RAIS WA AWAMU YA TATU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BENJAMIN WILLIAM MKAPA.
Makada CCM wamnyooshea kidole Mkapa
KITENDO cha Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kutengua matokeo ya ubunge
Jimbo la Igunga yaliyompa ushindi Dk Dalaly Peter Kafumu (CCM), kimeibua
mvutano mwingine ndani ya CCM, ambapo sasa baadhi ya makada wake
wameanza kumnyooshea kidole Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadhi ya
mawaziri kuwa ndiyo chanzo cha kushindwa huko.
Baadhi ya makada
maarufu na wenye uzoefu wa muda mrefu ndani ya chama hicho tawala, kwa
nyakati tofauti kwenye mahojiano na Mwananchi Jumapili wamekiri kwamba,
imefika mahali ambapo CCM inapaswa ijitazame na kuwa makini juu ya watu
inaopaswa kuwatumia katika kampeni zake.
Katika tathmini yao,
makada hao wamemtaja Rais Mstaafu Mkapa na mawaziri kadhaa, wakisema
kuwa CCM haikuwa makini katika kuwateua wasimame kwenye majukwaa kupiga
kampeni za kisiasa. Walitaja moja ya sababu kuwa ni Mkapa na baadhi ya
mawaziri hao mashuhuri kuwa siyo wanasiasa wa jukwaani bali ni
watendaji.
Licha ya CCM kujaribu kumtumia rais huyo mstaafu na
mawaziri hao kutokana na heshima iliyojengeka kwao mbele ya Watanzania
walio wengi, tathmini ya makada hao inaeleza kuwa hoja zao katika
kampeni ama ziliwapa mwanya wapinzani, hasa Chadema kuiumbua CCM kwenye
propaganda za majukwaani, hata kisheria.
Walikuwa wakizungumzia
chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni katika Jimbo la Arumeru na
ule wa Igunga Oktoba mwaka jana, ambao licha ya CCM kushinda, wiki hii
mahakama kuu ilitengua ushindi huo. Kuanguka Igunga Dk Kafumu aliibuka
mshindi kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Oktoba 2, mwaka jana kuziba
nafasi ya Rostam Aziz aliyejiuzulu kwa madai ya kuchoshwa na kile
alichoita siasa za majitaka ndani ya CCM, lakini mahakama imetengua
ushindi wake.
Uchaguzi huo ulikuwa wa ushindani mkubwa kati ya
Dk Kafumu na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye ambaye
aliamua kupinga ushindi wa Dk Kafumu mahakamani akidai hakuridhishwa na
mwenendo wa uchaguzi huo.
Kashindye alifungua kesi hiyo Machi 26, mwaka
huu. Wakati wa kampeni za uchaguzi huo vigogo mbalimbali wa CCM
akiwamo Mkapa walipiga kambi Igunga na kushiriki mikutano mbalimbali ya
kampeni, ambapo pamoja na mambo mengine walitoa kauli tata
zilizosababisha CCM kushindwa katika kesi hiyo.
Mbali na Mkapa
viongozi wengine waliotoa kauli hizo na sasa wananyooshewa vidole ni
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama na
Mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage. Kauli tata ya Mkapa Wakili wa
mlalamikaji, Profesa Abdallah Safari, Agosti 20 mwaka huu aliwasilisha
mahakamani hapo zaidi ya malalamiko 13 dhidi ya Dk Kafumu na wenzake.
Mbali
na kueleza yaliyozungumzwa na Dk Magufuli, Profesa Safari alidai hoja
nyingine ni Baraza la Waislamu (Bakwata) Wilaya ya Igunga kuwakataza
waumini wasiipigie kura Chadema na kwamba naye Rais Mstaafu Benjamin
Mkapa alitoa ahadi ya kugawa mahindi kwa wananchi wa Igunga siku moja
kabla ya uchaguzi ili waichague CCM. Makada waonya
Mbunge wa Kahama, James Lembeli alisema kuwa utaratibu wa sasa wa chama hicho kuwatumia viongozi wastaafu umepitwa na wakati kwa sababu Watanzania wa sasa hawahitaji kusikia maneno mengi, bali sera. Alisema kuwa CCM inatakiwa itazame ilipojikwaa na kuacha kutafuta mchawi kwa kuwa matatizo yaliyokifikisha chama hicho kilipo sasa yanajulikana.
Mbunge wa Kahama, James Lembeli alisema kuwa utaratibu wa sasa wa chama hicho kuwatumia viongozi wastaafu umepitwa na wakati kwa sababu Watanzania wa sasa hawahitaji kusikia maneno mengi, bali sera. Alisema kuwa CCM inatakiwa itazame ilipojikwaa na kuacha kutafuta mchawi kwa kuwa matatizo yaliyokifikisha chama hicho kilipo sasa yanajulikana.
