JESHI la Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) pamoja na Jeshi
la Kenya wamethibitisha kupambana na wanamgambo wa al-Shabaab ndani ya
mji wa bandari wa Kismayo, wakidai kukaribia kuuchukua mji huo muhimu
kimkakati.
"Lengo la AMISOM ni kuwakomboa watu wa Kismayo na kuwawezesha kuendelea
na maisha yao kwa amani, utulivu na usalama.
Operesheni zetu
zinaendelea kulenga shabaha maalum za al-Shabaab mjini Kismayo," alisema
Kamanda Andrew Gutti wa AMISOM, akiwataka wapiganaji wote wa al-Shabaab
walio ndani ya Kismayo kuweka chini silaha zao.
Katika hatua nyengine, Jeshi la Kenya limesema kwamba wapiganaji wake
wamelichukua eneo la kusini ya Kismayo, ngome ya mwisho ya kundi la
al-Shabaab.
Msemaji wa Jeshi hilo, Cyrus Oguna, aliliambia shirika la habari mapema
leo kwamba wanajeshi wa Kenya walikumbana na upinzani mdogo wakati wa
kuliteka eneo hilo.
WANAJESHI wa Kenya wanaopigana na al-Shabaab nchini Somalia.
Hata hivyo, wakaazi wa huko pamoja na wanamgambo wa al-Shabaab
wamekanusha taarifa hizo, wakisema kwamba ndio kwanza wanajeshi wa Kenya
walikuwa kwenye viunga vya mbali na Kismayo, ambako wamekuwako kwa
zaidi ya siku nne sasa.
"Maadui wakitumia mashua za kijeshi walituma mamia ya wanajeshi katika
eneo la pwani jana usiku na mujahidina wetu wanakabiliana nao katika
mapigano makali hivi sasa," alisema kamanda wa al-Shabaab, Sheikh
Mohamed Abu Fatuma, akisisitiza kuwa umbali walipo wanajeshi wa Kenya ni
kiasi ya maili sita kutoka Kismayo.
Wakaadhi kadhaa pia wa Kismayo walisema kwamba wanajeshi wa Kenya bado
walikuwa ufukweni, walikotia nanga wakiwa kwenye mashua mbili
zilizosindikizwa na helikota za kijeshi, umbali wa kilomita tano kutoka
katikati ya mji.
"Mji wenyewe bado uko chini ya udhibiti wa al-Shabaab. Radio Andalus
inaendelea kufanya kazi, ikiwataka watu kujitokeza kujiunga na jihadi na
kuwafukuza wavamizi," alisema mmoja wa wakaazi hao, Abdulahi Yakub.
Wanajeshi wa Kenya wanaopigana na al-Shabaab nchini Somalia.
MJI wa bandari wa Kismayo ni ngome kuu ya mwisho mikononi mwa
al-Shabaab, ambao tayari wameshapoteza ngome zao nyengine - ikiwemo miji
ya Afgoye, Baidoa na Marka - kwa kikosi cha wanajeshi 17,000 wa Umoja
wa Afrika, kinachojumuisha pia wanajeshi wa Kenya na Ethiopia.
Jumanne iliyopita (tarehe 25 Septemba) jeshi la Kenya liliushambulia
uwanja wa ndege wa Kismayo kwa ndege za kijeshi, ikiwa ni sehemu ya
operesheni kuu ya kuingia mji huo.
Tangu wanajeshi wa Kenya walipoingia nchini Somalia mwaka jana
kupambana na al-Shabaab, wamekuwa wakilenga kuuchukua mji huo. Lakini
kufikia lengo hilo kumewachukua muda mrefu zaidi kuliko walivyokuwa
wametarajia.
0 comments:
Post a Comment