JESHI LA POLISI WAZUNGUMZIA MATUKIO YALIYOIBUKA 2017 IKIWEMO KUPOTEA KWA MWANDISHI AZORY GWANDA KWA SIKU 30 SASA
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa kupotea mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda na mwanachama wa Chadema, Ben Saanane.
Pia, limesema uchunguzi wa kushambuliwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wa tuhuma za uchochezi zinazomkabili Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa unaendelea.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Boaz amesema hayo leo Jumatano Desemba 20,2017 alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Jeshi hilo jijini Dar es Salaam.
"Uchunguzi wa hili la mwandishi mwenzenu unaendelea ziko taratibu ambazo sisi polisi tunapaswa kuzifuata, hivyo muwe na subira wakati tukiendelea," amesema DCI Boaz.
Hadi leo, Gwanda amefikisha siku 30 tangu alipotoweka baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa Kibiti mkoani Pwani.
Kuhusu Saanane aliyepotea tangu Novemba, 2016 Boaz amesema uchunguzi unaendelea.
Ameomba ushirikiano kutoka kwa wananchi akitaka wenye taarifa kuziwasilisha kwao.
DCI Boaz akizungumzia tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Lissu Septemba 7,2017 amesema suala hilo limezungumzwa sana na viongozi wengine na kuomba waachwe ili uchunguzi uendelee. Kuhusu tuhuma za uchochezi anazokabiliwa nazo Lowassa, DCI Boaz amesema kuna taarifa wanaendelea kuzikusanya kwa kuwa kulikuwa na upungufu, hivyo wakikamilisha watachukua hatua zaidi.
Askofu azungumzia kupotea kwa watu
Moshi. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Issac Aman amezungumzia hali ya kupotea kwa watu nchini, akisema kumficha mtu haimaanishi unaziba ukweli.
Askofu Aman alikuwa akijibu maswali ya wanahabari Ijumaa, desemba 15 mwaka huu waliotaka kujua msimamo wake juu ya vitendo vilivyoanza kushamiri vya kutekwa na kupotea kwa watu nchini.
Askofu Aman alienda mbali na kueleza kuwa kutoweka kwa watu sio ajali bali ni mipango ambayo isipofanyiwa kazi, nchi itakuwa inajidanganya ina amani kumbe sio.
Kauli ya Askofu huyo imekuja zikiwa zimepita siku 26 tangu kutoweka kwa mwandishi wa kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) Wilaya ya Kibiti, Azory Gwanda.
MCL ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na tayari wamepaza sauti zao wakitaka mwandishi huyo arejeshwe akiwa salama aendelee na majukumu yake.
Pia kauli ya kiongozi huyo, imekuja zikiwa zimepita siku 365 tangu kutoweka kwa Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Askofu alitoa kauli hiyo baada ya kubariki kanisa jipya la mtakatifu Yudathadei lililopo ndani ya Chuo Kikuu cha Katoliki cha Mwenge (Mwecau) nje kodo ya mji wa Moshi.
“Watu wanatowekaje? Watu wanapotea tu. Wananchi wanashangaa na hata watu wa nje watatushangaa. Watu wanapoteaje kutoka nyumbani? Alihoji na kuongeza;-
“Anaenda nyumbani anafuatiliwa huko halafu anachukuliwa kwenye gari na haonekani tena,” alisema Askofu Aman, mazingira ambayo ndio aliyotoweka mwanahabari Azory.
“Hiyo si ajali hiyo ni mipango ambayo tusipoifanyia kazi tutajidanganya kuwa tunakaa kwa amani. Hiyo sio amani. Hiyo ni cheche ya fujo kwenye nchi,” alisisitiza Askofu.
0 comments:
Post a Comment