“Kampeni
za CCM hivi sasa hazina maandalizi, kila anayeweza kuzungumza
anachukuliwa na kujumuishwa kwenye kampeni, jambo ambalo siyo sahihi,”
alisema Lembeli na kuongeza:
“Inatumia watu bila kuangalia kama
wanakubalika, katika chaguzi zinazokuja, chama kiwatumie makada
wanaopendwa na wananchi na wenye uwezo wa kuuza sera za chama.”
Alitaja
sababu nyingine ya CCM kuanguka hasa Igunga kuwa ni pamoja na
mgawanyiko uliokuwapo ndani ya chama hicho baada ya baadhi ya makada
kuzuiwa kushiriki katika kampeni hizo wakati wana mvuto kwa wapiga
kura.
Akitolea mfano watu hao alisema kuwa ni pamoja na Mbunge wa
Urambo Mashariki, Samuel Sitta, ambapo alibainisha kuwa waliotoswa
katika kampeni hizo wasingeweza kuishiwa maneno ya kuzungumza na kuanza
kutoa ahadi zinazovunja sheria ya uchaguzi.
Dk Kigwangallah
Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dk Hamisi
Kigwangallah alisema kitendo cha CCM kutumia vigogo akiwamo Rais mstaafu
Mkapa katika uchaguzi wa Igunga, ndiyo chanzo cha kushindwa kwa kesi
hiyo kwa kuwa walizungumza mambo yasiyo na msingi wowote.
Dk
Kigwangallah ambaye Agosti 22 alichukua fomu za kuwania kiti cha
Uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa alisema kuwa uchaguzi mwingine
ukifanyika katika jimbo hilo, viongozi na wabunge kutoka mikoa ya
Tabora, Mwanza na Shinyanga ndiyo waachwe kufanya kampeni.
“Ni
kweli CCM tuliweka watu wengi, ambao walipunguza kura za chama, lakini
pia walizungumza mambo yasiyostahili,” alisema Dk Kigwangallah na
kuongeza:
“Uchaguzi ujao Igunga wasituletee watu kutoka CCM taifa,
wanakuja na helikopta na kutumia gharama kubwa halafu mambo
yanaharabika. Nadhani tubadilishe hali hii.”
Hata hivyo, alisema
kuwa CCM inakubalika kwa kiasi kikubwa mkoani Tabora, hasa katika Jimbo
la Igunga na kwamba kama Dk Kafumu akigombea tena, ataibuka mshindi
kwani anakubalika na alishafanya mambo ya maendeleo.
Ibrahim
Kaduma Kada mkongwe wa chama hicho, Ibrahim Kaduma alipoulizwa iwapo
moja ya sababu za CCM kushindwa ni kuwatumia vigogo ambao siyo mahiri
katika siasa za jukwaani, hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo akitaka
aachwe.
“Naomba uniache kwanza, masuala haya yanatosha …, naomba
uniache tafadhali kwa hisani yako tu,” alisema Kaduma.
Ole Moloimet
Naye Lepilal Ole Moloimet, kada wa CCM aliyewahi kushika nafasi
mbalimbali ndani ya CCM na Serikali, alikilaumu chama chake kwa tabia ya
kumtumia Rais Mstaafu Mkapa na baadhi ya mawaziri kwenye kampeni za
uchaguzi.
Alisema kitendo cha kuwatumia watu hao licha ya
kusababisha wadhalilike kinaonyesha udhaifu wa watu wanaoiongoza CCM
hivi sasa.
"Suala la kuwatumia marais wastaafu, kuwatumia mawaziri ni
udhaifu wa viongozi wa CCM wanaoiongoza hivi sasa," alisema Moloimet.
Akizungumzia uchaguzi wa Arumeru alisema:
“Mkapa alidhalilishwa na
mgogoro wa ardhi wa muda mrefu. …Wananchi walihoji kama alishindwa
mgogoro huo wakati wa utawala wake, akizungumzia suala hilo sasa atakuwa
anawaongopea."
Alisema kimsingi marais wastaafu hawapaswi
kutumiwa kwenye siasa, badala yake iwe ni matukio muhimu yanayohusu
Watanzania wote au juu ya uhusiano wa kimataifa kama vile mgogoro wa
mpaka na Malawi.
"Imefika mahali hawa viongozi wastaafu hata wakiombwa
wakanadi sera majukwaani wao wenyewe wanapaswa wajipime. Si kila kitu
wakubali," alisema Moloimet.
Tuvute subira- Mgeja Hata hivyo,
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja alisema:
“Nadhani
tuvute subira kwa sababu tukianza kunyoosheana vidole nani hakufaa nani
alifaa itakuwa siyo jambo zuri, kama ni hivyo mbona tulivyoshinda Igunga
hawakuwalaumu walioshiriki katika kampeni.”
Lusinde: Hakuna tatizo
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema kuwatumia wazee katika chaguzi za chama hicho hakuna tatizo, akiamini kuwa Jimbo la Igunga ni mali ya CCM na kwamba uamuzi wa kukata rufaa au kutokata anamwachia Dk Kafumu.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema kuwatumia wazee katika chaguzi za chama hicho hakuna tatizo, akiamini kuwa Jimbo la Igunga ni mali ya CCM na kwamba uamuzi wa kukata rufaa au kutokata anamwachia Dk Kafumu.
“Natamani kama uchaguzi ungefanyika tena ili twende tukalichukue jimbo,”
alisema Lusinde.
Sababu za kutenguliwa matokeo Akitoa hukumu
hiyo, Jaji Mary Nsimbo Shangali alisema Mahakama ilipokea malalamiko 15
ambayo yaliridhiwa na pande zote mbili lakini baadaye yakaongezwa madai
mengine mawili hivyo kufikia 17.
Alisema hoja zilizothibitishwa na
Mahakama ambazo zilizotumika kutengua matokeo hayo ni saba kati ya 17.
Baadhi ya hoja hizo ni pamoja madai kwamba Waziri wa Ujenzi, Dk
John Magufuli alitumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa
Daraja la Mbutu, ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa
Jimbo la Igunga.
Jaji Shangali aliikubali hoja nyingine ya washtaki
kuwa ni ugawaji wa mahindi ya kuwawezesha wakazi wa Igunga kukabiliana
na njaa wakati wa uchaguzi huo kwamba ulitumiwa vibaya na baadhi ya
wanasiasa kuwashawishi wananchi wawapigie kura.
Mbali na Dk
Kafumu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uchaguzi walikuwa ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga
aliyetangaza matokeo hayo.
Kauli ya Nape Hata hivyo, Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kwamba haoni kuwa
kauli za Rais Mkapa, Magufuli, Mukama ndizo zilizokiangusha chama hicho
alisema: “Ndiyo maana tunataka kukata rufaa kwa sababu hatukubaliani na
hiyo hoja.”
Vita ya kuwania uongozi
Katika hatua nyingine, upepo wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM umezidi kushika kasi baada ya Mbunge wa Jimbo la Kahama, James Lembeli kuchukua fomu ya kugombea Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga huku akitamba kuwa ameingia kwa lengo la kumaliza makundi ya kisiasa yaliyokithiri ndani ya chama hicho.
Katika hatua nyingine, upepo wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM umezidi kushika kasi baada ya Mbunge wa Jimbo la Kahama, James Lembeli kuchukua fomu ya kugombea Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga huku akitamba kuwa ameingia kwa lengo la kumaliza makundi ya kisiasa yaliyokithiri ndani ya chama hicho.
Lembeli amechukua fomu
sambamba na mpinzani wake mkubwa kisiasa Khamis Mgeja, ambaye kwa sasa
ndiye mwenyekiti wa CCM mkoani humo. Mbali na vigogo hao, mbunge wa
zamani wa Shinyanga mjini Leonard Derefa naye alichukua fomu za kuwania
nafasi hiyo.
Wengine ni Teresia Kashinje, Bonaventure Mguziki,
Regina Masanja na Alex Seseja.
Hata hivyo, katika kinyang’anyiro hicho
wagombea wanaoonyesha kuvutia hisia za wanaCCM wa Shinyanga ni Lembeli
na Mgeja, ambao wamekuwa mahasimu wa siku nyingi katika siasa za mkoa
huo, huku wote wakitoka wilayani Kahama.
Katika majigambo yao
Lembeli amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akitamba kuwa
atahakikisha anamng’oa Mgeja katika nafasi hiyo huku Mgeja naye akidai
hasimu wake huyo ni ‘sisimizi’ ambaye hamnyimi usingizi.
Makada
wengine wa chama hicho waliochukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali ni
pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi CCM Makao Makuu, Matson Chizii ambaye
amejitosa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Dar es Salaam.
Wengine waliochukua fomu za kuwania nafasi hiyo mkoani Dar es Salaam
ni John Guninita anayetetea nafasi hiyo na Mjumbe wa Nec, Ramadhan
Madabida.
Naye Katibu wa Nec, Uchumi na Fedha na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba amejitosa kuwania nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) kupitia kundi la viti 10 wakati Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda akijitosa kuwania nafasi ya NEC kupitia Wilaya ya Lindi Vijijini.
Naye Katibu wa Nec, Uchumi na Fedha na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba amejitosa kuwania nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) kupitia kundi la viti 10 wakati Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda akijitosa kuwania nafasi ya NEC kupitia Wilaya ya Lindi Vijijini.
Aliyekuwa mbunge wa Misungwi, Dalali
Shibiriti naye amechukua fomu ya kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (Nec) kupitia wilaya hiyo.
Uchaguzi huo pia umemwibua
aliyekuwa Mbunge wa Busega, Dk Raphael Chegeni ambapo baadhi ya vijana
wa wilaya hiyo walimchukulia fomu kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) kupitia Wilaya ya Busega.
Mbunge wa Jimbo la Mbozi
Mashariki, Godfrey Zambi naye amejitosa kuwania nafasi ya uenyekiti wa
mkoa wa chama hicho mkoani Mbeya.
CHANZA: MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment