BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAIZER CHIEF FC YAENDELEZA UTEJA LIGI YA TAIFA KUWANIA UBINGWA WA MKOA WA MOROGORO.


Mshambuliaji wa timu ya Kaizer Chief FC, Hassan Timbe kushoto akimtoka mlinzi wa Mpepo FC, Shabaan Togwa wakati wa michezo ya fainali ya ligi ya taifa kuwania ubingwa wa mkoa wa Morogoro katika uwanja wa Jamhuri mkoani hapa katika mchezo huo Kaizer Chief FC ilitandikwa bao 2-0.

TIMU ya soka ya Kaizer Chief FC imeendeleza uteja katika mfululizo wa michezo ya fainali ya ligi ya taifa kuwania ubingwa wa mkoa wa Morogoro kwa msimu wa mwaka 2011/2012 baada ya kukubali kipigo cha pili dhidi ya Mpepo FC kwa bao 2-0 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.

Kipigo hicho ni cha pili tangu kuanza kwa michezo hiyo kufuatia kufungwa bao 1-0 na Mkamba Rangers FC katika mchezo wa ufunguzi kabla ya kukubali kipigo kingine kutoka kwa Mpepo FC cha bao 2-0 na kupoteza michezo miwili ya kuwania ubingwa huo huku ikiwa imebakia michezo mitatu.

Timu ya Kaizer Chief FC walitawaliwa mchezo huo vipindi vyote kwa kutanda soka safi na kufanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa wapinzani wao lakini washambuliaji wake walishindwa mbinu ya kupenya ngome ya wapinzani wao na kufunga mabao huku Mpepo FC wakitumia mbinu ya kushambulia kwa kustukiza katika lango la Kaizer Chief FC ambapo mbinu hiyo iliwasaidia kwa kupata ushindi huo.

Uzembe wa mlinzi wa Kaizer Chief FC, Jobe Ayubu uliwapa faida timu ya Mpepo FC baada ya washambuliaji wake kutumia vema makosa ya mlinzi huyo na kupachika mabao mawili katika dakika ya 44 na 55 ya mchezo huo.

Bao la kwanza la Mpepo FC lililofungwa kiufundi na mshambuliaji, Abdallah Zungu baada ya mlinzi huyu wa Kaizer Chief FC, Jobe Ayubu kushindwa kuondoa hatari akiwa eneo la hatari kabla ya mshambuliaji huyo kuunasa mpira na kupiga shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Kaizer Chief FC,Mashaka Malipula na mpira kutinga wavuni na kwenda mapumzi wakiwa na hazina ya bao 1-0.

Mlinzi huyo wa Kaizer Chief FC alirudia makosa yale yale kwa kushindwa kumdhibiti mshambulia wa Mpepo FC, Abdallah Zungu ambaye alimzidi ujanja na kutoa pasi kwa mfungaji wa bao la pili mshambuliaji, Abasi Athmani aliyefunga kirahisi dakika ya 55 na kufanya mchezo huo kumalizika kwa kufungwa bao 2-0.

Nao mabingwa wa soka Manispaa 2011/2012 timu ya Uhuru Rangers FC ilishindwa kutumia vema nafasi walizopata kwa washambuliaji wake kupachika mabao dhidi ya timu ya The Wailes FC baada ya kutawala mchezo huo na kulazimishwa suluhu tasa ya 0-0 kwenye mchezo mkali uliofanyika majira ya saa 10 jioni kwenye uwanja huo huo wa Jamhuri.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: