BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CHIKAWE ASHINDWA KUPATA NAFASI YA HALMASHAURI KUU YA CCM (NEC) WILAYA YA NACHINGWEA LINDI.

NAYE AANGUKA NEC, ALIYEMSHINDA AZIRAI , MNALI ALIYEWATANDIKA WALIMU VIBOKO BUKOBA
 KUONGOZA CCM NACHINGWEA.
article thumbnail


UCHAGUZI wa nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umezidi kuwa mwiba mchungu kwa makada wake maarufu baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kushindwa katika nafasi ya Halmashauri Kuu ya chama hicho (Nec).

Chikawe alishindwa katika uchaguzi huo uliofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye Ukumbi wa Kiwanda cha Korosho, Nachingwea mkoani Lindi baada ya kupata kura 503 dhidi ya 749 za Fadhili Ali Liwaka ambaye alitangazwa mshindi, mgombea mwingine, Lawama Mtonya aliambulia kura 12.

Waziri huyo anaungana na makada wengine maarufu wa CCM kuanguka katika patashika ya kuwania ujumbe wa Nec wengine wakiwa ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye aliyebwagwa na mpinzani wake, Mbunge wa Hanang’, Dk Mary Nagu wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo kupitia Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu aliyeanguka wilayani Tanga.

Wakati waziri Chikawe ambaye pia ni Mbunge wa Nachingwea, akipigwa mwereka, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Singida Vijijini kwa kupata kura 897 kati ya 1,157 zilizopigwa.

Kilichotokea kwa Chikawe, Mnali
Matokeo hayo yalitangazwa huku Liwaka ambaye ni rafiki wa karibu wa Chikawe, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea kutokana na kuzirai wakati akiwa katika chumba cha kuhesabia kura, baada ya kubaini kuwa alikuwa akiongoza kwa kura nyingi.

Akizungumza kwa simu Liwaka ambaye mpaka jana mchana alikuwa hajaruhusiwa kutoka hospitalini, alisema hakutegemea kama angeshinda kwa kuwa nafasi hiyo ilikuwa ikiwaniwa na mpinzani wake ambaye licha ya uzoefu alionao katika siasa, pia ni Waziri.

“Nilipata mshtuko. Sikuamini kama nimemshinda Chikawe, kwanza ni mzoefu kuliko mimi na pia ni kiongozi wa siku nyingi, lakini ni mtu wangu wa karibu, nawashukuru walionichagua,” alisema Liwaka.

Wakati Liwaka akishangilia ushindi wake huku akiwa amelala kitandani, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali na baadaye kuvuliwa madaraka na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kuwacharaza viboko walimu, aliibuka kidedea katika nafasi ya Uenyekiti wa CCM Wilaya ya Nachingwea.

Katika tukio hilo lilitokea mwaka 2010, Mnali alimwamuru polisi kuwachapa viboko walimu wa shule tatu za msingi zilizopo Wilaya ya Bukoba kwa sababu wilaya hiyo ilikuwa ya mwisho katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Walimu waliocharazwa viboko walitoka katika Shule za Msingi Katerero, Kanazi na Kansenene.

Alipohojiwa kuhusu hatua hiyo, alisema alilazimika kuwatandika viboko walimu hao baada ya kugundua kuwa ni wazembe kazini, ikiwamo kuchelewa kufika katika maeneo yao ya kazi na kutofundisha kama mikataba yao ya ajira inavyosema.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo wa juzi, Mnali alipata kura 970 na kumshinda aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Mohamed Kamlo aliyepata kura 74 huku Fadhili Mkuti akipata kura 246.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Mnali alisema atahakikisha anajenga nidhamu ya chama kwa watendaji wote lakini akasema hatatumia viboko kama alivyofanya mkoani Kagera.

“Nitajenga nidhamu ya chama kwa njia ya majadiliano siyo viboko, kabla ya uchaguzi mkuu ujao, nitahakikisha kuwa nasimamia nidhamu kwa watendaji wote ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano,” alisema.

Singida Vijijini
Mkoani Singida, Hanje Barnabas alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida Vijijini kwa kupata kura 607, akifuatiwa na Mwiru Juma (480) na Sima Luther (51).

Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini, aliwashinda Dafi Bulali (131), Manase Sabasaba (102) na Juma Athuman (27).

Msimamizi wa uchaguzi huo, Mosses Matonya aliwatangaza washindi watano wa Ujumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kuwa ni Monko Justine, Mwalimu Mlozi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Amani Nyekele, Rehema Majii na Aziza Kiduda... 

“Walioshinda Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ni Manase Sabasaba, Jumanne Salum, Daud Elias na Hilda Lazaro.”
Alisema wajumbe wa Halmashauri ya Wilaya kupitia kundi la Wanawake ni Amina Mweri, Hilda Lazaro, Neema Matiti na Zuwena Mohammed.

Zainab Vullu apita Pwani
Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu alifanikiwa kutetea nafasi yake ya Uenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani, huku mbunge wa zamani Kibaha Mjini, Dk Zainab Gama akishindwa katika nafasi ya mjumbe wa Baraza Kuu la Halmashauri ya Mkoa.

Vullu ambaye alikuwa akichuana vikali na Daktari wa Kituo cha Afya Kibaha, Dk Maselina Kuandikwa, alipata kura 261 dhidi ya 157 za mpinzani wake.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Abdillahi Mihewa alisema ushindi huo umepatikana baada ya wajumbe 418 kupiga kura.

Mihewa ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam aliwataja walioshinda ujumbe wa mabaraza na wilaya watakazowakilisha katika mabano kuwa ni Mwajabu Kingwande (Rufiji), Hilda Mazengo na Saida Pazi (Mkuranga), Zakia Hatibu na Saada Amor (Mafia), Upendo Shija na Sofia Sheli (Kisarawe).

Wengine ni Mwajuma Ramadhani na Zuhura Ramadhani (Kibaha Vijijini), Catherine Makungwa na Asnati Jeremia (Kibaha Mjini), Nasi Mutalemwa na Shumira Rashid (Bagamoyo).

Walioshinda uwakilishi Jumuiya ya Wazazi ni Moshi Mkaramo, UVCCM mkoa ni Latifa Kasim, mkutano mkuu mkoa ni Latifa Mwijuma na Halisi Kaijage ambaye ameshinda ujumbe wa mkutano mkuu taifa.

Akifungua uchaguzi wa huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza aliwataka wajumbe kuwa mfano wa kuigwa katika kufanya kazi na kujitolea na kwa moyo wote ili kukijenga chama.

Tafrani Longido
Tafrani iliibuka juzi katika uchaguzi wa CCM wilayani Longido mara baada ya wajumbe wa mkutano wa uchaguzi huo kukataa uamuzi wa kupitisha kwa nguvu jina la mbunge wa jimbo hilo, Lekule Laiser kuwa mjumbe wa Nec wakidai kwamba hakupata kura zilizovuka idadi ya asilimia 50 hali iliyosababisha uchaguzi kukwama.

Uchaguzi huo ambao ulimalizika saa 4:30 ulijaa kila aina ya vituko kikiwamo cha jenereta iliyokuwa ikizalisha umeme kuzimika ghafla wakati wa kuhesabu kura za nafasi ya Mjumbe wa Nec.

Tukio jingine ni baada ya wajumbe kutoka Kata ya Tingatinga kupiga kura wakiwa ndani ya basi nje ya ukumbi huo sanjari na ofisa wa Serikali ambaye alikuwa wakala wa Laiser, Lee Loleukaa kuhudhuria uchaguzi huo kitendo kilichopingwa vikali na baadhi ya wajumbe.

Kitendo cha makatibu 17 wa kata mbalimbali ambao walihudhuria mkutano huo kuitwa nje ya ukumbi na kuelekea kusikojulikana wakati uchaguzi ukiendelea, nacho kiliibua gumzo na kuzua hofu kwamba huenda walikwenda kuwekwa sawa.

Kinyang’anyiro kikubwa katika uchaguzi huo kilikuwa baina ya Laiser aliyepata kura 417 na Peter Mushao aliyepata kura 381 huku wakimwacha mgombea mwingine Michael Siokilo akiambulia kura 51.

Upigaji kura ulianza saa 7:00 mchana huku idadi ya wapiga kura katika uchaguzi huo awali ikitangazwa kuwa 815, lakini ghafla ilibadilika na kutangazwa 871.

Baadhi ya taarifa zinadai kwamba kulikuwa na wajumbe 110 kutoka katika Kata ya Mundarara anayotoka Laiser waliohudhuria ilhali walipaswa kuwa 77 ikidaiwa kuwa waliletwa kwa lengo la kuimarisha ushindi wake.

Hata hivyo, vyanzo vya habari kutoka ndani ya uchaguzi huo vimedai kwamba ilipotimu saa 1:30 usiku baada ya wajumbe wa mkutano huo kupiga kura ya kumchagua mjumbe wa Nec, kura hizo zilichukuliwa na kupelekwa katika chumba kimojawapo kilichopo nyuma ya ukumbi.

Taarifa zimedai kwamba kitendo hicho kiliwashangaza baadhi ya wajumbe ambao waliamua kufuatilia tukio hilo. Walipoingia ndani ya chumba hicho walishuhudia kura hizo zikihesabiwa kwa tochi za mkononi na mara waliposogelea karibu walitimuliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni maofisa wa Usalama wa Taifa.

Kura hizo ziliporudishwa ukumbini na wajumbe kutangaziwa kwamba hakuna mshindi kwa kuwa hakuna aliyevuka asilimia 50, ndipo zilipofanyika juhudi za kupitisha kwa nguvu jina la Laiser lakini wajumbe wa mkutano huo walipinga.

Baada ya vuta nikuvute kudumu ndani ya ukumbi huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Longido, Esupat Naikara alitangaza ya kwamba uchaguzi wa nafasi ya mjumbe wa Nec itarudiwa lakini kwa kuwa hawana fedha za uchaguzi, hawataweza kutangaza tarehe ya uchaguzi.

Habari hii imeandikwa na Christopher Lilai na Mwanja Ibadi (Nachingwea), Gasper Andrew (Singida) na Julieth Ngarabali (Pwani).
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: