WANANCHI WAMTAKA NAIBU MEYA LIDYA MBIAJI KUSHUGHULIKIA KERO YA BARABARA MTAA WA MBUYUNI.
Gari ndogo likinasuliwa kutoka kwenye tope baada ya kukwama na lori la mchanga eneo la mtaa wa Mbuyuni kata ya Kihonda nyuma ya chuo kikuu cha kiislam Morogoro barabara iendayo maeneo ya magoholofa ya Bima mjini hapa ambapo mtaa huo umekuwa na barabara kuu mbili ambazo zimekuwa kero kutokana na halmashauri kushindwa kuzifanyia ukarabati kwa muda mrefu na kusababisha magari kukwama mkoani hapa.
WANANCHI wa mtaa wa Mbuyuni kata ya Kihonda Maghorofani manispaa ya Morogoro wamemtaka naibu meya wa Manispaa hiyo, Lidya Mbiaji, kushughulikia kero ya barabara inayounganisha mitaa ya Mbuyuni na Bima ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa magari na watu wanaopita eneo hilo.
Hata hivyo kwa upande mwingine mwingine kero hiyo imegeuka kuwa ajira kwa baadhi ya vijana wa eneo hilo ambao wamekuwa wakijipatia kipato kwa kusukuma magari yanayokwama katika eneo hilo kwa malipo.
Kwa mujibu wa dereva wa gari lenye namba ya usajiri T420 ANU, Salum Said, barabara hiyo inayopita nyuma ya Chuo Kikuu cha Wailamu Morogoro(MUM) na kuelekea katika maghorofa ya Bima imekuwa kero kubwa kwa wenye magari ambapo wamekuwa wakitozwa kiasi cha Sh5,000 hadi Sh10,000 kwa magari madogo wakati magari makubwa yamekuwa yakitozwa kati ya Sh15,000 hadi Sh20,000 ili kuyanasua.
Said alisema kuwa adha hiyo imemkumba hata yeye baada ya gari lake ndogo kukwama Januari 2 mwaka huu na kutozwa Sh10,000 ili kunasuliwa kwa kuvutwa na lori ambapo awali vijana walishindwa kulinasua gari hilo licha ya kukubaliana kulipa Sh5,000.
Naye mkazi wa mtaa huo, Adam Mwamsele alitaja kero nyingine wanazokumbana nazo wananchi wa mtaa huo na wananchi wengine kuwa ni magari matatu hadi sita kukwama katika eneo hilo kwa wa wiki katika barabara hiyo.
Mwamsele alisema kuwa waendesha baiskeli wamekuwa wakilazimika kuzibeba mabegani ili kuvuka nazo eneo hilo kutokana na matope huku baadhi ya mwenye pikipiki na magari wakitumia umbali mrefu kuepuka bughudha hiyo.
Kwa upande wa Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Lidya Mbiaji akizungumzia juu ya kero hiyo alikiri kuwepo kwa kero hiyo na kudai kuwa tayari mkandarasi wa kufanya marekebisha ya barabara hiyo amepatikana na wakati wowote shughuli za kukarabati eneo hilo itaanza.
0 comments:
Post a Comment