mikakati ambayo waliahidiwa madiwani hawa kuwa wakijiuzulu watapewa fursa ya kuja kugombea ndicho ambacho kinapangwa kuja kufanyika,"amesema
Amesema Diwani wa Kata ya Kimandolu alijiuzulu pia baada ya kupewa rushwa ikiwepo ya kufutwa kesi zilizokuwa zinamkabili na vikao vilifanyika eneo ambalo wanajua na walirekodiwa waliohusika.
"Kuna mambo ya hatari sana yanatajwa kwenye video hizi ambayo kama yote tukiyaweka hadharani yataleta mpasuko mkubwa ndani ya Serikali kwani zinatajwa hadi hujuma walizofanyiana viongozi," amesema.Mwananchi
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment