BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CHADEMA YAINGIA RASMI KWENYE MIKIKIMIKIKI NA CCM SINGIDA KASKAZINI

 
NI wazi kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho awali kilitoa tishio la kutosimamisha wagombea katika uchaguzi wa marudio katika majimbo matatu ambayo uchaguzi utafanyika mapema mwakani, kimebadili mawazo na kusimamisha mgombea katika moja ya majimbo hayo.

Uhakika wa chama hicho sasa kujitosa kupambana na wapinzani wao wakuu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) umejidhihirisha kupitia orodha ya vyama iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushiriki uchaguzi katika Jimbo la Singida Kaskazini mkoani Singida.

Katika orodha hiyo, vyama sita vya siasa, kikiwemo cha Chadema, vimepitishwa na NEC kushiriki kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo la Singida Kaskazini uliopangwa kufanyika Januari 13, mwakani.

Hata hivyo, orodha nyingine iliyotangazwa na NEC kwa Jimbo la Longido mkoani Arusha haijamjumuisha mgombea wa Chadema na ACT Wazalendo. Uchaguzi huo pia utafanyika Januari 13, mwakani.

NEC imetangaza kuwa vyama tisa vya siasa katika jimbo hilo la Longido mkoani Arusha ndivyo vilivyojitokeza katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge katika jimbo hilo na kufanikiwa kukamilisha vigezo vya kuwania ubunge, ikiwemo cha kuchukua fomu na kurudisha kwa wakati muafaka.

Katika hatua nyingine, vyama tisa vimejitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mdogo wa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma, huku pia kukiwa hakuna wagombea wa Chadema na ACT Wazalendo.

Jimbo la Singida Kaskazini Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Rashid Mandoa, Chadema ambacho awali kilitangaza kususa chaguzi zote ndogo nchini, hatimaye kimempitisha David Djumbe kutetea bendera ya chama chao katika kinyang’anyiro hicho.

Mandoa alivitaja vyama vingine vya siasa ambavyo vimesimamisha wagombea wao kuwa ni Chama cha AFP mgombea akiwa ni Omari Sombi maarufu kama OMOSO na Chama cha Wananchi (CUF), mgombea akiwa ni Dalphina Mlewa.

Vyama vingine vya siasa na wagombea wao kwenye mabano ni pamoja na CCM (Justin Monko), ADA-Tadea (Aloyce Nduguta) na CCK mgombea wake akiwa ni Mchungaji Yohana Labisu.

Mandoa alisema kuwa licha ya Chama cha NRA na UMD kuchukua fomu, vilishindwa kuingia kwenye mpambano kutokana na kukosa wadhamini huku UPDP na UDP pia vikikosa kushiriki baada ya kushindwa kurejesha fomu za wagombea wao kwa muda uliopangwa.

Mgombea wa CCM, Justin Monko aliahidi kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi ya chama hicho kutokana na kuwa na uzoefu wa kutosha katika nyanja ya utendaji. “Rais wangu Magufuli aliponiteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) imekuwa kama vile kunipeleka kwenye mafunzo.

Sasa nimeiva barabara na nawaahidi wananchi wangu utumishi uliotukuka iwapo watanichagua,” alisema Monko. Hata hivyo, katika hali ya kushangaza mgombea wa Chadema, Djumbe alitoweka ghafla ilipofika zamu yake ya kuhojiwa na waandishi wa habari ili kujua sababu iliyomsukuma yeye kugombea wakati msimamo wa chama chake ni kususa chaguzi zote ndogo nchini.

Akizungumzia kuonekana kwa jina la Djumbe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema chama hicho kinazo taarifa za kutajwa kwa jina la mgombea wake katika Jimbo la Singida Kaskazini lakini alisema ni kutokana na kasoro zilizofanywa na NEC.

“Ni kweli mgombea wetu anasema amesikia Msimamizi wa Uchaguzi ametaja jina lake na hivi tunavyozungumza amekwenda katika kituo cha uchaguzi ili kuonana na msimamizi wa uchaguzi kujua sababu zilizomfanya ataje jina lake bila jina lake kupitishwa na chama.

“Kwa kifupi ni kuwa msimamo wa chama chetu ni kutoshiriki uchaguzi wowote wa marudio kama ilivyoamuriwa na Kamati Kuu,” alisema Mashinji. Jimbo la Longido Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya muda wa kurudisha fomu majira ya saa 10 kufika, Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Longido, Juma Mhina alisema kuwa vyama hivyo tisa vyote vimekidhi vigezo na vimeruhusiwa kuanza kampeni kuanzia jana kwa kufuata ratiba iliyopangwa na NEC katika jimbo hilo na si vinginevyo.

Mhina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido aliwataja wagombea na vyama hivyo kuwa ni pamoja na mgombea wa CCM, Dk Steven Kiruswa. Wengine na vyama vyao kwenye mabano ni Kisiyongo Ole Kunda (CUF), Francis Ringo (CCK), Feruzily Feruzilyson (NRA), Simon Ngilisho (Chama cha Demokrasia Makini- CDM), Godwin Sarakikya (TADEA), Simon Bayo (SAU), Mgina Mustafa (AFP) na Robert Laizer (TLP).

Msimamizi huyo alisema kuwa vyama vyote vilikaa jana kuunda kamati ya maadili kwa ajili ya wagombea wenye kukiuka kanuni na sheria ya uchaguzi, hivyo aliwaasa wagombea wote kuzingatia sheria za tume ya uchaguzi katika mikutano yao ya kampeni na kufuata ratiba iliyopangwa.

Mhina alisema katika Jimbo la Longido lina kata 18 na vituo 175 vya kupiga kura na waliojiandika kupiga kura katika jimbo hilo ni wananchi 57,808 na kampeni zimeanza jana na uchaguzi unaratajia kufanyika Januari 13, mwakani.

Katika urejeshaji fomu kulikuwa na shamra shamra mbali ambapo mgombea wa CCM, Dk Kiruswa aliyesindikizwa na mamia ya wanachama wa mji wa Longido aliwataka wanachama wa chama hicho kufanya kampeni kwa ustarabu, hekima na busara kwa kunadi sera za chama na kusema yale mazuri yanayofanywa na Rais Magufuli.

Dk Kiruswa alisema pia ni wakati wa wana CCM kuungana na kuondoa tofauti zao na kuwashawishi wale wote waliokwenda upinzani kwa kufuata mkumbo. Alisema na kuwataka wana CCM kuhudhuria uzinduzi wa kampeni utakaofanyika Desemba 23, mwaka huu katika uwanja wa mpira uliopo karibu na Kituo Kikuu cha Polisi cha mji wa Longido bila kukosa.

Naye Mgombea wa NRA Feruziyson alisema kuwa vyama vilivyosusa uchaguzi katika jimbo hilo vinaogopa mageuzi na waoga katika demokrasia. Alisema kususa uchaguzi ni kufanya wananchi kutowaamini na kushindwa kuwapa dola hivyo kwa uamuzi uliofanywa na vyama hivyo umetia doa upinzania.

Mgombea wa Demokrasia Makini, Ngilisho yeye alisema chama chake kimejitoa na kushiriki uchaguzi huo kwa lengo la kuonesha kuwa chama hicho kina watu makini wenye kujua demokrasi ni nini.

Ngilisho alisema kamwe chama hicho hakitasusa uchaguzi wa aina yoyote kwani ni chama kinachojitambua na kujua nini maana ya upinzani na kutaka kujitangaza zaidi vijijini kuliko mijini kama baadhi ya vyama vingine.

Jimbo la Songea Mjini Kwa upande wa Jimbo la Songea Mjini, vyama tisa vimejitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mdogo wa nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.


Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Tina Sekambo alivitaja vyama ambavyo hadi jana tayari vilikuwa vimeshajitokeza kuchukua fomu kuwa ni CCM, UPDP, Demokrasia Makini, AFP, TLP, CCK, NRA, ADA na TADEA.

Hata hivyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hadi kufikia jana hakikujitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi huo, ambao unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Leonidas Gama wa CCM aliyefariki dunia mapema mwezi uliopita.

Aidha Sekambo alisema, mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni kesho kabla ya saa 10 na kusisitiza kuwa ofisi yake haitakuwa tayari kutoa na kurudisha fomu baada ya muda huo. 


Habari hii imeandikwa na Abby Nkungu, Singida, John Mhala, Longido na Na Muhidin Amri, Songea.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: